Habari ya leo mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa hujambo na unaendelea vizuri. Hongera sana rafiki kwa zawadi ya siku hii ya leo kwani kuamka salama ni ushindi mkubwa katika maisha yako hivyo tumia ushindi huo wa uhai kuacha alama siku hii ya leo kumbuka kuwa maisha ni muda. Kumbuka kuiendea siku hii ya leo kwa misingi yetu ya Amka Mtanzania ya nidhamu, uadilifu na kujituma.

Rafiki, napenda kutumia nafasi hii kukualika tena siku hii ya leo katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja yale mazuri niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo. Kwa namna ya pekee rafiki yangu, nakusihi sana tusafiri pamoja hadi mwisho wa somo letu la leo ambapo leo tutakwenda kujifunza mtu asiyeishiwa sababu katika maisha yake hivyo basi, karibu tujifunze.

Kitu chochote ambacho ni muhimu kwako lazima utapata muda wa kukifanya. Na kitu chochote ambacho siyo muhimu kwako lazima utakosa muda wa kukifanya. Kila binadamu ana masaa ishirini na nne kwa siku na utofauti wetu uko katika matumizi ya masaa haya ishirini na nne.

lazy-homer2

Rafiki, siku zote mtu mvivu huwa haishiwi sababu na mtu aliyechoka huwa haishiwi sababu za kutaka kupumzika. Hivyo basi, na mtafuta sababu huwa haishiwi sababu katika maisha yake hata siku moja. Kuna watu huwa hawaishiwi sababu hata siku moja katika maisha yao. Asili ni asili lakini tabia yeyote yakimazoea unaweza kuibadilisha kwa sababu hujafunga nayo ndoa na useme ushindwe kuiacha.

Katika maisha yetu ya kila siku huenda tumekuwa ni watu wa kufauta sababu kuliko matokeo. Tumekuwa ni watu wa kulalamika na kutafuta sababu na siyo kutafuta matokeo, jamii imeathirika katika kutafuta sababu na mtu anayetafuta sababu katika jamii anaonekana kawaida kwa sababu ndiyo asili ya watu wengi.

SOMA; Sumu Kali Inayoua Mahusiano Ya Ndoa Na Uchumba.

Tumekuwa ni watu kusingizia sina muda wa kufanya, niko bize , nitafanya baadaye na mengine mengi kumbe hizi zote ni njia za kujiridhisha tu sisi wenyewe kwa kujitafutia sababu nzuri kwa sababu mtafuta sababu siku zote huwa haishiwi sababu. Mambo mengine rafiki huwa yanastaajibisha sana kwa mfano, unaweza kuwekeana mpango na mtu wa kutaka kuanza kubadilika kutoka katika tabia za kimazoea lakini bado mtu huyo huyo anayetaka kubadilika huwa haishiwi sababu kwanini asibadilike na abaki palepale alipo.

Tunapenda mabadiliko katika maisha yetu huku tukitaka kubaki kama vile tulivyokuwa awali. Mabadiliko yoyote katika maisha hayajawahi kumuacha mtu salama kama vile alivyo lazima mabadiliko yoyote yatakuathiri kwa namna moja au nyingine. Huwezi kusema nataka kuanza kusoma kitabu lakini nakosa muda wa kusoma kitabu wakati huo huo unapata muda wa kucheza bao na kupiga stori. Unaweza ukajiuliza swali dogo kwanini wewe unashindwa na wenzako wanaweza? Na hizo sababu unazojiba tokea uanze kujiba sababu zimekunufaisha na nini?

Mpendwa msomaji, tunaalikwa tuyatafute mafanikio kule yaliko na siyo mafanikio yatufuate sisi. Tabibu hata siku moja hawezi kupita nyumba hadi nyumba kutafuta wagonjwa ila mwenye shida siku zote ndiye anamtafuta mganga kule aliko. Usisubiri kupata mabadiliko unayoyataka kwa kuendelea kubaki kama ulivyo bila kuchukua hatua yeyote.

Hatua ya kuchukua leo, kama wewe ni mtu wa sababu ni vema ukaacha sababu kwani sababu haziwezi kukutoa hapo ulipo sasa. Na siku zote tambua kuwa mtafuta sababu huwa haishiwi sababu ni sawa na mvivu huwa haishiwi sababu za kutaka kubaki katika uvivu wake. Yafuate mafanikio na usisubiri yakufuate wewe.

Kwahiyo, somo letu la leo limetualika sisi sote tuweze kuacha sababu na tutafute matokeo. Kama tukiendelea kutafuta sababu kamwe hatuwezi kukosa sababu kwa sababu mtafuta sababu huwa haishiwi sababu hata siku moja.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net  au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com kwa kujifunza zaidi kila siku. Asante sana.