Kuna watu wawili ambao wamesimama kati yako hapo ulipo wewe na pale ambapo unataka kufika, yaani mafanikio yako kimaisha. Hii ina maana kwamba, ukiweza kuwavuka watu hao wawili, hakuna cha kukuzuia wewe kufika pale unapotaka kufika.

IMG-20170217-WA0007

Lakini kama ilivyo, shida kubwa ya kutatua tatizo siyo tatizo lenyewe, bali kulijua tatizo. Wanasema kulijua tatizo ni nusu ya kulitatua. Hii ni kweli kwa sababu unakuta watu wanahangaika na kitu, unajiuliza kwa nini hawaoni njia rahisi ya kutatua, kumbe hawajui hata tatizo ni nini.

Sasa leo, mwanamafanikio mwenzangu, nakwenda kukukabidhi watu hawa wawili, ambao wewe mwenyewe utachagua kama uendelee kuwachekea na usifike unakotaka, au uwakomalie ili wakupishe ufike unakotaka kufika.

Nimekuambia ni watu wawili, lakini wa pili siyo mtu, ni kitu, au vitu, au watu. Hivyo kuna mtu mmoja, na upande wa pili kuna kitu, vitu au watu, ambao kwa minajili ya makala hii, tutaupa upande huo hadhi ya mtu.

Upo tayari kuuona ukweli na kupata uhuru wa kufikia mafanikio yako? Kama ndiyo basi karibu, lakini niahidi ya kwamba hutarudi nyuma. Maana nimekuwa najifunza sana kadiri ninavyowashauri na kuwakochi watu, wengi huwa wakishaujua ukweli wanarudi nyuma. Akishajua jukumu hasa lililopo mbele yake, atatafuta kila sababu ya kutolifanyia kazi kwa wakati huo. Sasa sipendi na wewe uwe kwenye kundi hili, nataka leo ujifunze kitu, na uweze kuchukua hatua.

SOMA; Zoezi La Kuitawala Fedha.

Mtu wa kuangusha; DUNIA.

Nimesema katika pande mbili tutakazokwenda kuangalia leo, upande mmoja tunaupa hadhi ya utu lakini kwa uhalisia siyo mtu. Upande huu ni dunia. Na kabla sijaenda mbali nikuambie tu, utakaposimama na kusema ninataka kufanya kitu hichi kikubwa ambacho hujawahi kufanya au wengi hawajawahi kufanya, dunia nzima itainuka na kukukatalia usipate kile unachotaka. Kama hujawahi kuona hilo jaribu tu sasa hivi, simama mbele ya marafiki zako, na waambie kwa sauti iliyonyooka, bila ya wasiwasi wowote ya kwamba miaka kumi ijayo utakuwa na utajiri wa dola bilioni 10. Watakuambia kila aina ya maneno, kila aina ya sababu kwa nini hilo haliwezekani, kama hawatakuchukulia umechanganyikiwa.

Sawa, tuachane na huo mfano na sasa turudi kwenye uhalisia, dunia itainua kila aina ya kizingiti kuhakikisha hupati unachotaka. Watu wataumwa, wewe mwenyewe utaumwa, utafungua biashara yako itakufa, utalima mvua hazitanyesha, utanyeshea, mbegu hazitakuwa nzuri au mavuno hayatakuwa mazuri, utapata mavuno mazuri na soko litakuwa limechafuka. Hivi unaona lakini namna ambavyo dunia haikunyimi wewe sababu?

Ndivyo dunia ilivyo, na hilo ndiyo inaloweza kufanya kwa usahihi mkubwa, kuhakikisha inaweza vizuizi ili usipate unachotaka. Hivi umewahi kujiuliza kwa nini madini yenye thamani ndiyo magumu zaidi kutafuta? Watu wataingia kwenye mashimo hatari sana ndipo waweze kuyapata madini. Ninachotaka rafiki ni uone namna gani dunia haitakupa kitu kirahisi.

Hivyo basi mtu au kitu cha kwanza kabisa kukiangusha, ni dunia. Hakikisha, hata dunia ikuletee kizingiti cha aina gani, haikupati. Yaani unahitaji kuwa mgumu mpaka dunia yenyewe ikuchoke, ikuone wewe umeshindikana, halafu ikuache ufanye yako.

Tukirudi kwenye ule mfano wa kuwaambia marafiki zako utafikisha dola bilioni 10, kila sababu watakayokupa kwamba huwezi wape jibu kwa nini unaweza, jaribu tu kuwapa jibu ambalo utalisimamia, hata kama huna uhakika nalo. Na baada ya muda au siku, watachoka kupingana na wewe, na watakuacha useme au ufanye yako. Nakuonesha ni namna gani dunia inachoka, kama wewe hutachoka haraka.

Hivi ndivyo unavyohitaji kwenda, umeumwa, imarisha afya yako na rudi kwenye mapambano. Umeanza biashara ikafa, simama na anza tena, ukiwa umejifunza zaidi, hata kama utaanza kwa kutembea nyumba kwa nyumba, anza, hakuna namna. Umefanya kilimo hujavuna vizuri, safi anza tena, na kila unachojifunza kiboreshe zaidi. Nakuhakikishia, dunia itasalimu amri, itakunyooshea mikono na kukuambia wewe nenda bwana, nimekushindwa.

Hapo tumeelewana rafiki? Utafanya hili? Tafadhali sana rafiki, fanya, fanya, fanya. Sijui hata nisisitizeje zaidi ya hapo. Lakini nakuomba, fanya, japo ni kwa mafanikio yako.

Mtu wa kutawala; WEWE MWENYEWE.

Ukishaiangusha dunia, unachohitaji sasa ni kujitawala wewe mwenyewe. Kwa sababu kama utaiangusha dunia, halafu ukashindwa kujitawala, utakuwa umewasha moto, halafu unajaribu kuuzima kwa mafuta ya taa. Kwa kifupi ni hatari. Utashindwa kuchukua hatua kabisa, au utachukua hatua ambazo zitakupoteza kabisa.

SOMA; Kama Unataka Kuitawala Siku Yako Ya Kesho Fanya Kitu Hiki Kimoja Kesho Asubuhi.

Kama yupo adui namba moja wa mafanikio yako, ambaye anakurudisha nyuma kwenye mambo mengi, basi ni wewe binafsi. Unataka kubisha hilo? jipe dakika chache na tafakari mipango yako yote mizuri ambayo umewahi kujiwekea kwenye maisha yako. Wala usiende mbali, anza tu na mipango ya mwaka huu, au ya mwaka jana. Ambayo ulipanga vizuri kabisa, lakini hukuifikia, kama utakuwa mwaminifu kwako, ni mingapi hata ulichukua hatua?

Mara ngapi umejiambia utawahi kuamka asubuhi ufanye kitu halafu hufanyi? Mara ngapi umejiambia utaanza biashara huanzi? Mara ngapi umesema kabisa utaacha tabia fulani ambayo inakuzuia kufanikiwa lakini huachani nayo? Unafikiri yupo anayekulazimisha au kukuzuia usichukue hatua? Sijui, angalia mwenyewe halafu uone majibu.

Ukweli ni kwamba, umekuwa unaruhusu mwili wako ukurudishe nyuma. Kama umewahi kuwa unataka kitu sana, lakini hupati msukumo wa kufanya, ni kwa sababu hujaweza kujitawala mwenyewe, hujaweza kuutawala mwili wako.

Nikupe mfano mwingine wa kufanya ili uone kweli nguvu uliyonayo kwenye kujitawala wewe mwenyewe, ambayo hujawahi hata kuitumia. Leo unapokwenda kulala, jiambie kabisa kwamba lazima uamke saa kumi kamili ya asubuhi. Jiambie ni muhimu sana kwako kuamka, na muda wote fikiria kuhusu kuamka saa kumi kamili ya asubuhi. Unapoingia kitandani fikiria tu kuhusu saa kumi asubuhi. Hakikisha mpaka unaingia usingizini, wazo pekee lililotawala akili yako ni kuamka saa kumi kamili ya asubuhi. Unapoenda kulala, usiweke hata alarm ya hiyo saa kumi asubuhi, wala simu isiwe karibu. Unapolala hata ukistuka kidogo, fikiria saa kumi kamili asubuhi. Endelea kulala, na muda ambao utastuka hasa, angalia saa, utakuta ni muda mfupi kabla ya saa kumi, au muda mfupi baada ya saa kumi. Fanya hivyo na nishirikishe imekuwaje kwenye maoni hapo chini.

Lengo la mfano huo hapo juu ni kutaka kukuonesha unahitaji nini ili uweze kujitawala wewe mwenyewe, uweze kuutawala mwili wako. Siyo kingine bali dhamira ya dhati, na kujikumbusha mara nyingi kipi ambacho unahitaji kufanya. Pale mwili unapokushawishi huwezi au hutaki, hapo ndipo unapoweka juhudi zaidi.

Bila kujitawala wewe mwenyewe, utakuwa unapelekwa na kila jambo kama bendera, mawazo yako hayatatulia mahali pamoja na hutaweza kukamilisha chochote.

Ukiweza kuiangusha dunia, kwa kupangua kila kikwazo inachokuletea, na ukiweza kujitawala wewe mwenyewe, kwa kuhakikisha mwili unafuata akili yako na siyo akili kufuata mwili, basi njia yako ya mafanikio ni nyeupe kabisa.

Uliniahidi utachukua hatua, wakati unaanza kusoma makala hii, naomba utimize ahadi yako. Na niambie chochote unachofikiri kwenye maoni hapo chini. Nimemaliza upande wangu, umebaki upande wako wa kutekeleza.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog