When you are offended at any man’s fault, turn to yourself and study your own failings. Then you will forget your anger. – Epictetus
Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo. Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya nakubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari HATA WEWE UNAKOSEA…
Wapo watu ambao wanatukosea kwenye mambo mbalimbali kwenye maisha yetu.
Ni rahisi sana kwetu kuwalaumu na kuwahukumu watu kwa yale makosa ambayo wanakuwa wameyafanya.
Tukishajua kwa hakika watu wametukosea, basi tunaweza kuwabebesha lawama ambazo hata hawastahili.
Hii ni kutaka tu kujiridhisha kwamba sisi hatuna hatia na tumeonewa.
Tunachosahau ni kwamba, sisi wenyewe kwa nyakati mbalimbali tumekuwa tunakosea.
Tumekuwa tunawakosea wengine kwa mambo mbalimbali.
Lakini tumekuwa tunafikiri makosa yetu si makubwa sana, na yanastahili kusamehewa au kutochukuliwa kwa uzito sana.
Lakini makosa ya wenzetu tunayachukulia kwa uzito.
Mtu anapokukosea, na ukajua kabisa amekukosea, iwe amekiri au hakukiri, kabla hujaendelea kumpa kila aina ya lawama zako, kumbuka kwamba hata wewe umekuwa unakosea, unakosea mara nyingi sana na wakati mwingine watu wanakuacha tu, hawayapi uzito sana makosa yako.
Kukosea ni ubinadamu, hivyo usitake kumkandamiza yeyote anayekukosea.
Uwe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kurasa