Kama unafanya biashara na hujawahi kuambiwa neno HAPANA, huenda kuna makosa unafanya kwenye biashara yako. Labda unaifanya kwa viwango vya chini sana, au huna mpango wa kuikuza. Lakini kwa kawaida, neno HAPANA utalisikia sana kwenye biashara, mno yaani. Na utalisikia kwa kila mtu, kuanzia wateja wako, wafanyabiashara wengine, washirika wako, watu wako wa karibu na hata kwenye taasisi unazohitaji huduma kutoka kwao.
Utaambiwa HAPANA kwenye mambo mengi ambayo utataka kufanya au kupata kwenye biashara. Na hapo ndipo inapoanzia tofauti ya wanaofanikiwa na wanaoshindwa kwenye biashara.
Neno HAPANA kwenye biashara, lina maana tofauti sana na tulivyozoea kwenye maisha ya kawaida. Kwenye maisha ya kawaida, mtu anapoambiwa HAPANA, huwa anatafsiri kwamba amekataliwa yeye na hafai kabisa. Hivyo wengi hukata tamaa na kuacha kabisa kile walichokuwa wanajaribu.
Lakini kwenye biashara, ukiwa mtu wa kuacha, au kukata tamaa mapema, utajaribu kila aina ya biashara, na hutaweza kupiga hatua. Kwa sababu kila biashara utakutana na HAPANA nyingi mno.
Kwenye biashara, neno HAPANA lina maana mbili;
Maana ya kwanza ni ‘hujanishawishi vya kutosha’. Mtu anakuambia hapana pale ambapo anakuwa hajakuelewa na hana muda wa kukazana kukuelewa. Hivyo neno rahisi kusema ni hapana ili msiendelee kupotezeana muda. Kwa maana hii, jukumu lako ni kuhakikisha wapi ambapo hujaeleweka, ili uweze kueleza vizuri, kwa njia ambayo utaeleweka. Kila unapoambiwa hapana, jiulize wapi ambapo hujaeleweka, au wapi ambapo hukuelewa vizuri mahitaji ya yule aliyekuambia hapana.
SOMA; Sababu Halisi Ya Watu Kukuambia HAPANA…
Maana ya pili ni ‘naogopa mabadiliko’. Watu hawapendi mabadiliko, wanayaogopa kweli, kwa sababu hawajui nini kinakuja, hivyo bora waendelee na kile walichozoea. Unapowaletea kitu ambacho kinawataka wabadilike, haraka sana watasema hapana, ili waendelee na kile walichozoea. Hivyo unaposikia neno hapana, jiulize watu wanahofia nini? Kipi ambacho unawataka wabadilike? Ukishakijua, wasaidie uhakika wa mambo kuwa mazuri baada ya mabadiliko hayo. Wape njia bora kwao kwenda na mabadiliko hayo bila ya kupoteza kile ambacho wanataka.
Elewa maana hii halisi ya neno HAPANA, ili unapoambiwa, usikate tamaa, bali ujipange zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog
