Kila mtu ambaye yupo makini na fedha, anataka kufikia uhuru wa kifedha na utajiri, basi uwekezaji ni kitu cha lazima kufanya. Siyo kitu cha kujaribu na wala siyo kitu cha kuangalia kama unaweza, bali ni kitu ambacho unapaswa kujifunza, kukijua kiundani na kuwekeza.
Hii ni kwa sababu kadiri umri wetu unavyokwenda, nguvu yetu ya kufanya kazi inapungua. Kwa mfano kijana wa miaka 30, anaweza kufanya kazi kwa muda mrefu na kwa nguvu zaidi kuliko mtu mzima wa miaka 50. Lakini vijana wengi wamekuwa hawafikirii hili, hivyo wamekuwa wakifikiri wataweza kufanya wanachofanya sasa milele. Katika ule wakati ambao nguvu za kufanya kazi zimepungua, ndiyo wakati wa kunufaika na uwekezaji ambao mtu anakuwa amefanya kwenye maisha yake.
Kadiri mtu anavyoanza uwekezaji mapema kwenye maisha yake, ndivyo manufaa yake yanavyokuwa makubwa baadaye. Hii ni kwa sababu kadiri uwekezaji unavyokaa muda mrefu, ndiyo unavyokusanya faida kubwa na kuwa na malipo makubwa sana. Hii ni kwa uwekezaji wa kila aina.
Kwenye makala yetu ya leo ya uwekezaji, tutakwenda kujifunza jinsi ya kuchagua uwekezaji unaokufaa wewe kulingana na mahitaji yako, na hata pale unapoanzia.
Kabla hatujaangalia jinsi ya kuchagua uwekezaji, kwanza ni vyema tukajua aina za uwekezaji ambazo zipo.
Zipo aina nyingi za uwekezaji, lakini tunaweza kuzigawa kwenye makundi makubwa matatu;
SOMA; Uwekezaji Kwenye Soko La Hisa na Hisa Za Vodacom
Kundi la kwanza ni uwekezaji kwenye mali.
Katika kundi hili la uwekezaji, mtu anaweza kuwekeza kwa kumiliki mali ambazo zinaweza kumzalishia sasa na hata siku zinazokuja. Mali hizi zinaweza kuwa mashamba, viwanja, nyumba na majengo ambayo yanaweza kutumika kwa shughuli mbalimbali.
Katika kundi hili la uwekezaji kwenye mali, kuna aina nyingi sana za uwekezaji, kwa mfano kwenye majengo, mtu anaweza kuwekeza kwenye majengo ya makazi, au majengo ya hoteli, biashara, magodowni na kadhalika.
Uwekezaji huu unahitaji kiasi kikubwa cha kuanzia, na pia inachukua muda mrefu mpaka kuweza kurejesha kiasi kilichowekezwa. Lakini huu ni uwekezaji ambao thamani yake inaendelea kupanda kadiri siku zinavyokwenda.
Thamani ya ardhi na majengo mara nyingi sana imekuwa inaongezeka na siyo kupungua. Hivyo mtu anaweza kununua ardhi au jengo na kadiri siku zinakwenda thamani yake ikaongezeka sana.
Kundi la pili ni uwekezaji kwenye masoko ya mitaji.
Huu ni uwekezaji ambapo mtu ananunua na kumiliki sehemu ya masoko ya mitaji. Uwekezaji huu unahusisha hisa za makampuni ya umma, vipande vya mifuko mbalimbali na hata hatifungani zinazotolewa na makampuni au taasisi za kiserikali.
Katika uwekezaji huu, mtu anawekeza fedha yake kwenye kampuni au taasisi mbalimbali, zenyewe zinafanya kazi na hatimaye mtu anapata faida kutokana na gawio au pale hisa au vipande vinapoongezeka thamani.
Huu ni uwekezaji ambao unaweza kuanza na kiasi kidogo cha fedha na kuendelea kuwekeza kadiri siku zinavyokwenda. Ni rahisi kuchukua fedha zako kwenye uwekezaji huu kwa muda mfupi ukilinganisha na uwekezaji kwenye majengo na ardhi.
Changamoto ya uwekezaji huu ni kuathiriwa na kuyumba kwa uchumi. Mabadiliko yoyote ya kiuchumi, huanza kuathiri uwekezaji kwenye masoko ya mitaji, hasa uwekezaji wa hisa. Pia iwapo kampuni au taasisi itapata hasara au kufilisika, basi wewe kama mwanahisa unakuwa umepoteza uwekezaji wako. Tofauti na uwekezaji wa mali, ambao ni vigumu sana kupoteza uwekezaji wako kabisa.
Kundi la tatu ni uwekezaji kwenye biashara.
Hapa mtu anawekeza kwenye biashara ambazo labda anafanya yeye mwenyewe, au zinafanywa na watu wengine. Mtu anaona fursa ambayo biashara fulani inayo, na anakwenda kuwekeza pale. Hizi ni zile biashara ambazo hazimtaki mtu kusimamia kwa karibu sana au kuwepo pale kwa muda mrefu. Mtu anawekeza mwanzoni na baada ya hapo anaendelea kufurahia matunda ya uwekezaji wake.
Changamoto ya uwekezaji huu ni kuathiriwa kwa biashara kunaathiri uwekezaji ambao mtu ameufanya. Pia kama biashara zinaendeshwa na wengine, makosa yao yanaweza kupelekea mtu kupoteza uwekezaji wake.
Baada ya kujua makundi haya ya uwekezaji, swali muhimu ni uwekeze wapi? Hasa kama ndiyo unaanza, upi uwekezaji unaokufaa wewe kulingana na mahitaji yako?
Kama ilivyo kwa kila jambo, hakuna uwekezaji mmoja ambao unamfaa kila mtu. Kwa sababu kila mtu anaanzia sehemu yake yeye, na ana mahitaji yake, basi uwekezaji unatofautiana kati ya mtu na mtu.
SOMA; Uwekezaji Muhimu Kwako Kufanya Na Unaolipa Sana.
Hivyo katika kuchagua uwekezaji, zingatia haya yafuatayo;
- Ndoto kubwa za maisha yako.
Unakwenda wapi na maisha yako ndiyo kitu cha kwanza kabisa ambacho kitakuongoza kwenye uwekezaji wako. Unapokuwa na malengo na mipango ya muda mrefu kwenye maisha yako, lazima uwekezaji wako pia uwe wa muda mrefu. Hivyo angalia unajiona wapi miaka 5, 10, 20 na hata 50 ijayo. Unapowekeza usiangalie tu leo na kesho, bali angalia miaka mingi ijayo.
Kama wewe bado ni kijana, chini ya miaka 40, uwekezaji wako lazima uangalie miaka 30 na kwenda mbele. Wekeza kwenye maeneo ambayo miaka 20 ijayo yatakuwa na faida na kuweza kukunufaisha zaidi.
Kama umri wako ni miaka 50 na kuendelea, uwekezaji wako inabidi ulenge kuweza kupata faida kuanzia miaka 5 mpaka kumi inayofuata.
Kigezo hichi cha miaka ni ule uwezo wa kuwekeza bila kutoa, sasa kwa kijana ambaye tayari ana shughuli nyingine, ana miaka mingi ya kuendelea na kazi zake kabla hajaanza kutegemea uwekezaji wake. Lakini kwa mtu mzima, ambaye umri umekwenda, inabidi uwekezaji wake uanze kumzalishia mapema kwa kuwa muda wake wa kufanya kazi unaweza usiwe mrefu.
- Unaanza na kiasi gani katika kuwekeza.
Moja ya makosa ambayo watu wamekuwa wanafanya na kushindwa kuingia kwenye uwekezaji, ni kuona hawawezi kuanza kwa sababu kipato chao ni kidogo. Wengi wamekuwa wakifikiria uwekezaji ni mashamba na majengo, na hivyo kwa kiasi kidogo hawawezi kuanza.
Unapaswa kuanza uwekezaji hata kama una shilingi elfu moja ya kuwekeza. Na hapo unahitaji kuanza na uwekezaji ambao unaweza kuweka kiasi kidogo na kuendelea kukua zaidi kadiri muda unavyokwenda.
Kwa mfano kuwekeza kwenye hisa au vipande, unaweza kuanza na kiasi kidogo ambacho unaweza kumudu. Halafu unaweza kuweka mpango wa kununua vipande au hisa kadhaa kila mwezi. Kwa mpango huo, ukishafikisha kiasi kikubwa, unaweza kuuza na kuwekeza maeneo mengine yanayohitaji kiasi kikubwa kuwekeza.
- Uelewa wako kwenye eneo unalowekeza.
Moja ya vitu vinavyoshauriwa sana kwenye uwekezaji ni kuwekeza kwenye maeneo ambao unayajua vizuri, ambayo unaweza kuyafuatilia na kujua ni nini kinaendelea. Unahitaji kuwa na taarifa za kutosha kuhusu maeneo ambayo unawezekana ili uweze kufanya maamuzi sahihi kwenye uwekezaji huo.
Kabla hujafanya uwekezaji wowote, kwanza jifunze uwekezaji ule kwa karibu, ufuatilie na kujifunza. Na hata unapowekeza, endelea kufuatilia, jua ni wakati gani wa kuingia na wakati gani wa kutoka.
- Mgawanyo wako wa uwekezaji.
Wawekezaji wenye mafanikio makubwa hawashauri uwekezaji wako wote uwe kwenye eneo moja. Wanasema usiweke mayai yako yote kwenye kikapu kimoja, kikianguka utapoteza kila kitu. Hivyo pia kwenye uwekezaji, unahitaji kugawanya uwekezaji wako kwenye maeneo tofauti.
Wekeza kwenye maeneo tofauti tofauti, kwa kuwa kila eneo lina changamoto zake, ukipata hasara kwenye uwekezaji mmoja, uwekezaji mwingine utakuletea faida.
- Ni kiasi gani cha fedha upo tayari kupoteza.
Uwekezaji una hatari, na wakati mwingine hatari inavyokuwa kubwa, ndivyo pia faida inavyoweza kuwa kubwa. Kwa mfano, kampuni inaweza kuwa inaingiza hisa zake sokoni kwa mara ya kwanza, hapo huna uhakika wa hisa hizo zitakwendaje. Unaweza kununua na ukanufaika, au ukanunua na ukapoteza. Kitakachokuongoza kwenye wakati kama huu ni kujua kiasi gani upo tayari kupoteza. Yaani hapo unaweza kuwekeza fedha, lakini iwe ni fedha ambayo hata ukiipoteza haina athari kubwa moja kwa moja. Yaani siyo utoe fedha mahali ambapo tayari ilikuwa inazalisha na kwenda kuwekeza eneo ambalo huna uhakika nalo.
Hivyo ndivyo unavyoweza kufanya maamuzi yako ya uwekezaji na kujua uanzie wapi au uwekeze wapi kwa wakati gani.
Kama una swali au maoni kuhusu uwekezaji, hasa kwenye kuchagua uwekeze wapi, weka kwenye sehemu ya maoni hapo chini ili tuweze kujadiliana.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Ahsante kocha kwa somo pana la Uwekezaji kiukweli limenifungua sana.
Nimependa kuanza na Uwekezaji wa Hisa.
lakini sijajua ni kampuni gani naweza kuanzanayo uwekezaji wangu japo kwa kiwango kidogo cha fedha na kisha nianze kukua hatimae kufanya uwekezaji mwingine hasa unao hitaji kiwango kikubwa cha kianzio.
Naomba ushauri wako Kocha.
Ernest Lwilla
LikeLike
Habari Ernest,
Hongera kwa kupanga kuwekeza kwenye hisa.
Katika soko la hisa la dar es salaam, DSE, zipo hisa za makampuni takriban 21.
Kulingana na uwezo wako na malengo yako ya muda mrefu, hapo ndipo unaweza kuchagua ununue hisa zipi.
Unaweza kuanza na hiza zinazoingia sokoni kwa mara ya kwanza au kama hisa za vodacom zikishaandikishwa.
Pia unaweza kununua hisa za mabenki kama crdb.
Tembelea tovuti ya dse kujua bei za hisa na pia kupata mawakala wa kununua hisa.
Tovuti ya dse ni http://www.dse.co.tz
Kila la kheri.
LikeLike
Naomba kuuliza kamaDSE wako kati ya makampuni yanayotoa gawio.
LikeLike
Habari Mbise,
DSE wameanza kuuza hisa zai mwaka jana katikati, sijapata taarifa yao ya mwaka na kujua kama wanatoa gawio au la.
LikeLike
Nimekuwa napata taabu mara kwa mara ya tamaa ya kwenda kuchukua akiba nayoweka bank ninaona nikijipangia kiasi fulani kuanzia kuwekeza ktk hisa ile akiba yangu itafaa huku ninakwenda kufungua gereza langu la hisa kwa CRDB bank
LikeLike
Vizuri Hendry kwa maamuzi hayo,
Hatua hiyo itakujengea nidhamu kwenye kuweka akiba na pia itakuza uwekezaji wako.
Kila la kheri.
LikeLike
Ahsante kocha
LikeLike