Waliosema mwanzo ni mgumu walikuwa sahihi kabisa.
Kitu chochote ambacho kinafanywa kwa mara ya kwanza huwa kigumu. Na hata mwanzo wa kufanya kitu huwa ni mgumu kuliko mwendelezo.
Mashine zinarahisisha kazi, lakini utatumia nguvu nyingi kuiwasha mashine kuliko nguvu inayotumika kuifanya mashine iendelee kwenda.
Utatumia nguvu nyingi kumpata mteja wa kwanza wa biashara yako, au kumshawishi mteja kununua mara ya kwanza kuliko nguvu unazohitaji kumfanya aendelee kununua.
Hivyo basi rafiki, unapoanza jambo lolote na ukakutana na ugumu mwanzoni, usikate tamaa na kuona hutaweza. Jua kabisa ya kwamba ugumu huo ni kwa mwanzo, mbeleni mambo hayatakuwa magumu kama unavyoyaona mwanzo.

Watu wengi wamekuwa wanapoteza nguvu kubwa wanayoweka mwanzo, kwa kuacha au kukata tamaa mapema. Wanakuwa wameshaweka ile nguvu kubwa ya mwanzo, na kabla hawajafika kwenye urahisi wanakata tamaa na kuacha.
SOMA; UKURASA WA 53; Hakuna Kinachodumu Milele…
Kila ugumu unaoupitia jua ni matunda mazuri ya baadaye. Kama utaweza kuvuka ugumu huo bila ya kukata tamaa, hutakwamishwa tena na ugumu wa aina hiyo. unakuwa umevuka ngazi ya chini na kwenda ngazi ya juu zaidi.
Na wenye hasara zaidi ni wale ambo hata hawaanzi kabisa. Wao kwa kufikiria ugumu wanaoweza kukutana nao na kuchanganya na hofu zinazokuwa zimewatawala, wanajitangazia hawawezi au hawapo tayari. Hawa ndiyo wanaokosa kabisa kujifunza na hata kupiga hatua.
Haijalishi kitu kinaonekana kigumu kiasi gani, haijalishi mwanzo unakuwa mgumu kiasi gani, kinachojali na cha muhimu, ni wewe kupita ugumu huo na kukutana na urahisi mbeleni. Maana bila ya kupita ugumu huo, hutafika kabisa kwenye urahisi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog