Tabia mbili kuu tulizonazo ambazo zinatuzuia kabisa kufanikiwa ni uvivu na kupenda kuwafurahisha wengine.

Hatupendi kufanya vitu ambavyo ni vigumu, vitu ambavyo vinatupa changamoto na kutusukuma zaidi, vitu ambavyo tunaweza kushindwa. Lakini vitu hivyo ndiyo muhimu kwa mafanikio yetu, vitu hivyo ndiyo vyenye maana kubwa kwetu na ndiyo vyenye mchango kwa wengine.

Lakini pia tunapenda kuwafurahisha wengine, tunapenda kukubalika na kila mtu, kila mtu atusifie kwa kile tunachofanya. Akitokea hata mmoja akatupinga au kutukatisha tamaa tunachukia, hatupendi na tunakazana kubadilika ili tuwafurahishe.

gold coins

Hayo mawili ni kikwazo kikubwa sana kwa mafanikio kwenye maisha yetu.

Mafanikio yanaendana na kukereka, yaani kama huwezi kuvumilia kujikera wewe mwenyewe, na kama huna uthubutu wa kuwakera wengine, unaweza kusahau kuhusu mafanikio.

Lazima ujikere wewe mwenyewe, ujilazimishe kufanya vitu ambavyo wewe mwenyewe hupendi kufanya, ujisukume zaidi ya unavyotaka kujisukuma. Hili ndiyo linakuwezesha wewe kupata kile ambacho wengine wanakosa.

Pia chagua kuwakera baadhi ya watu katika safari yako ya mafanikio. Jua kabisa wapo watu ambao hawataendana na kile unachofanya, hawatakifurahia na hawataweza kukivumilia. Hawa ni watu ambao lazima ukubaliane nao kwa namna walivyo, kisha wewe ukaendelea na mambo yako, usiwape nafasi ya kukuzuia wewe kufanikiwa.

SOMA; UKURASA WA 956; Usijioneshe, Bali Onekana…

Kero unayoikubali, ambayo wengine wanaikataa, inakuwezesha kufanya makubwa na kupata matokeo bora. Kero unayokubali kutoa kwa wengine, bila ya kufikiria watakuchukuliaje, inakupa wewe uhuru wa kuchukua hatua.

Mara zote fanya lile lililo sahihi, hata kama hupendi au kuna baadhi ya watu hawapendi. Lililo sahihi ndilo linaloleta mafanikio.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog