Katika safari ya mafanikio, ni vyema ukatambua ipo misingi ya mafanikio ambayo ukiisimamia inakupa mafanikio hata bila ya wasiwasi. Watu wengi wanashindwa kwenye maisha kwa sababu tu ya kubomoa mara kwa mara misingi ya mafanikio.

Tambua hivi, unapokuwa unabomoa msingi wa mafanikio, sio swala la kuuliza tena nini kitatokea, kushindwa kunakuhusu hapo. Ipo misingi mingi ya mafanikio ya kuizingatia, lakini leo naomba tujifunze misingi mitatu tu ambayo unatakiwa uizingatie sana.

vitabu softcopy

Heshimu vitu vidogo.

Moja ya msingi mojawapo ambao unatakiwa uuzingatie ili ukupe mafanikio ni kuheshimu vitu vidogo. Unatakiwa kuheshimu pesa zako hata kama ni kidogo, unatakiwa kuheshimu biashara yako hata ikiwa ni kidogo.

Unapokuwa unajenga dharau kwenye vitu vidogo, huko ni kujitengenezea kushindwa. kitu unachotakiwa ukumbuke mafanikio yanajengwa kwenye vitu vidogo sana ambavyo kuna wakati hata hufikirii, kama vinaweza vikakukapa mafanikio.

Angalia eneo ulipo na watu ulionao, wapo watu ambao walianza na vitu vidogo sana hadi wakafanikiwa. Kilichoweza kuwafanikisha si kitu kingine bali ni heshima ya vitu vidogo.Kwa hiyo,  heshima katika mafanikio ni kitu cha msingi sana.

Heshimu uwezo wako.

Wapo watu ambao hawako tayari hata kidogo kuheshimu ule uwezo walionao ndani mwao. Hapo ulipo unao uwezo mkubwa sana. Amua kuheshimu uwezo wako na kuutumia ili kufanikisha kile unachotaka.

Anza kukaa chini na kuangalia ni kitu gani ambacho unacho ndani mwako na unaweza ukakitumia na kuweza kukusaidia kufanikiwa. Je, ni kipaji na kama ni kipaji ni kipaji cha aina gani ambacho unacho? Ukishagundua hilo anza kukutumia kupata matokeo uyatakayo.

Kwa kadri,  utakavyokuwa ukitumia ule uwezo wako wote ndani mwako yaani unajikamua mpaka mwisho, utashangaa unavuta mafanikio makubwa. Usiishie kuona wengine wana uwezo mkubwa hata wewe uwezo huo unao, kikubwa utumie.

Wakati wote kuwa mkarimu.

Pia msingi mojawapo wa mafanikio ambao unatakiwa kuwa nao ni kwa wewe kukubali kuwa mkarimu. Kupiga kelele hovyo au kuwa mtu wa hovyo ni kitu ambacho kinaweza kukuangusha katika kuelekea mafanikio yako, ukarimu katika maisha unalipa.

Kuwa makarimu kwa watu wanaokuzunguka, kuwa mkarimu kwa wafanyakazi wako na hata bosi wako kama unae. Hapo utakuwa unapanda mbegu ya mafanikio kwa watu wengine ambao itakusaidia kufanikiwa kwako na kujenga msingi imara.

Kwa kuhitimisha makala haya, elewa hivi ikiwa wewe ni mtu wa kuheshimu vitu vidogo, kuheshimu uwezo wako na kuweza kujiamini kabisa na  mkarimu basi elewa moja kwa moja umepanda mbegu ambayo itakusaidia sana wakati wote kwenye mafanikio yako.

Fanyia kazi haya na chukua hatua kuhakikisha ndoto zako zinatumia.

Tunakutakia kila la kheri na endelea kutembelea AMKA MTANZANIA kila siku kujifunza maisha na mafanikio.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

Ni wako rafiki katika mafanikio,

Imani Ngwangwalu,

Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,

Tovuti; http://www.amkamtanzania.com,

Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713 048 035,

Email; dirayamafanikio@gmail.com