Moja ya vitu unapaswa kuelewa kwenye maisha kwa ujumla ni kwamba kila mtu anapigana vita yake. Usione watu kwa nje wanacheka, ndani wana changamoto na matatizo ambayo wanakabiliana nayo.
Hivyo pia kwenye biashara, mteja anapokuja kwenye biashara yako, jua ana matatizo na changamoto zake nyingi tu na za kumtosha kabisa. Hajaja kwako kuongeza changamoto zaidi, kama vile alizonazo hazimtoshi.
Hivyo jitahidi kadiri ya uwezo wako, kuhakikisha humwongezei mteja wako matatizo na changamoto zaidi.
Hii inapaswa kuanzia kwenye bidhaa au huduma unayompatia, hakikisha maelezo ni sahihi na anaweza kupata kile ambacho anataka kupata. Kama ipo changamoto yoyote unayoona mteja anaweza kukutana nayo, basi msaidie kuitatua. Na pale mteja anapokutana na changamoto kwenye biashara yako, msaidie kuitatua mara moja.
Hii ni muhimu zaidi kwenye mawasiliano yako na mteja, jinsi unavyomkaribisha kwenye biashara yako, jinsi unavyomjibu maswali yake. Yote hayo yanaweza kumfanya mteja kujisikia vizuri au kuona anaongezewa changamoto.
Hii ni muhimu zaidi kwenye mambo madogo madogo kama chenchi, hivi mteja anapokuja kununua kwako, akakupa fedha na wewe ukamwambia huna chenchi, unakuwa unamaanisha nini? Kwamba mteja ni mjinga, au ni mzembe, kwa nini abebe fedha ambayo siyo ya chenchi? Huu ndiyo ujumbe unaoupeleka kwa mteja wako kila unapomwambia kwamba huna chenchi.
SOMA; BIASHARA LEO; Kabla Ya Mteja Kununua Unachouza, Anakununua Wewe Kwanza.
Vipo vitu vidogo vidogo unaweza kuwa unafanya kwenye biashara yako, bila hata ya kujua, lakini vikawa vinatengeneza changamoto kwa wateja wako, kiasi cha kuamua kutokuja tena kwenye biashara yako.
Tafakari kila unachofanya kwenye biashara yako, kila unachosema na kila unavyomjibu mteja wako, na ona ni kwa namna gani kinamsaidia au kumwaza mteja.
Wateja tayari wana changamoto za kuwatosha, usiwaongezee nyingine.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Asante kaka.🙆🙆
LikeLike
Karibu sana.
LikeLike