Habari za leo rafiki yangu?

Karibu kwenye makala yetu ya leo ya ushauri wa changamoto mbalimbali ambazo zinatuzuia kuishi maisha ya mafanikio. Changamoto siyo kitu kigeni, kwani ni sehemu ya maisha. Lakini pia hakuna changamoto ambayo haina jawabu, hasa pale mtu anapojitoa kweli katika kuifanyia kazi.

Kwenye makala yetu ya leo ya ushauri, tunakwenda kuangalia jinsi ya kuondoka kwenye ulevi wa pombe na kuweza kuwa na maisha ya mafanikio. Kwa sababu ulevi wa pombe na vileo vya aina nyingine, ni adui mkubwa wa maisha ya mafanikio. Siyo kwenye fedha pekee, bali hata furaha na mahusiano bora. ukishakuwa mlevi huwezi kuwa na furaha, kwa sababu unakuwa umeweka hilo kwenye pombe. Pia mahusiano yako na wengine hayawezi kuwa mazuri. Hivyo ni muhimu kwa mtu yeyote ambaye anataka kuwa na maisha ya mafanikio, aepuke sana ulevi. Na kwa wale ambao wameshaingia kwenye ulevi basi waondoke mara moja.

Kwenye makala ya leo tunakwenda kuangalia jinsi ya kuondoka kwenye ulevi kwa wale ambao wameshakuwa walevi. Na kabla hatujaangalia namna ya kufanya hivyo, tupate maoni ya wasomaji wenzetu walioomba ushauri kwenye hili;

Za siku ndugu yangu mtafiti wa maswala ya mafanikio mimi nina tatizo la kunywa pombe kila nikipanga nifanye hivi zikipita siku chache nakuta tena nalewa mpaka mafanikio yangu nayaona magumu nifanye nini niweze kuacha pombe. Hussein G. H.

Tatizo ni pombe nashindwa nifanye nini. Abdallah M. N.

Kama tulivyoona hapo juu, wapo wenzetu ambao wanataka sana kuwa na maisha mazuri, ila wameshaingia kwenye kifungo cha ulevi.

Kwenye swala la ulevi, upo ushauri unaoweza kupata wa kisaikolojia, ushauri wa kitabibu na hata ushauri wa kiimani. Ushauri wa aina zote hizo ni muhimu sana. Lakini mimi sitagusia ushauri wa aina hizo, badala yake nakwenda moja kwa moja kwenye ushauri wa mafanikio. Ushauri wa mtu kufanya maamuzi muhimu ya maisha yake na kutokubali kurudi tena nyuma. Haya ni maamuzi muhimu na yenye nguvu kubwa. Nitakwenda kuwashirikisha hapa namna ya kuyafanya.
 
 

Ili kuweza kuondoka kwenye changamoto ya ulevi na kufikia mafanikio, nashauri kuzingatia mambo yafuatayo;

Moja; nini kinakusukuma kuingia kwenye ulevi?

Hakuna mtu ambaye analewa bila sababu. Kila mtu ana kitu ambacho kinamsukuma kwenda kwenye ulevi. Wapo ambao wanalewa kwa sababu wanaowazunguka nao wanalewa. Wapo ambao wanalewa kwa kuamini hilo ndiyo suluhisho la matatizo yao. Na wapo wanaolewa wakiamini ndiyo njia pekee ya kupata furaha ambayo wanayo.

Ni muhimu kujua wewe kipi kinakusukuma ulewe, kwani kwa kujua hili, utapata njia mbadala ya kupata unachopata kwenye ulevi.

Kama ulevi wako ni kwa sababu ya watu wanaokuzunguka, ukibadili wanaokuzunguka utaondokana na tamaa ya ulevi.

Kama ni sehemu ya kukimbia matatizo yako, ukiyakabili yale matatizo unayotaka kuyakimbia itakuwa bora zaidi kwako.

Kama ni sehemu ya furaha, ukijua maana halisi ya furaha, ambayo unaipata kwa kuishi vyema na wengine, utaweza kupata furaha kubwa bila hata ya kulewa.

Elewa kinachokusukuma, na angalia njia mbadala ya kukipata. Wapo wanaolewa kwa sifa, kwa sababu watu wanasema fulani anakunywa pombe kweli, sasa kama kinachokusukuma ni sifa, hamishia sifa hizo kwenye eneo jingine. Kwa mfano, fanya kazi yako kwa ubora sana, na watu wakusifie kwa kazi zako.
 

Mbili; ni kitu gani unataka kutoroka kwenye maisha yako.

Watu wengi sana ambao ni walevi, wamekuwa wakitumia ulevi kama njia ya kutoroka changamoto za maisha yao. Kuna kitu ambacho hawataki kukikabili na hivyo kuzubaisha akili zao kwa pombe ili wasikione kitu kile.

Ubaya wa hili ni kwamba, ulevi ukiisha kile unachokazana kukikwepa kinakuwa kipo pale pale. Hivyo njia pakee siyo kutumia ulevi, bali kutatua kile ambacho kipo mbele yako.

Wakati mwingine watu wamekata tamaa na kuona hakuna namna tena ya kufanya ili kuishi maisha waliyokuwa wanayataka. Ninachoweza kukuambia hapa ni kwamba, kama bado upo hai, hupaswi kukata tamaa hata kidogo. Unahitaji kuendelea kuweka juhudi na matokeo yanakuja.

Tatu; tafuta ulevi mpya.

Nilichojifunza ni kwamba, hakuna mtu anayeweza kuishi bila ulevi. Lakini upo ulevi mzuri na ulevi mbaya. Wengi wanakimbilia ulevi mbaya kwa sababu ni rahisi na hauhitaji changamoto kubwa. Lakini ulevi mzuri upo kwa kila mtu, ila ni mgumu na una changamoto nyingi.

Kwa mfano mimi ni mlevi wa kusoma na kuandika. Naweza kukaa chini siku nzima nikisoma vitabu, naweza kukaa chini na kaundika kurasa zaidi hata ya hamsini kwa siku. Na bado nikataka kuendelea kufanya tena na tena na tena. Lakini huu ni ulevi mzuri kwangu, kwa sababu una msaada kwangu na kwa wengine pia.

Hivyo kwa mtu yeyote ambaye ni mlevi, kaa chini na angalia kitu gani kinaweza kuchukua nafasi hiyo ya ulevi wa pombe kwa sasa. Angalia ni vitu gani unapenda kuvifanya hasa, na anza kuvifanya kwa wakati ule unaolewa. Ukiacha ulevi halafu muda huo ukabaki mtupu, utashawishika kurudi kwenye ulevi. Ila ukiacha ulevi na nafasi ile ukaipatia kitu kingine, utakuwa ‘bize’ na kitu kile na wala hutakumbuka tena pombe. Na ikiwa ni kitu unachopenda kufanya, utasahau kabisa kuhusu pombe.
 

Nne; epuka mazingira shawishi kwa ulevi.

Kama una marafiki ambao ni walevi, achana nao mara moja, bila ya kujali mmetoka wapi au mna mipango gani pamoja. Kama umeshakiri ulevi ni kikwazo kwako, na wanaokuzunguka ni walevi, waache tu kwa amani. La sivyo, utarudi kwenye ulevi, kwa sababu hakuna kitu chenye nguvu kama watu wa karibu kwako, hasa marafiki.

Mtu mmoja aliwahi kuniambia, lakini siwezi kuacha kwenda baa, kwa sababu baa ndipo kwenye ‘madili’ yote mazuri. Nikamwambia hilo linawezekana kwa sababu madili yake amezoea kuyapata baa, hivyo atakapobadilika, ataona njia nyingine za kupata madili nje ya baa.

Kuacha ulevi halafu ukaendelea kuwa maeneo ya baa, ni kujitengenezea majaribu na kujinyanyasa wewe mwenyewe. Chagua kuendelea na ulevi, au achana na ulevi na kaa mbali kabisa na baa na wale ambao ni walevi. Hakuna katikati.

Tano; tafuta watu wa kukufuatilia kwa karibu.

Mtangazie kile unayemfahamu na mnaheshimiana kwamba umeachana na ulevi kabisa. Wape na hatua za kuchukua iwapo watakukuta umerudi kwenye ulevi. Unaweza kutangaza hata kwenye mitandao ya kijamii. Na kuwapa watu hatua kazi za kukuchukulia iwapo watakukuta umerudi kwenye ulevi. Hili litakufanya ushinde ushawishi wa kurudi kwenye ulevi.

Ukiwa na uwezo, tafuta kocha wa kukuongoza kwenye hilo. Kocha atakusaidia pale unapokutana na changamoto kubwa kabisa na kukaribia kukata tamaa. Ukipata usimamizi wa karibu unaweza kuondokana na tabia yoyote usiyopenda na kujenga tabia mpya. Iwapo utanihitaji mimi kama kocha kwenye hilo, tuwasiliane kwa wasap 0717396253.
 

Fanyia kazi mambo hayo matano niliyokushirikisha hapa ili uweze kuondoka kwenye ulevi na kutengeneza maisha yako ya mafanikio. Usikubali kuendelea na tabia ambayo haina msaada kwako. Wala usikubali mtu akuambie kwamba ukishakuwa mlevi huwezi kuachana na ulevi. Wewe ndiye mwamuzi wa mwisho wa maisha yako, fanya maamuzi sahihi kwako.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,



TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog