Never in any case say I have lost such a thing, but I have returned it. Is your child dead? It is a return. Is your wife dead? It is a return. Are you deprived of your estate? Is not this also a return? – Epictetus
Hongera rafiki yangu kwa siku hii nzuri na ya kipekee sana kwetu.
Ni nafasi nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana leo na kila siku ya maisha yetu.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Mwongozo wetu wa mwaka 2018 ni TATUA, AMUA NA ONGOZA ambapo tutaweza kupiga hatua zaidi kwa kuzingatia haya.
Asububi ya leo tutafakari kuhusu HUJAPOTEZA, BALI UMERUDISHA…
Tumekuwa tunajidanganya sana eneo moja, kwamba chochote ambacho tunacho, ni chetu na hivyo tunapaswa kuwa nacho kwa namna tunavyotaka sisi wenyewe.
Lakini hilo haliwezekani kwa yeyote yule. Kuna kipindi utakuwa na vitu fulani na kuna kipindi hutakuwa navyo.
Kipindi unapokuwa na vitu, siyo vyako milele, bali vimewekwa chini yako kwa muda, umepewa nafasi ya kuvisimamia kwa muda huo.
Na kipindi vitu hivyo vinapoondoka kwako hujavipoteza, badala yake umevirudisha kule vilipotoka.
Mtazamo huu juu ya vitu ni muhimu sana kwa sababu utakusaidia wewe usiumie sana pale kitu ulichokuwa nacho umekikosa. Usipate msongo wa mawazo na hata magonjwa kama presha na kiharusi kwa sababu umeshtushwa na kitu ulichokosa.
Inapotokea umepata taarifa kwamba fedha ulizokuwa nazo huna tena, au nyumba uliyokuwa nayo imeungua moto, unajua kwamba hujapoteza, bali umerudisha. Na kwa kuwa upo hai, basi utapata vingine vizuri zaidi.
Hata pale unapopata msiba wa mtu wa karibu yako kabisa, hujapoteza, bali umerudisha, kwa sababu hukumtengeneza mtu huyo kwenye maisha yako, uliletewa.
Huenda unarudisha kizuri ili upate kilicho bora.
Pia huenda kurudisha kwako ni somo kwako kujua umuhimu wa vitu wakati uko navyo.
Kwa vyovyote vile, jua ulichonacho sasa, unacho kwa muda, ambao huujui, lakini kuna wakati utarudisha.
Lakini pia hili lisikufanye uwe mzembe, uchukulie vitu hovyo kwa sababu unajua hutakaa navyo muda mrefu.
Badala yake inakupasa uwe makini sana na vitu, kwa sababu ukishavipoteza, hutavipata tena.
Uwe na siku njema sana rafiki yangu,
Kumbuka NUK-TAO, huu ndiyo mpango mzima wa maisha yanmafanikio kwa mwaka huu 2018 na kuendelea.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha