Kitu kimoja ambacho huwa napenda kuwakumbusha wafanyabiashara mara kwa mara ni kwamba wateja wananunua kwa sababu zao binafsi na siyo kwa sababu zako.
Mteja hanunui kwa sababu wewe unauza, ila ananunua kwa sababu anahitaji kununua. Na kama ambavyo tunajua, sisi binadamu ni wabinafsi, tunajali mambo yetu zaidi kuliko kitu kingine chochote.
Sasa kutegemea tu wateja wajisikie kununua kwako unaweza usiwe mpango mzuri sana. Unahitaji kuwapa wateja sababu zaidi ya kununua kwako, siyo tu ule uhitaji wao, bali uwape kitu kama deni hivi, ambacho kitawafanya wajisikie kulipa deni hilo.

Na hapa ndipo urafiki na mapenzi vinapoingia kwenye biashara.
Watu watakaokusaidia kwenye biashara na hata maisha kwa ujumla ni wale watu ambao umechukua muda kutengeneza nao urafiki. Wale ambao umechukua hatua ya kutengeneza mahusiano bora na wao.
Unakuwa umetengeneza thamani kubwa na watu hao kupitia mahusiano hayo kiasi kwamba mtu anaona ni wajibu wake kufanya kitu kwa ajili yako. Unakuwa umewapa thamani kubwa kiasi kwamba unapouliza chochote wanakuwa tayari kusema ndiyo, kwa sababu wanajua namna ambavyo wamenufaika na wewe.
Ili uweze kujenga mahusiano haya na wateja wako, ili uweze kuwapa thamani kubwa sana itakayowasukuma kukupa wewe kile unachotaka, unahitaji kupenda sana kile unachofanya. Na zaidi unahitaji kuwapenda wale unaowahudumia.
SOMA; BIASHARA LEO; Kabla Watu Hawajanunua Wanataka Hichi, Na Baada Ya Kununua Wanataka Hichi.
Kama utakuwa unafanya tu kitu kwa sababu huna kingine cha kufanya, au kwa sababu unataka tu kupata fedha, zoezi hilo la kutengeneza mahusiano litakuwa gumu sana. Kama utawaona wateja wako kama watu ambao wanataka tu kunufaika, watu wasio na shukrani, itakuwa vigumu kwako kutoa thamani kubwa kwao.
Hii ni kazi ngumu ndiyo maana wengi hawawezi kuifanya, lakini wachache wanaoifanya, inawanufaisha sana.
Urafiki na mapenzi ndiyo jina la mchezo, kama unataka kupiga hatua kwenye biashara, basi chukua muda kutengeneza mahusiano bora na wateja wako, mahusiano yatakayowafanya waone ni wajibu kwao kununua kutoka kwako. Huhitaji kupoteza fedha kwenye hilo, bali unachohitaji ni kujali na kwenda hatua ya ziada kwenye huduma unazotoa na matatizo unayotatua.
Kama biashara unayofanya hupo tayari kuweka kazi ya aina hii, kutoa thamani kubwa na kutengeneza mahusiano bora na wateja wako, upo kwenye njia ya kushindwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog