Zipo aina mbili za uchumi wa biashara, aina moja ni rahisi kufanya lakini matokeo yake siyo mazuri. Aina nyingine ni ngumu kufanya lakini matokeo yake ni mazuri, hasa ukiweza vizuri.

Aina ya kwanza ni kuwafikia wateja wengi uwezavyo, kukazana kila mtu awe mteja wako. Hapa inakubidi uwe na kitu ambacho kitamfaa kila mtu, na hivyo kitakuwa kitu cha bei rahisi na ambacho ubora wake siyo mzuri.
Kwa aina hii ya uchumi, huhitaji kujitofautisha sana, wala kufikiri kwa kina na kuwa na ubunifu. Unaangalia tu namna gani utawafikia wengi, na mara nyingi unaanzia kwenye bei, ambayo ni kuwa rahisi kuliko wengine wote.
Sasa unapokuwa na bei rahisi, maana yake kiasi cha faida ni kidogo, huduma utakazotoa ni mbovu na ubora wa bidhaa au huduma unayotoa utakuwa hafifu.
Lengo lako lakuwafikia wengi linaweza kutimia, lakini hiyo itakuchosha na ni mbio za kuua biashara.
Aina ya pili ya uchumi ni kuwalenga wachache ambao wana sifa za kuwa wateja wa biashara yako. Hapa unawaangalia wale hasa ambao wana uhitaji wa kile unachotoa, ambao wapo tayari kukipata kwa sababu wana matatizo au changamoto ambazo unaweza kuzitatua.
Kwa njia hii, unawavutia watu ambao wanauhitaji wa kweli, ambao kama wanapata kile wanachotaka hasa, bei kwao siyo tatizo kubwa sana.
Hawa huwa ni wachache, lakini pia unaweza kutengeneza faidia nzuri, huku ukiwapa huduma bora sana. hili linakuhitaji uwe na ubunifu mkubwa, uweze kujitofautisha kabisa na wengine.
Huduma zako pia zinapaswa kuwa bora sana, hata kama unachouza kinauzwa na kila mtu, huduma unayompa mteja, iwe kubwa na nzuri sana. Mshangaze mteja kiasi kwamba atashindwa kunyamaza na muda wote atataka kuwasimulia wengine namna ulivyomhudumia vizuri.
Biashara yoyote unayofanya, kazana kutumia uchumi wa pili, wa kuwafikia wale hasa wenye uhitaji, kuwasaidia na wao kuwa wateja wazuri na waaminifu kwenye biashara yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog