It is not because things are difficult that we do not dare, it is because we do not dare that they are difficult – Lucius Annaeus Seneca
Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?
Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo. Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari SIYO UGUMU NI UTHUBUTU…
Kuna wakati hatuthubutu kufanya au kujaribu vitu fulani kwa sababu tunaona ni vigumu.
Tunaona tutashindwa au hatutaweza kupata kile tunachotaka kupata.
Lakini ukweli ni kwamba, siyo kwamba ugumu ndiyo unatufanya tusithubutu, badala yake kutokuthubutu kwetu ndiyo kunafanya mambo yawe magumu.
Yaani mambo yanakuwa magumu kwa sababu hatujathubutu kuyafanya. Lakini wakati huo tunajidanganya kwamba hatuthubutu kufanya kwa sababu mambo ni magumu.
Chochote unachoona ni kigumu, wewe thubutu kuanza kukifanya. Kigawe kwenye mafungu madogo madogo kisha anza kufanya. Weka juhudi na kuwa mvumilivu na hakika utaona namna ambavyo ni rahisi na inawezekana kabisa kufanya.
Kipi ambacho umekuwa unashindwa kufanya kwa muda mrefu kwa kuamini kwamba ni kigumu? Hebu thubutu leo kuanza na utaona namna gani ugumu uliokuwa unaifikiria upo ndani ya akili yako tu, na siyo uhalisia.
Ukawe na siki bora sana ya leo, siku yenye uthubutu wa hali ya juu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha