Habari za asubuhi ya leo rafiki yangu?

Ni siku nyingine mpya, ambapo tumepata nafasi ya kipekee ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora.

Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu CHAKO NI UNACHOKIELEWA…

Watu wengi wamekuwa wakijidanganya kwamba wana vitu, lakini siyo vyao, kwa sababu hawavielewi vizuri.

Kama kitu hukielewi vizuri, bila ya shaka yoyote, basi hicho siyo chako, huwezi kusema unakimiliki.

Unachomiliki kweli ndiyo unaweza kusema ni chako, kwa sababu unakielewa vizuri.

Hata wewe mwenyewe, kama bado hujajijua na kujielewa vizuri, utatumiwa na wengine ambao wanajijua na kujielewa vizuri. Maisha yako, akili yako, nguvu zako na hata ujuzi wako vitakuwa mali ya wengine, wale ambao wameshajijua vizuri.

Ndiyo maana ni muhimu sana kukijua kwa kina kitu chochote unachojihusisha nacho, kijue nje ndani.

Anza na wewe mwenyewe, kisha kwenye kazi, biashara na kingine chochote unachofanya.

Jambo lolote unalojihusisha nalo, chukua muda kulijua kwa kina, ili uweze kulifanyia kazi vizuri.

Usiishie tu kufanya kwa sababu wengine wanafanya, au kufanya kwa sababu umezoea kufanya. Fanya kwa kujua kwa nini unafanya, na fanya ukiwa bora zaidi.

Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.

Rafiki yako,

Kocha Makirita Amani,

MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.

www.kisimachamaarifa.co.tz