Watu wengi wamekuwa wakijinyima vitu wao wenyewe. Unakuta mtu kuna kitu anataka kutoka kwa mtu mwingine, lakini anajiambia hawezi kunipa, au hatakubali, halafu anaishia hapo.
Ukiangalia hapo, unachoona ni kwamba mtu amechagua kujinyima yeye mwenyewe. Hajamuuliza mtu yule kitu, lakini amekuja na majibu kwamba atakataa au hatokubali.
Kuna kitu kinawafanya watu wajinyime vitu wao wenyewe, kitu hicho ni hofu ya kukataliwa. Watu wengi wanapofika hatua ya kuomba kitu kwa mtu, huwa wanakuwa na hofu kwamba huenda mtu yule atakataa. Hofu hii ni kubwa sana kiasi kwamba wengi hawathubutu kabisa kuchukua hatua.
Wapo watu ambao wamekosa biashara nzuri kwa kuogopa kuuliza, wapo watu wamekosa kazi nzuri kwa kuogopa kuomba. Na pia wapo watu ambao wamekosa wenzi wazuri kwao kwa kuogopa kuwaambia wanawapenda. Hofu hii ya kukataliwa imekuwa kikwazo kwa wengi kupata kile hasa wanachokitaka.

Leo nakwenda kukupa dawa kamili ya hofu hii ya kukataliwa, ili isiwe kikwazo kwako kufanikiwa.
Dawa hii inahusisha vitu viwili muhimu;
Moja; tambua kwamba mtu anapokataa kitu unachomwambia, hajakukataa wewe kama mtu, hajasema kwamba hufai kabisa, hajamaanisha wewe ni mtu wa hovyo na usiyefaa kwa lolote. Bali alichomaanisha ni kwamba, kwa kile ulichomweleza, siyo anachohitaji au kwa namna ulivyomweleza hujaweza kumshawishi mpaka achukue hatua.
Kwa kutambua hili inakuondolea mzigo mkubwa kwa sababu utaacha kuona kama watu wanakukataa wewe na pia utajifunza zaidi pale watu wanapokataa. Utajifunza kuwajua watu sahihi na pia utajifunza njia bora za ushawishi kwa wengine.
SOMA; Hizi ndio Hofu mbili ulizozaliwa nazo, nyingine ni uongo.
Mbili; tambua kwamba neno kubwa unalohofia ni HAPANA, ambalo utalipata hata kama hutaomba au kuuliza. Kama utamwuliza au kumwomba mtu kitu, anaweza kusema NDIYO, na mambo yako yakawa vizuri, au anaweza kusema HAPANA. Kama hutamuuliza kabisa, jibu moja kwa moja ni HAPANA. Hivyo basi, kama hutauliza jibu ni hapana, kama utauliza, huenda ukapata jibu la ndiyo, sasa kwa nini usiulize?
Uliza ukiwa unajua kwamba hata kama utakataliwa, hicho ndiyo ambacho kingetokea kama usingeuliza. Lakini kwa kuuliza una nafasi ya kupata ndiyo, na hata ukipata hapana, una nafasi ya kujifunza kwa nini mtu amesema hapana na hivyo kubadilika na kuwa bora zaidi.
Usikubali tena hofu ya kukataliwa ikawa kikwazo kwako kupata kitu chochote unachotaka kwenye maisha yako. Uliza, omba bila ya kuhofia kuambiwa hapana, kwa sababu utaipata hapana hata kama hutaomba au kuuliza.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog