Habari rafiki?

Hongera sana kwa zawadi nzuri sana ya siku hii ya leo. Leo ni siku bora sana kwako hivyo kumbuka kuiendea siku hii ya leo kwa misingi ya maisha ya mafanikio ya Amka Mtanzania ambayo ni nidhamu, uadilifu na kujituma.

Wote ambao tunasoma hapa miaka 100 ijayo hatutokuwepo duniani. Tutaondoka na kuwaachia wengine nafasi ya kuendelea kuishi hata wale watu wa kale,wanafalsafa walioshi miaka ya nyuma zaidi ya miaka elfu mbili iliyopita leo hii tunakumbuka kwa zawadi yao walioacha hapa duniani ambayo ni misingi ya maisha ambayo wao waliishi kipindi hicho ambayo na wewe ukifanikiwa kuitumia katika maisha yako hakika hutobaki kama ulivyo kwani ni falsafa nzuri sana walizokuwa wanaishi wakati huo ambazo kwa sasa bado zina nafasi kubwa sana.

02638-malezi

Rafiki, kadiri dunia inavyokua na watu ndivyo wanazidi kupunguza ustarabu kwa sababu kuelimika siyo kustarabika. Wazazi au walezi nao wamejisahau sana katika malezi ya watoto hivyo watoto ndiyo wanaopata sana shida katika zama hizi za taarifa. Wako watoto wadogo wanakosa malezi mazuri hivyo wanaishia kujiongoza wao wenyewe bila kuwa na msingi wowote wa maisha. Wazazi wanaona wakishazaa jukumu la kulea na kuhakikisha mtoto anakuwa salama na afya bora ni la wasaidizi wa kazi yeye kazi yake ni kutoa fedha tu lakini mambo mengine hataki kujua nini kinaendelea kwa mtoto.

Hivyo kama wazazi mnatakiwa kuamka usingizini kwa sababu wazazi ndiyo wanaweza kuamka kutengeneza dunia wanayotaka kupitia familia yao. Kama umeshindwa kutengeneza dunia yako unayotaka kuishi ni rahisi kuchukuliwa kama upepo ndiyo maana watoto ambao wamekosa msingi huwa wanachukuliwa na uelekeo wowote kwa sababu ukikosa mwelekeo basi mwelekeo wowote utakuchukua.

SOMA; Jinsi Ya Kumfundisha Mtoto Kuvua Samaki.

Mpendwa msomaji, ni namna gani tunaweza sasa kuwafundisha watoto jinsi ya kuwa wakifikiriaji bora na mwenye akili?

Kwanza dunia ya leo watu hawataki kabisa kufikiri ndiyo maana mtu akiwa na kitu kidogo tu anaona bora aingie gugo kuuliza hata kama kitu chenyewe siyo cha kuuliza. Tusipojenga kizazi cha watu wanaofikiria tutakuwa na taifa la ajabu sana hapa baadae.

Kwanza kabisa, wajengee watoto utamaduni wa kusoma vitabu tokea wakiwa wadogo.

Hapa ni pagumu kama mzazi mwenyewe tokea amalize shule hajawahi kusoma kitabu ndiyo aje amwambie mtoto inakuwa ni ngumu lakini inawezekana kama kuna nia. Kama wengine wanaweza kwanini wewe usiweze? Kama anayeweza ana milango mitano ya fahamu kwanini wewe usiweze? Labda kama huna milango mitano ya fahamu lakini kama unayo nia ya kumfunisha mtoto utamaduni wa kusoma lazima utafanikiwa.

Hatuwezi kuwa na watoto ambao wana akili na kuwa wafikiriaji bora kama tunawahamasisha zaidi kuangalia TV na kusikiliza redio kuliko kusoma vitabu. Watoto wengi wanakosa maarifa chanya kwa sababu hata jamii inayowazunguka imejaa mitazamo hasi hivyo wewe kama unataka mtoto wako awe bora na wa mfano mjengee utamaduni huu na acha kumjengea utamaduni wa kuangalia vitu hasi ambavyo havina msaada kwake.

Itakuwa ni litania au orodha ndefu sana nikianza kuandika hapa faida za kusoma vitabu lakini njia rahisi ya kutaka kujua faida za kusoma vitabu ni kuanza kusoma vitabu. Panda mbegu bora leo kwa mtoto wako na hutokuja kujutia.

SOMA; Changamoto Moja Ya Kuepuka Kumshirikisha Mtoto Wako

Rafiki, njia nyingine ni kumfundisha mtoto kuwa mtu wa kufikiria kwanza yeye mwenyewe.

Kwa mfano, mtoto akikuuliza swali usimjibu kwanza muulize wewe unaonaje au unafikiri jibu lake ni nini. Mpime kwanza kadiri ya uwezo wake, watoto muda mwingine wana majibu hivyo Wanataka wapewe nafasi ya kuelezea hivyo kwa njia hii utaweza kumjengea mtoto uwezo mkubwa sana.

Kama akishindwa kujibu swali basi au hata akiweza wewe unaweza sasa ukaongezea na kutoa ufafanuzi zaidi au hata mifano ili kumjenga zaidi. Mwache mtoto atumie elimu na utambuzi aliokuwa nao kupima uwezo wake kupitia maswali mbalimbali. jenga tabia ya kumuuliza mtoto maswali kadiri ya darasa lake la elimu ili kumpima uelewa.

Hatua ya kuchukua leo, kama kwako huna vitabu kwa sasa hujanunua usisubiri mpaka ununue bali chukua vitabu vya dini ambavyo hivi natumaini viko kila nyumba na mpe kadiri ya imani yako ya dini angalau awe anasoma na halafu akupe mrejesho je amejifunza nini kupitia kitabu hiko. Ili mtoto aweze kujenga utamaduni wa kusoma vitabu mzazi naye anatakiwa kuwa kiongozi wa kuonesha mfano bora na nidhamu ya kusoma vitabu lakini kama wewe unamjenga mtoto na wewe huna nidhamu hivyo usitegemee mabadiliko makubwa.

Kwahiyo, ili tuweze kuwa na familia bora lazima tuwe na jamii bora. Na jamii bora inajengwa na wanafamilia imara waliokuwa na misingi mizuri. Mzazi ndiyo jicho la mtoto hivyo usimwache mtoto aone vitu ambavyo viko nje ya umri wake.

Nakutakia kila la heri rafiki yangu, ukawe na siku bora sana ya leo.

Rafiki na mwalimu wako,

Deogratius Kessy

Mawasiliano; 0717101505//0767101504, deokessy.dk@gmail.com // kessydeo@mtaalamu.net  au unaweza kutembelea tovuti yangu  hapa www.mtaalamu.net/kessydeo kujifunza zaidi kila siku.