Muda tulionao kwenye siku yetu ni masaa 24 pekee, haujawahi kuongezeka na hakuna dalili kwamba muda huu utaongezeka siku za hivi karibuni.
Lakini mambo ya kufanya yanazidi kuwa mengi, tunazidi kuwa na majukumu mengi katika muda mfupi tulionao.
Kama hiyo haitoshi, kiasi cha taarifa na maarifa tunayoyapata kwenye siku yetu ni kikubwa mno. Tunakutana na taarifa nyingi kuliko tunavyoweza kuzifanyia kazi. Tunapata maarifa mengi kiasi cha kushindwa kuyatumia yote.

Kuwa na orodha ya vitu vya kufanya kwenye siku yako na kuifuata orodha hiyo imekuwa mapinduzi makubwa kwa wengi. Kwa kufuata orodha, wengi wameweza kukamilisha mambo muhimu licha ya kusongwa na mambo mengi ya kufanya.
Lakini watu hawana orodha kwenye upande wa mambo ya kufikiria, upande wa mambo ya kuhofia na kuwa na wasiwasi nayo. Hivyo wengi wanaruhusu akili zao zichoke kwa kufikiria mambo ambayo hayana maana yoyote kwao.
SOMA; UKURASA WA 965; Kufanya Vitu Kwa Usahihi Na Kufanya Vitu Sahihi…
Hivyo ni muhimu sasa tuwe na orodha ya mambo ya kufikiria. Tuchague ni mambo ya aina gani tutaruhusu akili zetu zijiingize kwenye kuyafikiria. Hapa unaifanya akili iache kusumbuka na kila aina ya taarifa na maarifa, na badala yake ichague maeneo muhimu ambapo unaweza kuyafikiri na kuchukua hatua.
Kwa kuwa na orodha hii, kunasaidia sana akili yako kuweza kufanya kazi vizuri kwa maeneo machache na muhimu badala ya kusumbuka na maeneo mengi na yasiyo muhimu.
Chagua maeneo ambayo ni muhimu zaidi kwako, kisha chagua vitu ambavyo vinastahili muda wako kufikiria na kufuatilia. Kisha toa vipaumbele kwenye mambo hayo muhimu. Ipe akili yako nafasi ya kufikiri mambo machache kwa kina, badala ya kufikiri mambo mengi kwa juu juu.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog