Mtu mmoja amewahi kusema kwamba tabia ni kama uzi mwembamba, ambao unajisokotea kidogo kidogo kila siku. Ni rahisi kukata uzi huo unapokuwa umejisokotea kidogo, lakini kadiri unavyozidi kusokota, ndivyo inavyokuwa vigumu kuukata.

Katika kujenga tabia na hata kwenye hatua tunazopiga au kuacha kupiga, siku moja inaweza kuonekana kama siyo kitu.

Njia Panda

Siku moja ya kufanya kazi yako kwa juhudi kubwa, kutoa thamani kubwa na kufanya mambo yako kwa uadilifu inaweza kuonekana kama siyo kitu. Kwa sababu hutayaona matokeo ya kile unachofanya ndani ya siku moja.

Siku moja ya kufanya mambo yako kwa uzembe inaweza isilete matokeo yatakayokustua kwamba unakoelekea siko. Siku moja ya kutafuta njia ya mkato ya mafanikio inaweza kuonekana kitu cha kawaida. Siku moja ya kuwadhulumu wengine inaweza kuonekana ni faida na ujanja, kupata kile ambacho hukustahili kupata.

Lakini kadiri unavyoendelea kufanya, ndivyo unavyozidi kutengeneza matokeo yanayotokana na kile unachofanya. Labda ndani ya mwaka mmoja utaanza kupata matokeo ya tofauti, labda utaanza kuona dalili za mbali sana, lakini hazitakustua sana.

Ni miaka kumi ndiyo itakayokustua na kukuonesha ni kiasi gani umepiga hatua au umepotea. Kama utaziishi siku zako kwa namna unavyoziishi, kwa miaka kumi ijayo, utakuwa umepiga hatua kubwa sana au utakuwa umepotea sana kulingana na kile unachofanya.

SOMA; UKURASA WA 1009; Matokeo Ni Muhimu Zaidi Kuliko Maelezo…

Baada ya miaka kumi utaangalia ulipotokea na kuona namna gani mambo yameenda. Hapo ndipo unapoona kwamba umefanya kazi au biashara kwa muda mrefu lakini bado upo pale pale. Au ndipo utakapoona yale matendo madogo madogo ya uaminifu uliyokuwa unafanya kila siku, yamepelekea wengi kukuamini na kushirikiana na wewe kwenye mambo mbalimbali.

Hivyo rafiki yangu,  ni vigumu sana kuona matokeo ya kile unachofanya ndani ya siku moja. Kama unafanya mazuri usikate tamaa na kuona hayana matokeo, matokeo yanaitengeneza. Na pia kama unafanya mabaya usijisifu kwamba hakuna anayekuona au anayejua, itafika wakati kila mtu atajua.

Chochote unachofanya, fikiria miaka kumi ijayo, huo ndiyo wakati ambao utakuwa umepata matokeo makubwa kulingana na chochote unachofanya.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog