Mpendwa rafiki yangu,

Sheria zimewekwa kwa ajili ya kulinda haki za kila mmoja wetu, ziko sheria za kibinadamu na hata za wanyama pia.

Changamoto ya wazazi wengi katika karne hii ni malezi ya watoto. Watoto wanakosa malezi bora pamoja  na misingi sahihi ya kuishi. Wako wazazi ambao wanawanyima watoto baadhi ya haki na hii inawapelekea watoto kutojisikia vizuri.

Na wazazi wengi wanaishi kimazoea,hawapendi kujifunza mbinu mpya wala mambo mapya watu wanataka kuendelea kuwalea watoto kama vile wao walivyozoea kulelewa.  Hatutakiwi kukariri maisha hata siku moja , mambo yanabadilika hivyo na wewe kama mzazi unatakiwa kubadilika siyo kuishi kimazoea.

Haki ambayo watoto wengi siku hizi wananyima ni haki ya kucheza. Tunaweza kuona kucheza kwa watoto ni kama kupoteza muda ila ni haki yao. Kama wewe ulicheza ukiwa mdogo naye ana haki ya kucheza. Mtoto anapocheza na watoto wenzake anakuwa anajifunza pia vitu vingi.

Kitu cha kuzingatia katika michezo, anagalia watoto anacheza nao tabia yao ikoje, kama wanatabia nzuri waruhusu watoto wacheze na wachangamane na watoto ambao ni sahihi kwao. Kuwakataza watoto wasicheze ni kuwanyima haki yao ya kimsingi.

Tumekuwa tunawanunulia watoto michezo mingi ya kisasa badala ya kuwaacha watoto wacheze na michezo ya asili. Michezo ya asili ambayo hata wewe ulicheza ukiwa mdogo inawafanya watoto nwengi kwa wabunifu na kuwawezesha kuishi maisha kadiri ya asili.

Ujio wa teknolojia ni mzuri lakini kama tunavyojua kila kitu kizuri kinakuja na faida na hasara zake.  Wazazi wanaelekeza nguvu kubwa kwa watoto kucheza michezo ya kisasa badala ya asili. Kwanza michezo ya kisasa  ina gharama lakini ya asili haina gharama ni mtoto tu kuwa mbunifu wa kubuni michezo. Michezo ya kisasa inawafanya watoto kuwa tegemezi , wanashindwa kuwa wabunifu wa kutengeneza vitu mbalimbali kadiri ya asili.

Uwape watoto wako muda wa kucheza, ndiyo maana hata kigezo mojawapo cha kuwa na shule ni uwanja wa michezo wa watoto. Lazima watoto wacheze ili waweze kugundua vipaji vyao, tuwakaririshe tu watoto maisha mazuri yanapatikana kwa kupata alama nzuri darasani na kufaulu. Hata kupitia hivyo vipaji vyao watakavyoviibua ndani yao vinaweza kuwafanya kuwa na mafanikio makubwa. Kwa mfano, kila mmoja wetu ni shahidi wa hili ukiangalia wachezaji wa mpira wa miguu kama kina Mbwana Samata wanalipa fedha nzuri kupitia michezo lakini kama angelelewa maisha ya kuangalia tut v na kukomaa darasani asingekuwa hapo alipo leo.

SOMA; Jinsi Ya Kumfundisha Mtoto Kuwa Mfikiriaji Bora Na Mwenye Uwezo Mkubwa AkiliJinsi Ya Kumfundisha Mtoto Kuwa Mfikiriaji Bora Na Mwenye Uwezo Mkubwa Akili

Hatua ya kuchukua leo; wape watoto muda wa kucheza. Wafanye kazi, wasome lakini usisahau kuwapa muda wa kucheza na wenzao na waache wacheze michezo ya asili ndiyo itaweza kuibua vipaji na kuwafanya kuwa wabunifu.

Hivyo  basi, kila mzazi awe mtetezi wa haki za mtoto. Wafundishe watoto michezo ya asili na siyo kuwaachia michezo ya kisasa inayowafanya watoto kushindwa kuendana na mazingira ya asili. Asili huwa haina madhara siku zote.

Makala hii imeandikwa na

Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa www.mtaalamu.net/kessydeo, vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI.  Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Mwl, Deogratius kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com // kessydeo@mtaalamu.net

Asante sana