Huwa ninaamini kwamba, kila mmoja wetu ana kitabu ndani yake. Wewe hapo ulipo ni kitabu kinachotembea. Tangu kuzaliwa na kupata utambuzi mpaka hapo ulipo sasa, kuna mambo mengi sana ambayo umekutana nayo kwenye maisha, ambayo siyo kila mtu ameweza kukutana nayo.

Lakini pia, hutaishi milele hapa duniani, hivyo yale uliyojifunza kwenye maisha, yanaweza kupotea haraka sana pale utakapoondoka hapa duniani. Na huenda watoto au wajukuu zako wasipate kunufaika na mambo hayo.

Hivyo, njia pekee ambayo nimekuwa nasema ni ya mtu kuweza kuishi milele, ni kuandika. Leo hii tunajifunza kupitia maisha ya watu walioishi miaka mingi iliyopita. Kama wewe ni Mkristo, unajifunza mengi kupitia maisha ya Yesu, ambaye unamjua kupitia maandiko yaliyoandikwa kuhusu yeye. Kama wewe ni Mwisilamu, unajifunza mengi kupitia maisha ya Mohammad ambaye aliishi miaka mingi iliyopita, lakini leo unaweza kujifunza kwake kupitia maandiko.

andika kitabu

Tangu enzi na enzi, maandiko yamekuwa njia kuu ya kufundisha na kupeana taarifa. Watu walikuwa wakiandika kwenye mawe, magome ya miti na mapangoni. Baadaye watu walikuwa wakiandika kwenye makaratasi. Lakini sasa hivi, imekuwa rahisi zaidi kwani watu wanaandika hata kwenye simu zao za mkononi.

Hivyo rafiki yangu, kama unataka kuishi milele, kama unataka kile ulichojifunza kwenye maisha yako kiweze kuwasaidia vizazi vinavyokuja, basi huna budi kuandika.

Lakini wengi wanaposikia kuandika ni kama wanapata ganzi, wakiangalia jinsi vitabu vilivyo vikubwa, kurasa mia tatu na kuendelea. Hapa wengi hujiuliza hivi mimi naweza kuandika kurasa mia tatu kweli? Kwa wingi huo, wengi wanajiambia kwamba hawawezi, na hivyo ndoto zao za uandishi zinaishia hapo.

Leo nataka kukuonesha ni kwa namna gani, ndani ya mwaka mmoja, unaweza kukamilisha kuandika na hata kuchapa kitabu chako. Kwenye makala hii, nakupeleka hatua kwa hatua, jinsi ya kupata wazo la kuandika kitabu, kukiandika, kukihariri, kukichapa na hata kukitangaza, kama unataka kukiuza kwa wengi.

Karibu kwenye makala hii, ujifunze na kuweza kuchukua hatua.

Hatua ya kwanza; wazo la kuandika kitabu.

Ni kweli kwamba ndani yako kuna kitabu, lakini je ni kitabu gani? Huwezi tu kuandika kitabu na kukiita jina lako, labda kama wewe tayari ni mtu mashuhuri, ambaye watu wanataka kujua kuhusu wewe.

Kama bado hujafikia ngazi hiyo ya umashuhuri, basi unahitaji kuja na wazo jingine la kuandika kitabu chako. Na hapa unahitaji kufikiri kwa kina ili kuja na kitu ambacho kitawasaidia watu.

Njia bora ambayo huwa nawashauri wengi kwenye kuja na wazo la kuandika ni kujiuliza hivi; ni kitu gani ambacho kipo ndani yako ambacho unatamani kila mtu duniani angepaswa kukijua? Ni kipi ambacho unakijua wewe, kupitia kujifunza na uzoefu, ambacho unakiamini sana na unatamani kila mtu duniani angekijua?

Njia nyingine ya kujua hili ni kujiuliza ni kitu gani kila ukisikia au kuona unapata hasira? Kwamba watu wanaamini na kufanya kitu ambacho siyo sahihi. Labda wanajidanganya au wanadanganywa, na kwa uzoefu wako, wanachofanya siyo sahihi.

Fikiria kwa kina eneo hilo, na utakuja na wazo sahihi kwako kuandika, kwa sababu utaandika kitu unachoamini kweli, na utakuwa unaongea na wale unaowaandikia moja kwa moja na watakusikiliza.

Baada ya kupata kile ambacho unataka kuandikia, kaa chini na tengeneza majina matatu ya kitabu. Pata majina matatu ili uweze kuchagua jina lipi unaenda nalo.

Kwa mfano, kama wewe ni mtu unayejihusisha na mambo ya fedha, labda unafanya kazi benki ambapo unahusika na mikopo, au unafanya kazi kwenye taasisi inayotoa mikopo, au unatoa mikopo, au umewahi kuwa kwenye mikopo na ikakusumbua sana. Sasa kila unapowaangalia watu wanaoteseka na mikopo, unapata hasira, na kuona kuna kitu watu hawa hawaoni, ambacho kinawafanya wateseke.

Hivyo unakuja na wazo la kuandika kitabu, cha kuwasaidia watu kuondokana na madeni au kuweza kuchukua mikopo ambayo ina faida kwao.

Hapa sasa unaweza kuja na majina mbalimbali ya kitabu.

Moja; ONDOKA KWENYE UTUMWA WA MADENI NA FIKIA UHURU WA KIPATO.

Mbili; MADENI; GEREZA ULILOJIJENGEA NA JINSI YA KUONDOKA KWENYE GEREZA HILI.

Tatu; MADENI MAZURI, MADENI MABAYA NA MKOPO SAHIHI KWAKO KUCHUKUA.

Kama unavyoona, majina yote hayo yanaongelea kitu kimoja, lakini kwa njia tofauti. Hivyo hapo utaona wale unaowaandikia watasukumwa zaidi na jina lipi.

Baada ya kuja na jina la kitabu, pangilia sura za kitabu chako.

Unaweza kuchagua idadi ya sura utakazo, lakini kwa urahisi wa uandishi, nakushauri uwe na sura kumi. Na kwa kila sura, uwe na vipengele vitatu.

Kwa mfano wetu wa madeni unaweza kuwa na sura zifuatazo;

UTANGULIZI.

MOJA; MAANA YA MADENI NA CHIMBUKO LAKE.

MBILI; KWA NINI WATU WENGI WANAINGIA KWEYE MADENI.

TATU; AINA ZA MADENI.

NNE; MADENI MABAYA NA JINSI YANAVYOKUANGUSHA.

TANO; MADENI MAZURI NA JINSI YA KUYATUMIA KUSONGA MBELE.

SITA; JINSI YA KUONDOKA KWENYE MADENI MABAYA.

SABA; VIGEZO VYA KUZINGATIA KABLA YA KUINGIA KWENYE MADENI MAZURI.

NANE; USIMAMIZI BORA WA FEDHA UNAZOPATA KWA NJIA YA MADENI.

TISA; JINSI YA KUWATUMIA WENGINE KUKULIPIA MADENI YAKO.

KUMI; UHURU WA KIFEDHA NA NAMNA YA KUUFIKIA.

Hii ni mifano ya sura ambazo unaweza kuwa nazo kwenye kitabu chako.

Kwenye kila sura, kuwa na vipengele visivyopungua vitatu. Hivyo jumla utakuwa na angalau vipengele 30 vya kuandika kwenye kitabu chako.

Katika hatua hii ya kwanza, unakuwa na jina la kitabu na sura za kitabu. Hatua hii inaweza kukuchukua wiki moja mpaka mbili.

Hatua ya pili; fanya utafiti wa kitabu chako.

Baada ya kuwa umepata jina la kitabu na sura za kitabu, fanya utafiti wa kitabu unachotaka kuandika

Hivyo  unahitaji kuingia ndani na kujifunza kuhusu kile ambacho unataka kuandikia kitabu.

Na sehemu ya kwanza kabisa, siyo GOOGLE, maana hapo ndipo wengi hukimbilia. Sehemu ya kwanza ni kutafuta vitabu ambavyo vimeandikwa kuhusu kile unachotaka kuandika katika vipindi tofauti.

Tafuta vitabu ambavyo vimeandikwa zaidi ya miaka 100 iliyopita, zaidi ya miaka 50, zaidi ya miaka 10 na pia vilivyoandikwa ndani ya miaka mitano iliyopita. Angalau pata vitabu vitano, ambavyo utavisoma na kuelewa kwa kina kile ambacho unataka kuandikia kitabu.

Hii ni hatua muhimu sana, kwa sababu hapa ndipo utajifunza na kuelewa kwa kina kile unachotaka kuandikia kabla hata hujakaa chini na kuandika. Na unaposoma vitabu hivi, soma kuelewa na andika yale ambayo umejifunza kwenye kila kitabu, na kwa namna unavyoweza kuyaeleza kwa ubora zaidi kwenye kitabu chako unachokwenda kuandika.

Hatua hii inaweza kuchukua wiki moja mpaka miezi mitano kadiri ulivyo na kasi. Kama unaweza kusoma kitabu kimoja kila siku, ndani ya wiki utakuwa umemaliza vitabu vitano. Kama utaweza kusoma kitabu kimoja kila wiki, basi ndani ya miezi miwili utakuwa umemaliza vitabu vitano.

Lakini kama wewe ni yule ambaye unasema huna muda wa kusoma kabisa, yaani umebanwa kweli kweli, basi nakuambia soma kitabu kimoja kila mwezi. Na ndani ya miezi mitano utakuwa umemaliza vitabu vitano. Hata kama umebanwa vipi, unaweza kusoma kitabu kimoja kila mwezi. Unachohitaji ni kusoma kurasa kumi tu kila siku, ambazo kila mtu anaweza.

Hivyo tukichukua wiki mbili au hata mwezi wa kuja na jina la kitabu na sura zake, kisha miezi mitano ya kufanya utafiti, tunapata miezi sita.

Hatua ya tatu; andika kitabu.

Hii ndiyo hatua wengi wanaiogopa, lakini ndiyo hatua rahisi kuliko zote iwapo umefanya utafiti wa kutosha. Hii ni hatua ambayo itaenda haraka kama umeelewa kwa kina kile unachoandikia na utafiti uliofanya.

Kurahisisha hatua hii fanya hivi, kwa kuwa una vipengele 30 vya kuandikia, amua kuandika kila kipengele maneno elfu 2 tu. Kwenye kila kipengele andika maneno elfu 2, na mpaka unafika mwisho unakuwa umeandika maneno elfu 60, ambayo kwa wastani ni kitabu cha kurasa zaidi ya 300.

Najua unajiuliza unawezaje kufikia maneno hayo elfu 60, au hata maneno elfu mbili kwa kila kipengele. Na hapo ni rahisi pia, unachokifanya ni wewe kuandika maneno 500 tu kila siku. Kila siku andika maneno 500 kulingana na kipengele ulichonacho. Usikazane kwenda zaidi ya hapo, lakini kama unaweza hakuna ubaya, lakini usichuke chini ya hapo.

Kwa wastani wa uandishi wa kawaida kabisa, maneno 500 yatakuchukua dakika 30 mpaka saa moja kuandika. Kitu ambacho kila mtu anaweza kukifanya, iwapo amejitoa kufanya.

Hivyo ukiandika maneno 500 kila siku, utahitaji siku 120 kukamilisha maneno elfu 60. Siku 120 ni miezi minne. Hivyo kwa miezi minne, unakuwa umekamilisha kuandika kitabu chako.

Muhimu; usifanye uhariri wakati huu wa kuandika, wewe andika, kazi ya kuhariri ni baadaye. Na ni vyema ukaenda maneno mengi zaidi ili kwenye uhariri upunguze yale ambayo hayana maana. Pia usisome maneno ya nyuma wakati wa uandishi, wewe nenda mbele tu.

Mpaka sasa kwa hatua hizi tatu, umeshatumia miezi 10.

Hatua ya nne; hariri kitabu chako, na tafuta mwingine wa kuhariri.

Baada ya kuwa umekamilisha kuandika kitabu chako, kisome mwanzo mpaka mwisho, bila ya kupunguza au kuongeza lolote. Ukishakimaliza sasa anza mwanzo kusoma tena na kila neno au sentensi unayokutana nayo na unaona haiko sawa, ifute au ibadili na kuwa bora zaidi. Fanya hivyo kwa kitabu kizima.

Jipe mwezi mmoja wa kufanya zoezi hili, kwa kutumia siku moja kuhariri sura moja na kuikamilisha.

Ukishakamilisha kuhariri, tafuta mtu mwingine wa kukusaidia kuhariri, awe ni mtu mwenye uelewa, na ambaye hatakuonea aibu kukukosoa. Kama una uwezo unaweza kuwalipa wahariri ambao ni wataalamu kwa kazi hiyo. Kama huna uwezo huo angalia mtu anayeweza kukusaidia hilo, ila awe na uwezo wa kufanya hilo.

Hatua ya tano; tengeneza mwonekano wa kitabu, tafuta mchapaji na anza kutengeneza mfumo wa masoko.

Baada ya kitabu kuwa kimekamilika kuhaririwa, sasa unahitaji kuwa na mwonekano mzuri wa ganda la nje. Na hapa unahitaji kufanya kazi na mtu mzuri kwenye uandaaji wa picha na maganda ya vitabu. Unahitaji kukaa naye chini, kumwelezea wazo lako na yeye atengeneze mifano isiyopungua mitatu ili wewe na watu wengine unaoweza kuwashirikisha uchague ganda zuri la kitabu chako.

Wakati huo pia unakuwa unatafuta mchapaji wa kitabu chako, ambaye ataweza kukuchapia vizuri kitabu chako. Kwenye uchapaji, kadiri unavyochapa vitabu vingi ndivyo bei ya kuchapa kwa kitabu kimoja inakuwa ndogo. Kwa mfano kitabu cha kurasa 300, ukitaka kuchapa nakala 500, mchapaji atakuambia anakuchapia kila nakala kwa shilingi elfu 6. Lakini kama utachapa nakala 1000, anaweza kukuchapia kwa shilingi elfu 5 kwa kila nakala moja.

Huu pia ndiyo wakati wa wewe kuandaa mfumo wa masoko wa kitabu chako. Jua utakiuza kwa njia gani na utawafikiaje wasomaji unaowalenga. Jua wasomaji watajuaje kuhusu kitabu chako.

Kama utasambaza mwenyewe, au utakuwa na mawakala, au utatumia maduka ya vitabu, vyote hivi unahitaji kuvipangilia mapema.

Pia unahitaji njia za wasomaji kujua una kitabu, na hapa nimekuwa nasisitiza uwe na blog ambayo unaitumia kutengeneza wasomaji wako. Kwenye blog hiyo unatengeneza wasomaji ambao wameshajua kuhusu wewe na hivyo ukiwaambia kitabu kipo tayari, watakuwa wa kwanza kununua na hata kuwaambia wengine.

SIRI KUBWA NINAYOKUPA; Anza na blog kabla ya kitabu, na njia rahisi ni kuanza blog kile kipindi unafanya utafiti wa kitabu chako. Kila unachojifunza kwenye utafiti, washirikishe wasomaji wako kwa njia ya makala. Nakuambua hapo utakuwa unaua ndege wawili kwa jiwe moja. Kwa sababu kwa miezi yote kumi ambayo unatafiti na kuandika kitabu, kama utakuwa unaandika hata makala fupi kila siku, utatengeneza wasomaji wengi, ambao baadaye watakuwa wanunuaji wa kitabu chako.

Hatua ya sita; uza na tangaza zaidi kitabu chako, kila siku.

Mwezi wa mwisho kwenye mwaka wako wa kuandika kitabu, unakuwa ni mwezi ambao unauza kitabu chako. Unakuwa tayari una kitabu na sasa kazi kwako ni kukiuza na kuwafikia wengi. Siri moja kwenye uuzaji wa kitabu, hakikisha kila kinayemhusu anakijua. Tumia kila njia kufikisha ujumbe wako kwa wasomaji wa vitabu kwamba kitabu chako kipo.

Na hili ni zoezi endelevu, hufanyi mara moja ukasema umeshamaliza, badala yake unahitaji kuendelea kufanya hivyo kila siku. Kila siku wakumbushe wasomaji wako na watu kwa ujumla kwamba kitabu kipo. Endelea kuandika makala zinazoelezea kitabu chako. Andika makala na toa mfano wa sura kwenye kitabu. Yaani asiwepo mtu ambaye anakujua halafu anakuuliza hivi wewe hunaga vitabu? Hapo utakuwa umeshindwa wewe.

Rafiki yangu, hizo ndizo hatua sita, za kukuwezesha kuandika kitabu bora kabisa na kuweza kukiuza ndani ya mwaka mmoja. Kama umeweza kusoma hapa, maneno zaidi ya elfu mbili, basi nakuambia kwamba, unaweza kuandika kitabu.

Na kama utakuwa unakwama popote, ninazo rasilimali za kukuwezesha wewe kukamilisha kitabu chako ndani ya mwaka mmoja. Na kama unahitaji kitabu kwa haraka na upo vizuri, yaani unajituma, ndani ya miezi miwili utakuwa umekamilisha kitabu chako.

Rasilimali hizi nilizoandaa kwa ajili yako zitakufaa;

  1. Kupata blog ambayo unaweza kuitumia kuandika na kutengeneza wasomaji wako, blog ambayo ipo tayari na kazi kwako ni kuandika tu fungua; http://mtaalamu.net/pata-blog/
  2. Kuweza kusoma kurasa kumi za kitabu kila siku, jiunge na kundi la KURASA KUMI ZA KITABU, kupata maelezo yake fungua; amkamtanzania.com/kurasa
  3. kama unahitaji nikusimamie kwa karibu na uweze kukamilisha kitabu chako ndani ya miezi miwili, karibu niwe kocha wako, kujua zaidi kuhusu mimi kuwa kocha wako fungua; kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Rafiki yangu, ni imani yangu kwamba kama ulikuwa unafikiria kuandika kitabu ila unakwama, hujui uanzie wapi, basi sasa una pa kuanzia na anza sasa.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.