Unapokutana na marafiki au jamaa zako, huwa mijadala yenu imetawaliwa na nini? Kwa wengi, mijadala wanayokuwa nayo wanapokutana imegawanyika kwenye makundi mawili, kutoroka na kujisumbua.
Mijadala ya kutoroka ni ile ya kulalamika na kulaumu, hii ni mijadala inayotufanya tuone kwamba sisi hatuna tatizo bali wengine ndiyo wanatuletea matatizo. Kwa mijadala hii tunajiaminisha kwamba kama isingekuwa watu fulani au hali fulani basi tungekuwa mbali sana.
Mijadala ya kujisumbua ni ile ambayo inafanya akili zetu zisifikirie yale ambayo ni muhimu. Hii ni mijadala ya kutuweka ‘bize’ ili tusipate muda wa kufanya mambo ambayo ni muhimu kwetu kufanya, lakini ni magumu. Mijadala hii ni ile inayohusu michezo na hata maisha ya wasanii au watu wengine maarufu.

Najua unajua kitu kikubwa ambacho nimekuwa nakuambia ni usilalamike wala kulaumu, kama kuna kitu hupendi kibadili na kama huwezi kukibadili basi achana nacho. Na pia nimekuwa nakuambia usipoteze muda kwa mambo yasiyokuhusu au usiyoweza kuyaathiri.
Wewe kama wewe unaweza kuelewa hili, na ukaona umuhimu wake. Changamoto ni kwa wale wanaokuzunguka, wale ambao unatumia nao muda mrefu. Hawa wanaweza kuwa na mijadala hii ambayo wewe umechagua kuachana nayo wakati wewe upo.
Najua huwezi kumpangia kila mtu ajadili nini au afuatilie nini, lakini kama utawavumilia watu kwenye mijadala ya aina hiyo, basi utakuwa sehemu ya mijadala hiyo.
Unaweza kuwa kwa ndani huitaki na unakazana sana kuiepuka, lakini wao wanaendelea kukuletea mijadala hiyo. na kwa kuwa hutaki kuwaudhi, basi unawasikiliza. Usichojua ni kwamba unapowavumilia na kuwasikiliza, wanajifunza kwamba ni kitu unapenda na wataendelea kukuletea mijadala ya aina hiyo.
SOMA; UKURASA WA 688; Unapata Kile Unachovumilia…
Hivyo kama utavumilia mijadala usiyokubaliana nayo, utaendelea kuipata zaidi na zaidi.
Dawa ya mijadala ya aina hii ni kutokuvumilia, kuwaeleza watu ukweli kwamba huhitaji mijadala ya aina fulani. Wanaweza kuchukia au kujisikia vibaya, lakini wataheshimu maamuzi yako na hawatakuhusisha tena kwenye mijadala hiyo.
Utaendelea kupata unachoweza kuvumilia, hivyo kama kuna kitu unakipata na hukipendi, jua kuna namna umekuwa unakivumilia. Acha kukivumilia na utaweza kuondokana nacho.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog