Habari za asubuhi ya leo rafiki?
Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Tumepata nafasi nyingine nzuri na ya kipekee ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora zaidi.

Tukumbuke kuweka juhudi kubwa siku hii ya leo ili kuweza kupata matokeo bora kwa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu kutengeneza habari zako mwenyewe.
Tunaishi kwenye dunia ya habari masaa 24, muda wote kuna habari zinakuzunguka, kabla hujalala kuna habari nyingi zinakusubiri uzipitie, na hata unapoamka zipo habari zinakuaubiri kwa hamu.
Na kwa bahati mbaya sana, habari hizo huna haja ya kuzifuata mbali, zipo hapo kwenye kiganja chako, kwenye simu yako janja.
Watoa habari wamekugeuza wewe kama mtaji wao, kama bidhaa ambayo wanaiuza watakavyo kwa wengine.
Wanachofanya ni kukunasa wewe, kwenye habari zao ambazo hazina umuhimu kwako ili waweze kukuuza kwa watangazaji.
Hii ni hatari sana kwako kwa sababu unapoteza muda wako wa kufanya makubwa, na pia unajazwa hofu ambazo siyo halisi.
Hivyo kwako rafiki yangu na mwanamafanikio, leo nakuambia uache kufuatilia hizi habari ambazo zinashika hisia zako, lakini hazina manufaa kwako.
Badala yake utengeneze habari zako wewe mwenyewe, habari unazotaka kuzisikia, habari zinazokupa hamasa ya kuweka juhudi zaidi na zinazokupa hamasa ya kuchukua hatua.
Zipo kelele nyingi, usikimbikie kuwa sehemu ya kelele hizo, badala yake tengeneza habari zako, na zifuatilie hizo.
Habari zako unaweza kuzitengeneza kwa kuanza siku yako kwa kujisomea vitabu vizuri vinavyokupa maarifa na hamasa ya kufanikiwa zaidi.
Pia unaweza kujifunza kupitia wale waliopiga hatua zaidi kwenye mafanikio.
Muhimu sana ni wewe uweze kudhibiti kile unachosikia na unachofuatilia, acha kuwa mteja wa habari ambazo hazina manufaa kwako.
Nakutakia siku njema sana ya leo rafiki yangu.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
Success Coach, Author and Entrepreneur
Blogs; http://www.amkamtanzania.com and http://www.kisimachamaarifa.co.tz
SUCCESS IS YOUR BIRTHRIGHT