Tunaposikia neno mafanikio, watu wengi hufikiri vitu vya nje na vinavyoonekana, hivyo wengi hukazana kutafuta vitu hivyo vya nje, lakini wanapovipata wanaona bado kuna utupu ndani yao.

Stephen Covey kupitia kitabu chake cha Primary Greatness aliandika kwamba, zipo aina kuu mbili za mafanikio au ukuu. Aina ya kwanza ni yale mafanikio yanayoanzia ndani ya mtu mwenyewe, haya yanatokana na mtu kuijua misingi ya sheria za asili na kuiishi. Aina ya pili ni yale mafanikio ya nje, ambayo yanatokana na wadhifa, umaarufu na vitu vinavyoonekana.

Watu wengi wamekuwa wakikazana kutafuta mafanikio ya nje, na hawayapati au wakiyapata hayadumu muda mrefu. Lakini Covey anatuambia kupitia kitabu hichi kwamba, mtu akikazana kutafuta mafanikio ya ndani, ambayo yanatokana na tabia za ndani na kuishi misingi ya sheria za asili, mafanikio ya nje yanakuja yenyewe, bila ya kutumia nguvu kubwa.

Kupitia kitabu hichi cha Primary Greatness, tunakwenda kujifunza nyenzo 12 za kutuwezesha kutengeneza mafanikio ya ndani, ambayo yatadumu miaka yetu yote na kutuwezesha kuwa na mafanikio ya nje pia.

Mimi binafsi napenda sana misingi, hasa ile misingi ya sheria za asili. Misingi hii huwa ipo sahihi wakati wote, na ukiivunja huwezi kubaki salama. Misingi inafanya kazi iwe mtu anajua au hajui, na hivyo ni muhimu sana tuijue misingi ili tuweze kufanikiwa.

primary greatness

Karibu kwenye uchambuzi huu wa kitabu tujifunze misingi 12 ya maisha ya mafanikio.

 1. Msingi wa mafanikio ni kuiishi misingi.

Huwezi kufanikiwa kama huijui misingi na kuifuata. Kila kitu hapa duniani kinaendeshwa na misingi ya sheria za asili, kuna kupanda na kuvuna, kuna kutoa na kupata. Usipoijua misingi hii na kuiishi, huwezi kufanikiwa. Misingi hii haiwezi kuvunjwa bila ya madhara.

Watu wengi wamekuwa wakijaribu kutumia njia za mkato kufanikiwa, wamekuwa wanaumia kuliko mafanikio wanayopata.

 1. Misingi ya sheria za asili ipo nje ya uwezo wetu.

Jambo moja tunalopaswa kujua na kukubali kuhusu misingi ya sheria za asili ni kwamba, ipo nje ya uwezo wetu. Hakuna mtu yeyote, hata awe mjanja kiasi gani, hata awe na nguvu kiasi gani, anayeweza kuivunja au kubadili misingi hii.

Misingi hii inafanya kazi yenyewe, haijalishi watu wapo au hawapo. Hivyo ni muhimu kuijua misingi na kuiishi ili kunufaika, badala ya kuipuuza na kuumia.

 1. Tuna maisha ya aina tatu.

Maisha ya nje, haya ni yale yanayoonekana na kila mtu, kwenye maisha yetu ya kawaida, kazi au biashara.

Maisha ya familia, haya ni yale maisha tunayoishi na kuonekana na familia zetu.

Maisha binafsi, haya ni yale maisha tunayoishi sisi kama sisi, haya ni maisha ya siri, yale mambo ambayo tunafanya kama tuna uhakika hakuna anayetuona.

Ili kujua kusudi kubwa la maisha yako, unapaswa kuyatembelea na kuyajua maisha yako ya sirini.

Na ili kuwa na mafanikio, kile unachoishi kwenye maisha yako binafsi, kiwe ni ambacho upo tayari kuishi kwenye amisha ya nje. Usiwe na maisha ya aina mbili, nje unaonekana hivi lakini ndani upo tofauti, hapo huwezi kufanikiwa.

