Kuna tabia moja ambayo watu wengi wanayo, tabia hiyo ni kutaka kuonewa huruma kutokana na matatizo na changamoto ambazo wanapitia.

Unakuta mtu ameshindwa kukamilisha kitu ambacho alipaswa kukamilisha, lakini anataka watu wamwonee huruma kwa sababu ya changamoto zake.

Unakuta mtu ni mfanyabiashara, ameshindwa kutimiza mahitaji ya mteja wake au kutimiza ahadi aliyompa mteja, lakini anaanza kumweleza ni kwa namna gani kazi yake ni ngumu, au namna gani amekazana kufanya kitu hicho. Unaweza kuona mteja anakusikiliza na kukuonea huruma namna unavyokazana, lakini akitoka hapo ataenda kutafuta mtu wa kumtatulia tatizo lake bila ya kumweleza matatizo yake. Kwa sababu anachotaka yeye siyo hadithi za matatizo ya watu, bali ni kutatua matatizo yake yeye.

Hata kama umeajiriwa, usitumie matatizo yako kama sehemu ya kupata huruma kwa wateja wako au mwajiri wako. Hakuna mtu anataka kusikia matatizo yako, watu wanachotaka kusikia ni namna gani unatekeleza kile ulichowaahidi, au wanachotegemea kupata kutoka kwako.

Hivyo leo nataka nikuambie kitu kimoja mwana mafanikio, unaweza kutafuta huruma ya aina hii popote unapoitaka, lakini siyo kwenye kazi yako wala biashara yako. Usitake kutafuta huruma kwa mteja wako, au mwajiri wako. Kama kuna kitu ulitegemewa kufanya, na umeshindwa kufanya, kiri umeshindwa na omba radhi, kisha fanya. Hakuna mtu anataka kusikia ni kwa kiasi gani kazi yako ni ngumu kwako, au majukumu yako ni mengi. Watu wamekuja kwako kwa sababu wana shida zao, na wanaamini wewe utawatatulia, hawana muda na shida zako wewe.

Moja ya siri kubwa unayopaswa kujua kuhusu watu, ili uweze kufanikiwa ni kwamba watu ni wabinafsi. Kila mtu ni mbinafsi, tunachotofautiana ni kile kiwango cha ubinafsi wetu. Watu wanayafikiria zaidi matatizo yao kuliko matatizo yako. Hivyo ukiwa mtu wa kuwapa matatizo yako badala ya kuwapa suluhisho la matatizo yao ambacho ndiyo kitu walitegemea kutoka kwako, unawapoteza.

Kuwa mtu wa kufanya, kuwa mtu wa kuweka matatizo yako pembeni na kuweka juhudi kuhakikisha unatimiza kile ambacho umeahidi na unategemewa kukamilisha. Kama utashindwa, usitafute sababu ya kuonewa huruma, badala yake kubali kwamba umeshindwa kukamilisha kama ilivyotegemewa na anza kufanyia tena kazi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK