Ustoa ni falsafa ambayo inawapa watu maarifa na namna sahihi ya kuishi, namna ya kuenda na sheria za asili na kuwa na maisha yenye furaha. Kwa mfano moja ya mambo ambayo yanasisitizwa kwenye falsafa hii ni kujua mambo ambayo yapo ndani ya uwezo wako na yale ambayo yapo nje ya uwezo wako. Ukishajua hivyo, jambo lolote linapokutokea, unajiuliza lipo ndani ya uwezo wako au la. Kama lipo ndani ya uwezo wako chukua hatua, na kama lipo nje ya uwezo wako basi achana nalo au kama huwezi kuachana nalo basi angalia namna ya kuishi nalo.
Falsafa hii pia inasisitiza kwamba hakuna kitu kizuri wala kibaya, bali mawazo yetu ndiyo yanafanya kitu kiwe kizuri au kibaya. Kwa asili kila kitu kinatokea kwa sababu, na sababu zetu tunazoweka kwenye vitu hivyo ndiyo zinazoleta maana ya kitu kutokea.
SOMA; Je Haya Unayoishi Ndio Maisha Yako Halisi?
Kitu kingine ambacho falsafa hii inasisitiza na kutufundisha ni kufurahia na kuthamini kitu wakati unacho, kabla hujakipoteza. Kwa falsafa hii ni kwamba chochote ambacho unacho sasa, siyo chako bali umeazimwa kwa muda, na ipo siku kitachukuliwa kutoka kwako. Hii inaanza na wale watu unaowapenda, wazazi, watoto, ndugu, marafiki. Pia mali yoyote unayomiliki, umepewa kwa muda tu. Kwa kuthamini vitu hivi wakati vipo, vitakapoondoka hutaumia sana. Kwa mfano, kwa kuwapenda watu wa muhimu wakati wapo hai, na kuhakikisha kila muda unaoupata kuwa nao unautumia vizuri, siku wakifa hutaumia sana. Tunaumia pale watu wanapokufa kwa sababu kuna vitu tunakuwa hatukufanya nao au kwao na tulidhani wataendelea kuwepo. Kwa falsafa ya ustoa, ni ujinga kulia na kuhuzunika pale mtu anapokufa, kwa sababu kufanya hivyo ni sawa na kulazimisha watu waishi milele, kitu ambacho hakiwezi kutokea. Hivyo ni vyema kutumia muda ulionao sasa, kufanya kila unachotaka kufanya na wale watu wa muhimu kwako, ili watakapoondoka usiumie kwa kuona bado ulikuwa hujafaidi kuwa nao.
Falsafa ya ustoa imekuwa inaonekana kama ni falsafa ya watu wasio na hisia, watu wanaoficha hisia zao na kupuuza kila jambo. Lakini hivi sivyo ilivyo, wastoa badala ya kukubali kuendeshwa na hisia zao, wao wanaendesha hisia zao.
Falsafa hii ilikuwa maarufu sana enzi za utawala wa Roma na iliwawezesha watu kuwa na maisha bora kupitia falsafa hii. Baadaye ilikuja kupotea baada ya wale waanzilishi na waendelezaji wa mwanzo kufariki. Lakini miaka ya hivi karibuni, imekuwa ni falsafa inayofuatiliwa na wengi, kwa sababu inaendana sana na changamoto za maisha ya sasa. Mimi binafsi naweza kujiita mwanafalsafa wa Ustoa kwa sababu nimekuwa nanifunza mengi kupitia falsafa hii na kuweza kuendesha maisha ambayo siyo ya kuyumbishwa yumbishwa katika zama hizi. Mwanafalsafa
Seneca amekuwa ni mtu ambaye namsoma na kujifunza mengi kutoka kwake, kwanza alikuwa mwandishi na ameandika mengi sana na pia alikuwa ni mtu mwenye busara kubwa, aliyekuwa akishauri watawala wa roma. Na kikubwa ambacho wengi wamekuwa wakishindwa kukielewa ni kwamba alikuwa tajiri mkubwa, licha ya kuonekana kwamba falsafa hii haihamasishi watu kuwa matajiri, lakini inaonesha ukifuata falsafa hii, unajikuta unaishia kuwa tajiri hata kama siyo lengo lako kuu.
SOMA; Hii Ndio Siri Kubwa Kuhusu Maisha Ambayo Mpaka Sasa Hujaijua.
Epictetus alikuwa mmoja wa wanafalsafa wa ustoa na pia mwalimu aliyefundisha ustoa. Yeye binafsi hakuandika vitabu, ila mafundisho yake yalikusanywa na wanafunzi wake na kukapatikana vitabu kadhaa. Moja ya vitabu hivyo ni kile tunachokwenda kukichambua leo, kina miongozo ya maisha bora, yenye furaha na mafanikio makubwa.
Karibu ujifunze miongozo na kama utapenda kujifunza zaidi ustoa wasiliana na mimi kwa wasap, 0717396253. Karibu tujifunze kwa pamoja falsafa hii ya maisha ambayo iliwawezesha wengi kupambana na changamoto zao na hata sasa wengi wanaitumia kuboresha maisha yao.
Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu cha EPICTETUS;
1. Kuna vitu ambavyo vipo ndani ya uwezo wetu, na kuna vitu ambavyo havipo ndani ya uwezo wetu. Vilivyopo ndani ya uwezo wetu ni maoni yetu, hisia zetu, tamaa zetu, hofu zetu na matendo yetu. Ambavyo havipo ndani ya uwezo wetu ni mazingira yetu, mali zetu, sifa zetu, na vitu wanavyofanya wengine. Ukitaka kuwa na maisha bora, dhibiti vilivyopo ndani ya uwezo wako na angalia namna bora ya kwenda na vile ambavyo havipo chini ya uwezo wako, usijaribu kuvidhibiti.
2. Kamwe usiendeshwe na tamaa zako, kuendeshwa na tamaa ni kuwa mtumwa wa maisha yako.
3. Sema kile ambacho nataka kusema juu ya kitu au watu. Kama ni mtu unampenda, mwambie unampenda na fanya yale ya kuonesha mapenzi yako kwa mtu huyo. Fanya hivyo kwa nafasi unayopata sasa ili ikitokea hupati tena nafasi usijutie.
4. Weka akili yako yote kwenye kile kitu ambacho unakifanya. Usifanye kitu fulani huku mawazo yako yapo kwenye vitu vingine.
5. Kinachokukasirisha wewe siyo kile kinachotokea, bali tafsiri yako kwenye kile kinachotokea.
6. Usifurahie ukuu ambao siyo wa kwako, ukuu usio wako utaondoka kama ulivyokuja.
7. Popote unapokuwa, kumbuka kusudi lako kuu, usibabaishwe na mambo mengine na kusahau kusudi lako kuu.
8. Usilazimishe mambo yatokee kama unavyotaka wewe, yaruhusu mambo yatokee kama yanavyotokea yenyewe na maisha yako yatakwenda vizuri.
9. Ugonjwa unaathiri mwili wako na siyo utu wako labda mpaka uamue hivyo. Chochote kibaya kinachotokea kwako, kumbuka utu wako unabaki kuwa huru. Usikubali kupoteza uhuru wako.
10. Chochote kinachotokea kwenye maisha yako, jiulize una uwezo gani wa kupambana na kitu hicho. Na kama huwezi kukikabili moja kwa moja, utajifunza uvumilivu.
11. Usiseme umepoteza kitu, bali sema nimekirudisha kwa wenyewe, kwa kuwa kila ulichonacho siyo mali yako ya kudumu, bali umepewa utumie kwa muda, ipo siku kitarudi kilipotoka. Hivyo tumia vizuri kila ulichonacho sasa.
SOMA; Hizi Ndizo Sababu Zinazopelekea Watu Kukata Tamaa Ya Maisha.
12. Kama unataka kuwa na maisha bora, acha kuyashikiza maisha yako kwenye vitu. Kwa mfano usifikiri kwamba kama utakosa kila ulichonacho sasa basi ndiyo mwisho wa maisha yako, jua vitu vinakuja na kuondoka, lakini wewe utaendelea kubaki, mpaka mwisho wako utakapofika.
13. Kama unataka kupiga hatua, waache watu wakuone wewe ni mjinga na hujui unachofanya. Hawatakusumbua kwa lolote mpaka siku wanashangaa umefanya makubwa.
14. Ni upumbavu kufikiri wazazi wako, watoto wako na watu wengine wa karibu kwako wataishi milele. Kuhuzunika sana pale wanapoondoka ni kutaka wangeishi milele, kitu ambacho hakiwezekani.
15. Kila kitu fanya kwa kiasi, wakati mwingine puuza vitu ambavyo siyo muhimu kwako. Usiwe mtu wa kuongea sana, usijiingize kwenye mabishano yoyote.
16. Unapokutana na mtu mwenye huzuni na majonzi, mpe moyo kwa huzuni yake, lakini usikubali akuingize na wewe kwenye huzuni hiyo.
17. Kumbuka wewe ni mwigizaji kwenye filamu ya maisha yako, kila tukio ni wewe unaamua liweje, fupi au refu, utapewa matukio mengi ya kuigiza katika kipindi cha maisha yako, mazuri na mabaya, yote yaigize vizuri.
18. Usijiingize kwenye mashindano yoyote ambayo ushindi haupo chini ya uwezo wako. Na usiwe na wivu na ushindi wa wengine.
19. Kumbuka anayekutukana siyo anayetoa tusi, bali wewe mwenyewe kwa tafsiri ya neno hilo ambalo ni tusi. Ukipuuza chochote hakiwezi kukuumiza.
20. Chochote ambacho unahofia kwenye maisha yako, kifanye kwenye maisha yako. Kama unahofu ukikosa mali zako utakuwa na maisha magumu, jaribu kuyaishi maisha magumu, utaona siyo ya kutisha kama ulivyofikiri.
21. Kama umechagua kuishi falsafa na kuwa mwanafalsafa, iandae kudhihakiwa na kudharauliwa na wengine ambao hawaishi falsafa. Utakapoendelea na falsafa yako, wale waliokudharau na kukudhihaki, watakuja kwako kuomba uwasaidie kwa namna falsafa itakavyoyafanya maisha yako kuwa bora.
22. Ukishajiona unafanya kitu ili kuwaridhisha wengine, jua tayari umeshapoteza maisha yako.
23. Wale unaofikiri wanakuhitaji sana wewe, kwamba bila ya wewe hawawezi kuishi, wataishi vizuri tu bila ya wewe. Hivyo hivyo, usijidanganye kwamba bila ya fulani huwezi kuishi, unaishi vizuri kabisa, usiwe mtumwa.
24. Usione wivu pale mtu mwingine anapopewa heshima kuliko wewe, kuna namna ambavyo wamegharamia heshima hiyo. Waheshimu pia na kama unataka heshima kama yao, lipa gharama waliyolipa wao.
25. Ni rahisi kuona mambo ni ya kawaida pale yanapotokea kwa wengine, lakini siyo ya kawaida pale yanapotokea kwako. Mfano mtu akifiwa ni rahisi kusema kila mtu atakufa, ila ukifiwa wewe unasema unaumia sana. Yape mambo yote uzito sawa.
26. Asili (nature) haileti jambo lolote baya duniani.
27. Kuwa na namna unavyoyaendesha maisha yako ya kila siku, namna unavyokula, unavyofikiri, unavyofanya kazi zako. Usifanye mambo kama ajali, kuwa na utaratibu unaoufuata kila siku.
28. Jinsi unavyokuwa mwangalifu utembeapo usije ukajikwaa, ndivyo unavyopaswa kuwa mwangalifu kwenye akili yako na mawazo yako. Kujikwaa kwa mawazo kuna madhara makubwa kwenye maisha yako.
29. Ni kupoteza kipaji chako pale unapotumia muda mwingi kwenye mwili wako kuliko kwenye akili yako. Kula sana, kunywa sana na hata kufanya mapenzi sana kuliko unavyoitumia akili yako, ni kuharibu maisha yako.
30. Kama mtu anakufanyia mabaya au anakunenea mabaya, kumbuka anafanya hivyo kwa sababu hicho ndiyo anaamini ni sahihi kwake. Mtu anayekufanyia mabaya naye amefanyiwa mabaya hivyo anaamini kufanya mabaya ni sehemu ya maisha. Achana naye na asikuvuruge.
Yapo mengi sana ya kujifunza kupitia kitabu hichi na hata kupitia falsafa ya ustoa kwa ujumla.
Nakusihi ujifunze zaidi kuhusu falsafa hii na uchague kuishi kwa misingi yake, utaweza kuwa na maisha bora sana. Kama ungependa kujifunza zaidi juu ya falsafa ya ustoa, wasiliana nami kwa wasap 0717396253.
Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.
Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita