Moja ya vitu vinavyowasukuma wengi kudanganya au kutafuta njia zisizo sahihi za kufanya mambo, ni kuwaonea wengine aibu. Kuona kama wengine wakijua ukweli ulivyo, basi watawadharau na kuona hawafai.

Hivyo watu wanadanganya, au kuigiza mambo ili wengine wasiwachukulie kwa namna ya tofauti. Kwa kudanganya huko au kuigiza, watu kwa nje na kwa muda wanaweza kudanganyika. Lakini mara zote, ukweli huja kuwa wazi baadaye, na watu hupoteza imani zaidi wanapogundua mtu alidanganya au kuigiza ili achukuliwe kwa namna fulani.

Pia hii ni njia ya kujitengenezea utumwa mkubwa, ambao unamnyima mtu uhuru wa kuweza kuchukua hatua na kuyafanya maisha yake kuwa bora. unakutana na fursa nzuri lakini huwezi kuchukua hatua kwa sababu umeshawatengenezea watu picha tofauti kuhusu wewe, ambayo kwa kuchukua fursa hiyo utaiharibu.

Njia Panda

Na kibaya zaidi, unapodanganya, au kuigiza, inabidi uendelee kudanganya zaidi na kuigiza zaidi ili watu wasigundue ukweli. Na kadiri uongo na maigizo yako vinavyokua, ndivyo inavyokaribia hatua ya kuanguka na ukweli kujulikana.

Ninachoweza kukuhakikishia ni kwamba, iwapo umedanganya au unaigiza, ni swala la muda tu, lakini kila kitu kitakuja kujulikana.

SOMA; UKURASA WA 984; Usinunue Hofu Za Wengine…

Hivyo basi rafiki yangu, mtu pekee unayepaswa kumwonea aibu ni wewe mwenyewe, kujiuliza utaishije baada ya uongo unaotaka kutengeneza kuanguka? Kabla hujaigiza jiulize je watu wakija kujua ukweli, kitu ambacho lazima kitokee, watakuchukuliaje?

Ukijiuliza hayo, utaona aibu na kufanya lililo sahihi.

Kumbuka unaweza kumdanganya kila mtu hapa duniani kwa muda fulani, lakini huwezi kujidanganya wewe mwenyewe hata kwa dakika moja. Ukweli utaendelea na wewe na utaendelea kuumiza. Wakati unadanganya na kuigiza kwa nje, nafsi yako inakuambia wewe ni mtu wa hovyo, na hilo litakuumiza sana.

Mtu pekee wa kumwone aibu kwenye maisha yako ni wewe mwenyewe, na unahitaji kuishi maisha ambayo yanaendeshwa kwa msingi wa ukweli na kujiamini, kwa popote ulipo na lolote unalopitia.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog