Wanasema kwamba njia bora ya kulipa kisasi kwa watu waliokusumbua au kukukwamisha kwa namna yoyote ile, ni kuwa na mafanikio makubwa sana.
Tumekuwa tunafikiri hivi kwamba kama kuna mtu anatusumbua, amewahi kutunyanyasa kwa namna yoyote ile, basi tukikazana na kufanikiwa tutamfundisha somo. Tutamwonesha kwamba alikosea sana kutufanyia kile alichofanya.
Lakini hivi sivyo mambo yanavyokwenda, hakuna mtu yeyote ambaye unamfundisha somo lolote kwa njia hiyo unayofikiria. Kwa sababu anayekusumbua au kukupinga kabla hujafanikiwa, ataendelea hivyo hata baada ya wewe kufanikiwa.

Kitakachofanyika ni atabadili njia ya kukusumbua au kukukataa. Anaweza kusema njia uliyotumia kupata mafanikio siyo sahihi, au mafanikio hayo umeyapata kwa bahati. Au mbaya zaidi wanaweza kusema kama siyo wao kukusukuma usingefanikiwa.
SOMA; UKURASA WA 920; Ukweli Haumbadilishi Mtu Huyu…
Sasa unapokuwa umeyaweka maisha yako yote kwa kusudi la kuwafundisha watu somo, kwa kusudi la kuwaonesha kwamba walikosea na wanapaswa kujifunza, utakuwa umechagua kupoteza maisha yako. Kwa sababu hutafikia hilo na chochote ambacho umefanyia kazi utaona hakijaleta mafanikio.
Kama yupo mtu amekunyanyasa au kukuzuia kwa namna yoyote ile usipate mafanikio, kitu bora kwako kufanya ni kumsamehe na kuachana naye. Halafu wewe kazana kuwa bora zaidi, siyo kwa sababu yao, bali kwa sababu zako binafsi, kwa sababu umechagua kuwa bora.
Iwe watajifunza au hawatajifunza hilo halihusiani na wewe, lipo nje ya uwezo wako na huwezi kuliathiri kwa namna yoyote ile.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog