MAKIRITA AMANI:
Hongera rafiki yangu kwa siku hii nzuri sana ya leo.
Hii ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora.

Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tutaweza kwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu KAMWE USIJIWEKEE UKOMO…
Sisi ni utabiri unaoishi, maisha yetu yapo vile ambavyo tumekuwa tunayatabiri yawe.
Kila kinachotokea kwenye maisha yetu, tumekitengeneza kwa fikra ambazo zinatawala akili zetu.
Umewahi kujiambia ukila kitu fulani huwa unaumwa na tumbo? Nini kinatokea unapokula kitu kile? Hakika tumbo linakuuma. Mara nyingi tumbo linakuuma siyo kwa sababu ya kile ulichokula, bali kwa sababu akili yako inatengeneza kuumwa kwa tumbo, ili utabiri wako ukamilike.
Hivi ndivyo ilivyo kwenye kila jambo;
Kama umekuwa unajiambia watu wanakudharau, kila neno litakalotoka kwa yeyote ni la dharau.
Kama utajiambia wateja hawanunui kwako, kila anayekuja hatanunua kabisa.
Kama unajiambia kazi yako haina maana na hakuna wa kukujali, hicho ndiyo utaona kwenye kazi hiyo.
Kama unajiambia mwenza wako ni mkorofi au hajali, hicho ndiyo atakupa.
Na pale unapojiambia kwamba huwezi kitu fulani, kamwe hutakiweza, kwa sababu akili yako haitaki kukusaliti wewe.
Kwa mfano, umewahi kutumwa kitu labda mahali, wewe ukasema sioni kitu hicho, ukaambiwa kipo hapo, ukasema huoni, halafu mtu akaja na kukuonesha hichi hapa ni nini? Umekuwa huoni siyo kwa sababu hakipo, ila kwa sababu umeifunga akili yako isione.
Hivyo basi rafiki yangu, kamwe usijiwekee ukomo kwenye jambo lolote la maisha yako, kwa sababu ukomo huo utajidhihirisha kwenye maisha yako na kuwa kikwazo kikubwa cha maisha yako.
Weka akili yako wazi wakati wote, kuwa chanya wakati wote na kuwa tayari kuweka juhudi kubwa kila wakati. Utatengeneza utabiri mwingine ambao ni bora zaidi kwako.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.