 1. Tabia ni muhimu kuliko kitu kingine chochote.

Ukiangalia kwa kina tofauti ya wanaofanikiwa na wanaoshindwa, hutaona elimu, vipaji, fedha na hata uwezo vikileta tofauti. Bali tofauti kubwa inatokana na tabia.

Ukiangalia wale wanaofanikiwa wanakuwa na tabia za tofauti kabisa na wale wanaoshindwa. Tabia ina nguvu sana kwenye matokeo ya maisha yetu.

Makampuni makuba yameanza kuelewa hili na sasa kigezo kikubwa cha kuajiri siyo elimu wala uwezo, bali tabia. Kwa sababu tabia ina mchango mkubwa sana wa mafanikio ya mtu.

 1. Vitu viwili vinavyojenga maisha ya wema.

Moja; unyenyekevu, huu ndiyo unaotuwezesha kuielewa misingi na kuwa tayari kuiishi.

Ujasiri; huu ndiyo unatuwezesha kuchukua hatua, kusimamia misingi sahihi na kufikia mafanikio makubwa.

SOMA; ONGEA NA COACH; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuishinda Hofu Ya Kushindwa Na Kuweza Kufanikiwa.

 1. Vunja utumwa wa mwili na hisia.

Watu wengi wamekuwa watumwa wa miili yao na hisia zao kiasi kwamba hawawezi kuiishi misingi ya sheria za asili. Watu hawa wanakuwa wameshauzoesha mwili kupata kile unachotaka, na kupata zaidi ya unavyostahili kupata. Kwa mfano kula kupita kiasi, kutumia ulevi, kutofanya mazoezi.

Ili mtu kuweza kutoka kwenye hali hizi, lazima kwanza avunje utumwa ambao amejijengea kwenye mwili na hisia. Unahitaji kujijenga kiroho ili kuweza kuwa na nia ya dhati ya kuvunja utumwa huo.

Bila kuvunja utumwa, huwezi kabisa kupiga hatua.

 1. Zawadi nne ambazo binadamu tunazo.

Sisi binadamu tupo tofauti kabisa na viumbe wengine hai kwa sababu tuna zawadi hizi nne;

Moja; kujitambua, ambapo tunajua sisi ni nani na tupo hapa duniani kufanya nini.

Mbili; uwezo wa kufikiri, hatufanyi tu kwa sababu kila mtu anafanya, bali tunaweza kufikiri na kufanya.

Tatu; utashi huru, tunaweza kuamua kufanya au kutokufanya jambo.

Nne; ubunifu, tuna uwezo wa kutengeneza kitu kipya, ambacho hakijawahi kuwepo kabisa, kwa kuanzia na fikra zetu.

Wapo watu wengi ambao hawatumii kabisa zawadi hizi nne, na hivyo kupita hapa duniani na kuondoka bila ya kufanya lolote kubwa. Kazana kutumia zawadi hizo na utaweza kufanikiwa.

 1. Uadilifu usiotiliwa shaka ndiyo msingi mkuu.

Katika misingi yote tunayokwenda kujifunza kwenye kitabu hichi, upo msingi mmoja mkuu ambao ni uadilifu, tena uadilifu usiovunjika wala kutiliwa shaka.

Watu wengi wamekuwa wana maisha ya aina mbalimbali. Wakiwa mbele ya jamii wanaishi kwa taswira fulani wanayotaka waonekane, wakiwa na familia wana taswira nyingine na wakiwa faraghani wana taswira nyingine.

Maisha ya aina hiyo hayajawahi kumpa mtu mafanikio yanayodumu. Wapo wanaofanikiwa kudanganya kwa muda, lakini mwisho kila kitu huwa wazi.

Hivyo kama unataka mafanikio ya kweli, mafanikio yadumuyo, hakikisha unakuwa na uadilifu usiotiliwa shaka.

Zifuatazo ni nyenzo kumi na mbili za mafanikio ya ndani na yadumuyo;

 1. Nyenzo ya kwanza; UADILIFU.

Kama tulivyoona, msingi mkuu wa maisha ya mafanikio ni uadilifu, usiovunjika wala usiotiliwa shaka.

Maisha yako ya ndani lazima yaendane na maisha yako ya nje.

Vitu viwili vitakavyokusaidia kujenga uadilifu ni unyenyekevu na ujasiri.

Kuwa wewe, usitake kuwashawishi watu kwa vitu vya nje, bali washawishi kwa vitu vya ndani.

 1. Nyenzo ya pili; MCHANGO.

Huwezi kufanikiwa kama unategemea dunia na kila mtu vikupe kila unachotaka na wewe usitoe chochote. Lazima uwe na mchango mkubwa kwa wengine na kwa dunia kwa ujumla ndiyo uweze kufanikiwa.

Hivyo kila wakati jiulize ni mchango gani unatoa kwa wengine? Unataka fedha sawa, lakini je unawapa wengine nini mpaka wakupe fedha. Ukifikiria hivi kamwe hutatafuta njia za mkato, ambazo hazifanyi kazi.

 1. Nyenzo ya tatu; KIPAUMBELE.

Una mambo mengi unayotaka kufanya kuliko muda ulionao wa kuyafanya. Kitu pekee kitakachokuwezesha kufanya yale muhimu ni kuwa na kipaumbele kwenye maisha yako.

Kipaumbele ni pale unapojua mambo yapi ni muhimu zaidi kwako na kuyafanya hayo, huku yale ambayo siyo muhimu zaidi ukaachana nayo, au ukatafuta wengine wakayafanya.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Born To Win (Umezaliwa Kushinda, Ijue Siri Yako Ya Mafanikio)

 1. Nyenzo ya nne; KUJITOA.

Huwezi kupata kile unachotaka, kwa namna unavyokitaka, kwa wakati unaotaka. Kuna wakati utahitaji kupoteza kitu fulani ili kupata kile unachotaka.

Lazima uwe tayari kujitoa kwa ajili ya wengine, wakati mwingine ukose au kupoteza vitu kwa ajili ya wengine. Unahitaji kuona umuhimu wa wengine na kujitoa kwa ajili yao, ndiyo uweze kufanikiwa.

 1. Nyenzo ya tano; KUHUDUMU.

Yapo mambo madogo madogo sana ambayo ukiyafanya, unaongeza thamani kwa wengine na wao wanakuwa tayari kukupa wewe kile unachotaka. Kwenye kila unachofanya kwenye maisha yako, hakikisha unatoa huduma bora kabisa kwa wengine. Weka utu kwenye kila unachofanya, mfanye mtu kujisikia vizuri, kujisikia ni mtu muhimu. Na kila anayeguswa na huduma yako, atakuwa tayari kufanya zaidi kwa ajili yako.

 1. Nyenzo ya sita; MAJUKUMU.

Mambo yanapokuwa yanaenda vizuri, kila mtu anaweza kufanya na kusema yeye ndiyo amesababisha mambo yaende vizuri. Ni pale mambo yanapokwenda vibaya ndipo utaona kila mtu anakataa kuhusika.

Ili ufanikiwe lazima uwe tayari kukubali jukumu lako kwenye kila hali. Pale ambapo mambo hayaendi vizuri ukubali kwamba umechangia hali hiyo na uwe tayari kuchukua hatua.

 1. Nyenzo ya saba; UAMINIFU KWA WENGINE.

Waheshimu na kuwaamini wengine, hata kama hawapo pale ulipo. Usimseme mtu vibaya ambaye hayupo, usishiriki maongezi ya kuwateta watu ambao hawapo. Na wakati wowote unapokutana na hali ya mtu kusemwa vibaya, mtetee kama ni mtu unayemfahamu na unajua mazuri yake.

Tabia ya kuwasema watu vibaya huwa ina madhara makubwa kwa sababu chochote kibaya unachomsema mtu, hata kama ni kwa siri, kuna wakati kitamfikia, na hilo litaharibu mahusiano.

 1. Nyenzo ya nane; USAWA.

Wafanyie wengine kile ambacho unapenda wakufanyie wewe, kwa sababu kile unachowafanyia wengine, kwa hakika hicho ndiyo watakufanyia na wewe pia. Au kama siyo wao watakufanyia, basi wengine watakufanyia wewe.

Dunia inalipa kila tendo unalofanya, hivyo fanya yale ambayo unataka dunia ikulipe. Na usifanye kwa sababu unataka dunia ikulipe, bali fanya kwa sababu ni kitu sahihi kufanya.

SOMA; Mambo Muhimu Ya Kujifunza Kuhusu Nidhamu Binafsi Na Mafanikio.

 1. Nyenzo ya tisa; UTOFUTI.

Tunapenda sana kufanya vitu sawa, kuzungukwa na watu wanaokubaliana na sisi na wanaofanya kile tunachotaka bila ya kupinga au kuhoji. Lakini mafanikio hayajawahi kutengenezwa na watu wanaofikiria kitu kimoja.

Mafanikio makubwa yanatengenezwa na watu wanaotofautiana, kimawazo na kimtazamo. Utofauti wao ndiyo unatengeneza kitu kizuri kinachogusa maeneo yote. Usitake kuzungukwa na watu ambao wanakubaliana kila kitu na wewe, na ambao mnafanana kwa kila kitu. Unahitaji watu tofauti, watakaoleta ujuzi tofauti na watakaokufanya ufikiri kwa kina kwenye maamuzi unayofanya.

 1. Nyenzo ya kumi; KUJIFUNZA.

Kama hujifunzi kila siku, huna nafasi ya kutengeneza mafanikio makubwa kwenye maisha yako. Tunaishi kwenye zama ambazo mabadiliko yanatokea kwa kazi sana. chochote tunachojua leo, miaka mitatu ijayo kitakuwa hakina maana tena.

Jifunze sana kuhusiana na kazi yako, biashara na mafanikio kwa ujumla. Usiseme unajua kila kitu, kila wakati lipo jambo la kujifunza.

 1. Nyenzo ya kumi na moja; KUJIHUISHA.

Huwezi kufanikiwa kama utapuuza maeneo muhimu ya maisha yako kama afya, akili, imani, mahusiano na hisia. Haya ni maeneo muhimu sana ambayo unahitaji kuyafanyia kazi kila siku ili kukua na kuwa bora zaidi.

Unahitaji kupata muda wa kupumzika, kutafakari, kusali, kutahajudi na kujifunza zaidi ili kuwa vizuri kwenye kila eneo la maisha yako. Usiwe mtu wa kazi tu muda wote, utauchakaza mwili kama utapuuza hayo maeneo mengine.

 1. Nyenzo ya kumi na mbili; KUFUNDISHA.

Njia bora kabisa ya kujifunza na kuelewa kitu chochote, ni kufundisha. Chochote unachojifunza, chochote unachotaka kuwa bora kwenye maisha yako, tafuta watu na wafundishe. Hili litakuwezesha kuelewa na kuishi kile unachojifunza.

 1. Neno la mwisho; PATA HEKIMA.

Stephen Covey alimaliza kitabu hichi kwa kutuasa tupate hekima. Kwa sababu tunaishi kwenye ulimwengu ambao taarifa tunazopata ni nyingi mno. Lakini taarifa hizi hazitakuwa na maana kwetu, kama hatutaweza kuzielewa na kuzitengeneza kwa njia nzuri ambayo tunaweza kuiishi kwa misingi ya sheria za asili.

Hekima ni pale taarifa na maarifa unayopata, unaweza kuyatumia kwenye maisha yako kwa kuzingatia misingi ya sheria za asili. Hivyo tukiweza kuishi nyenzo hizi 12 kwenye maisha yetu, utakuwa na maisha yenye mafanikio makubwa na tutakuwa na hekima pia.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kusoma kitabu kimoja kila mwezi tembelea www.amkamtazania.com/kurasa

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

www.kisimachamaarifa.co.tz