A gem cannot be polished without friction, nor a man perfected without trials. – Lucius Annaeus Seneca

Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Leo tumepata nafasi nyingine nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari; KITU HUNG’ARISHWA KWA KUSUGULIWA….
Kila kitu kwenye maisha, hung’arishwa kwa kusuguliwa.
Ili kitu kiwe safi na king’ae, kinahitaji kusuguliwa.
Kuondoa kila aina ya uchafu, lazima kitu kisuguliwe sana.

Madini hufanywa kuwa safi kwa kusuguliwa,
Hata samani hufanywa kuwa nzuri kwa kusuguliwa.
Kadhalika, hata vyombo vya chakula, hufanywa kuwa safi kwa kusuguliwa.

Hivi pia ndivyo ilivyo kwetu sisi binadamu,
Tunafanywa kuwa safi kwa kusuguliwa,
Tunakuwa bora na kung’aa sana baada ya kusuguliwa.

Hivyo unapoona unapitia magumu kwenye maisha yako, jua ni wakati wa kusuguliwa.
Jua ndiyo unang’arishwa zaidi, na baada ya ugumu huo, utakuwa mtu bora kabisa.

Mara nyingi kinachotuzuia kufanikiwa ni fikra na imani ambazo tumejenga kwenye akili zetu tangu tukiwa watoto.
Bila ya kusuguliwa na kuondokana na fikra na imani hizi, mtu huwezi kufanikiwa.

Kwa mfano mtu ambaye tangu ukiwa mdogo umekuwa unaimbiwa wimbo huu; nenda shule, soma kwa bidii, ufaulu vizuri na utapata kazi nzuri na kuwa na maisha ya mafanikio
Unatimiza hivyo, unapata kazi lakini maisha yanakuwa magumu na kazi hairidhishi wala huipendi.
Lakini bado mtu unakazana na kazi hiyo kwa sababu hujawahi kufikiria maisha mengine nje ya mfumo huo wa kazi.
Inapotokea matatizo kwenye kazi yako, na ikapelekea wewe kuikosa kazi, hapo ndipo unapokuwa umepata kusuguliwa, kwani pamoja na kwamba mambo yatakuwa magumu, lakini utajifunza njia nyinyine za kujipatia kipato.
Zile fikra na imani kwamba ajira pekee ndiyo tegemeo lako, zinasuguliwa na kuondolewa kabisa.

Hivyo rafiki, unapopitia ugumu kwenye maisha yako, jiulize je ni kitu gani kinasuguliwa na kuondolewa kwenye maisha yako?
Ukijua hili mapema, hutateseka kabisa kwenye maisha yako, na utarahisisha zaidi zoezi la kusuguliwa, utapunguza vipindi vya magumu.

Ukawe na siku bora sana ya leo rafiki.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha