Katika kila aina ya fani, kuna makundi mawili ya watu.

Kuna watu ambao wamebobea kwenye fani hiyo, hawa ni wale ambao wameshajijengea majina kwenye kile wanachofanya. Hawa ni watu ambao watu wanawatafuta wanapokuwa na shida na wanatoa thamani kubwa.

Pia kuna ambao ni wachanga, hawa ni watu ambao wanaingia kwenye fani hiyo na bado hawajajijengea majina na hawajaweza kufanya makubwa kwenye fani hizo.

Kila Mtu

Sasa wengi hufikiri ubobezi kwenye kile wanachofanya unakuja tu kwa uzoefu, kwamba ukifanya kwa muda mrefu basi unakuwa na uzoefu na hivyo unakuwa mbobezi.

Watu hufikiri wakifanya kitu miaka kumi basi wanakuwa na uzoefu wa miaka kumi. Kumbe ukweli ni kwamba wanakuwa na uzoefu wa mwaka mmoja waliourudia kwa miaka kumi. Kwa sababu kila mwaka wanafanya yale yale.

SOMA; UKURASA WA 959; Jitangazie Uhuru Huu Muhimu Sana Kwa Mafanikio Yako…

Ninachosema hapo juu ni kwamba, mtu anaweza kuwa amefanya kitu kwa miaka 10, lakini bado akawa ni mchanga, akawa hajabobea bado.

Tofauti ya wabobezi na wachanga inatokana na namna wanavyofanya mambo yao.

Wabobezi wana ujuzi, uzoefu na wanajua namna ya kukaa chini na kufanya kitu kila siku. Wanapanga kufanya kitu na wanakifanya kweli, wao ni watu wa vitendo pekee.

Wachanga wao wanapanga kufanya na wanasema watafanya, ila hawajui namna ya kukaa chini na kufanya kitu. Watapanga na kupangua, watasema na kuahidi, lakini kukaa chini na kufanya ndiyo changamoto kubwa kwao.

Kama bado hujaweza kukaa chini na kufanya kitu kila siku, iwe unajisikia kufanya au hujisikii kufanya, wewe bado ni mchanga. Kama bado unafanya mambo pale unapokuwa na msukumo, au kwa sababu muda umefika ukongoni, bado wewe ni mchanga.

Jifunze namna ya kukaa chini na kufanya kitu kila siku, jifunze namna ya kuwa mfanyaji na siyo msemaji pekee, na hapo utakuwa umeufikia ubobezi kwenye chochote unachofanya.

Kumbuka, kwenye fani yoyote, wabobezi wana mafanikio makubwa sana ukilinganisha na wale ambao ni wachanga. Kila mwenye uhitaji, anawaangalia wabobezi na siyo wachanga. Kuwa mbobezi uweze kunufaika na kazi unayofanya.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog