Kwenye kitabu cha The Lean Startup, mwandishi Erick Ries anatushirikisha dhana ya MVP ambayo kirefu chake ni Minimum Viable Product. Dhana hii inaeleza kwamba unapoanza biashara, anza na bidhaa ambayo haujakamilika, lakini iwe na sifa ambazo inaweza kumsaidia mtu. Badala ya kutumia nguvu nyingi kuja na bidhaa au huduma kamili, unaanza na kitu ambacho hakijakamilika lakini kinaweza kumsaidia mtu mwenye uhitaji au changamoto. Hapo sasa mteja akitumia anakupa maoni na unaboresha zaidi.

Dhana hii ina mambo mawili;
Moja kuanza kidogo, kutokusubiri mpaka ujione upo kamili, kwa sababu wengi wamekuwa wakisubiri wawe kamili na hilo kuwachelewesha kuchukua hatua.
Mbili ni kuanza na kitu ambacho watu tayari wanakihitaji. Hapa unaanza na kitu ambacho watu wanahitaji kweli, lakini huwezi kujua kwa hakika wanataka nini, na hivyo unaanza na bidhaa ambayo haijakamilika, kadiri wanavyotumia, wanakupa maoni na wewe unayafanyia kazi ili kuboresha zaidi. Mwishowe unakuwa na bidhaa ambayo watu wanaihitaji kweli.
SOMA; BIASHARA LEO; Biashara Yako Inavyozidi Kukua, Unahitaji Kubadili Mikakati…
Leo hapa tutajadili jambo hilo la pili, hasa kwa wale wanaoanza bishara. Hii ni kwa sababu wengi huanza na kile ambacho wanataka kuanza nacho wao. Wanauza kile ambacho wao wanaweza au wanapenda, na wanasahau kwamba hawajiuzii wao wenyewe.
Unapoanza biashara, anza na kitu ambacho tayari watu wanakihitaji kweli. Anza na shida au tatizo ambalo watu wanalo na wapo tayari kulitatua, na liwe na kipaumbele kwao.
Lakini changamoto ni kwamba huwezi kujua kwa hakika watu wanataka nini. Kwa sababu hata ukifanya utafiti, wanachokujibu watu siyo wanachotaka kweli. Hivyo unahitaji kuanza kwa kujaribu, unaanza kwa kile kidogo ambacho kinamwezesha mtu kutatua changamoto yake, kisha angalia wanakipokeaje. Angalia wanatumiaje, angalia wanatoa maoni gani. Hapo sasa unaweza kuboresha zaidi ili kuweza kuwapa watu kile wanachohitaji kweli.
Hata kama biashara unayofanya ni ya kununua jumla na kuuza rejareja, unapoanza huna uhakika watu wanataka nini hasa. Hivyo usitumie mtaji wako wote kununua mali nyingi. Badala yake acha sehemu ya mtaji ujifunze kwanza watu wanahitaji nini zaidi. Ukishajua basi tumia sehemu hiyo ya mtaji kununua kile wanahitaji zaidi.
Ukitumia mtaji wote kununua vile vitu unavyofikiri watu wanataka, utajikuta una bidhaa nyingi ambazo watu hawazihitaji sana, na zile wanazohitaji zimeisha huku huwezi kununua nyingine.
Anza na kile ambacho watu tayari wanahitaji, anza kwa kujaribu kisha boresha zaidi kadiri unavyokwenda.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog