Rafiki mzuri ni yule ambaye anakuambia ukweli kama ulivyo, yule ambaye hafanyi kitu ili kukufurahisha au kukuridhisha, bali anafanya kile sahihi kufanya.

Kadhalika mwalimu mzuri ni yule ambaye anafundisha kile ambacho ni kweli hata kama kinaumiza au hakifurahishi. Anafundisha kama kilivyo na mwanafunzi anachagua kuchukua hatua kulingana na alichojifunza.

Sifa hizi mbili, yaani rafiki na mwalimu mzuri, tunazipata ndani ya maisha.

Dunia Inajiendesha

Maisha ni rafiki na mwalimu mzuri sana, japo wengi wamekuwa hawaoni hili.

Wengi wamekuwa wanaona maisha ni mateso, maisha ni magumu na maisha ni kitu cha kupita tukielekea kwenye raha zaidi.

Lakini ukweli ni kwamba, kile tunachoona ni mateso na ugumu wa maisha, ndiyo urafiki na ualimu wa maisha yenyewe.

Unapokutana na ugumu kwenye maisha, jua kuna kitu maisha yanataka kukufundisha. Huenda maisha yanakufundisha thamani ya vitu, kwamba hakuna kinachopatikana kiurahisi hivyo lazima ujitoe ili kupata unachotaka.

Wakati mwingine maisha yanakupa maumivu, unapanga unachotaka na unaweka kila juhudi kuhakikisha unakipata, unafanya kila lililopo ndani ya uwezo wako, lakini matokeo yanakuja tofauti kabisa. Hapa maisha yanakuonesha urafiki, yanakutaka ujue kwamba siyo mara zote unapata unachotaka, hata kama umefanya unachopaswa kufanya. Hapa rafiki maisha anakukumbusha umuhimu wa kuwa na subira, kuwa mtulivu na kuwa mvumilivu ili kupata kile unachotaka.

SOMA; #TAFAKARI YA LEO; MAANA YA MAISHA KWA MWEREVU NA MPUMBAVU….

Yachukulie maisha kama mwalimu mzuri na rafiki mzuri, na kila unapokwama, jiulize ni kipi unakumbushwa na rafiki yako, au somo gani unalopewa na mwalimu wako. Hapo utajionea mwenyewe hatua muhimu unazoweza kuchukua na maisha yako yakawa bora kabisa.

Lakini kama kila unalopitia utaona kama maisha ni magumu na hayafai, utaishia kuyaona maisha ni adui yako na hayafai. Yataendelea kuwa magumu na utaishia kulalamika kila wakati.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog