Hongera rafiki yangu kwa siku hii nzuri na ya kipekee sana ya leo.
Ni nafasi nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa, ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu NJIA YA UHAKIKA YA UMASIKINI….
Yapo mambo mengi ambayo watu wamekuwa wanayafanya na yanawaingiza au kuwahakikishia kubaki kwenye umasikini.
Lakini kati ya hayo mengi, jambo moja lina nguvu kubwa ya kumfanya mtu aendelee kuwa masikini maisha yake yote.
Jambo hilo ni kuwa na matumizi yanayozidi kipato.
Haijalishi kipato ni kikubwa kiasi gani, kama matumizi yanazidi kipato ambacho mtu anacho, basi ana uhakika wa kuwa masikini.
Kwa sababu ni hali hiyo ambayo hupelekea watu kukopa, na unapokopa unalipa fedha zaidi ya ulizopokea.
Pia kwa matumizi kuwa makubwa kuliko mapato, kunamnyima mtu fursa ya kuwa na akiba na hata kuwekeza.
Hivyo anajikuta maisha yake yote anakazana kutafuta fedha lakini hakuna hatua kubwa ambayo anakuwa amepiga.
Matumizi ni eneo nyeti sana katika mipango yako ya kifedha, usipoliangalia vizuri, litakuwa mzigo mkubwa kwako na tiketi ya kubaki kwenye umasikini daima.
Katika kuweka sawa mambo yako ya kifedha, kwanza anza na kuangalia matumizi na kuweza kuyadhibiti vizuri, kisha nenda kwenye mapato na kuyaongeza.
Ukikimbilia kuongeza kipato wakati bado hujadhibiti matumizi, utaishia kupoteza fedha zaidi. Kama wafanyakazi wengi ambao hata mshahara unapoongezeka, maisha bado yanazidi kuwa magumu kwa sababu kile kilichoongezeka kinaliwa na matumizi yanayoongezeka pia.
Na sheria ya fedha ni kwamba kama kila kitu kitaachwa kama kilivyo, yaani hakuna jitihada za dhati zinazowekwa, mapato yanapoongezeka na matumizi pia yanaongezeka.
Ni wajibu wako kuhakikisha matumizi yako yanakuwa madogo kuliko mapato yako.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.