Kila mtu anaishi, lakini ni wachache sana ambao wanaishi maisha yao halisi, wengi wanaishi maisha ambayo siyo yao, maisha ambayo hawayafurahii, lakini inawalazimu kuyaishi, wakiamini yatawafanya kuwa bora.

Lakini hayawafanyi kuwa bora, badala yake yanafanya maisha yao kuwa magumu zaidi na kukosa furaha na mafanikio.

Zawadi Kubwa

Kuna vitu vitatu unapaswa kuvipotezea ili kuishi maisha yako, kuishi maisha ambayo yatakuwa na maana kwako, yenye furaha na mafanikio makubwa.

Kitu cha kwanza; chuki.

Kuna watu watakuwa na chuki na wewe haijalishi unafanya nini. Wao watatokea tu kukuchukia na kukupinga kwa chochote unachofanya. Fanya kazi yako kwa kujituma watasema unajipendekeza, fanya kazi yako kwa kutokujituma watasema ni mvivu. Watu wenye chuki ni watu unaopaswa kuwapotezea, kwa sababu hakuna chochote unachoweza kufanya kikabadili chuki zao. Kumbuka chuki ni zao, na zinawaumiza wao, wewe ishi maisha yako.

Kitu cha pili; mazoea.

Ukifanya kitu chochote ambacho kimezoeleka kufanyika, utapata matokeo ambayo yamezoeleka kupatikana. Kufanya kile ambacho umekuwa unafanya, utaendelea kupata matokeo ambayo umekuwa unapata. Hivyo kama unataka kupiga hatua, kuwa na maisha bora na yenye furaha, usijifungie kwa chochote kile. Badala yake kuwa bora zaidi kwa kujifunza na kujaribu vitu vipya zaidi.

SOMA; Njia 30 Za Kufikia Mafanikio Makubwa Sana(World Class)

Kitu cha tatu; kundi.

Binadamu sisi ni viumbe wa kijamii, tunajisikia salama tunapokuwa ndani ya kundi kubwa la watu. Hivyo tumekuwa tunakazana kufuata kundi, kufanya yale ambayo wengi wanafanya, tukiamini ndani ya kundi kuna usalama. Hata hivyo si wanasema kifo cha wengi harusi? Ni rahisi kusikia ule usalama wa ndani ya kundi, lakini pia kundi ni kikwazo kwako kuchukua hatua na kufanikiwa. Kama unataka kufikia ule uwezo mkubwa ulipo ndani yako, lazima uwe tayari kwenda kinyume na kundi, lazima uwe tayari kusimama mwenyewe, kutetea kile unachoamini. Na kama utakuwa umewapotezea wenye chuki, na umepotezea mazoea, hili litakuwa rahisi kwako.

Hayo hapo, mambo matatu, yapotezee ili uwe na maisha bora.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog