Let not your mind run on what you lack as much as on what you have already. – Marcus Aurelius

Habari za asubuhi ya leo rafiki yangu?
Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari ANGALIA ULICHONACHO NA SIYO ULICHOKOSA…
Akili zetu zimetengenezwa kuangalia hatari na kile kinachokosekana.
Ndiyo maana mtu anaweza kufanya mazuri na makubwa, lakini akakosea kidogo, watu wakaachana na mazuri yote na kuhangaika na alichokosea.

Kadhalika kwetu binafsi, watu huwa tuna vitu vingi, lakini huwa hatufikirii vile tulivyonavyo.
Badala yake tunafikiria vile tulivyokosa.
Na kwa kuwa hakuna wakati mtu anaweza kuwa na kila anachokitaka, wengi wamekuwa wakiishi maisha yasiyo na kuridhika.

Kwa kuwa pia mawazo yetu ni sumaku, yanavutia kile tunachofikiri muda mrefu, unapofikiri kile ulichokosa, unavutia kukosa zaidi.
Haijalishi unakosa vitu vingi kiasi gani, kuna vitu ambavyo tayari unavyo.
Ukivifikiria hivyo na kuvitumia vizuri, utaweza kupiga hatua zaidi.

Lakini kama utafikiria yale uliyokosa, utaendelea kukosa zaidi.
Fikiria zaidi kile ambacho tayari unacho, angalia ni kwa namna gani unapiga hatua zaidi kwa kuanzia pale ulipo sasa.

Uwe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha