Kama kuna mahali unataka kuwahi, na kuna njia ambayo ni ndefu na nyingine ya mkato, kama umewahi kupita njia hiyo ya mkato siku za nyuma, basi unaweza kuipita na ukawahi kufika. Kama hujawahi kupita njia hiyo, huwa unasikia tu ipo njia ya mkato, usiipite siku ambayo unataka kuwahi, kwa sababu utachelewa.
Hivi ndivyo ilivyo kwenye safari ya mafanikio, njia ya mkato, huwa ndiyo njia ndefu kuliko ile njia ambayo inaonekana kuwa ndefu.
Kwenye mafanikio, njia ndefu, njia ambayo ndiyo inajulikana kuwafikisha watu kwenye mafanikio, ndiyo njia sahihi ya kutumia.
Lakini njia ya mkato, njia ambayo inaonesha kuna namna ya kupata mafanikio bila ya kuweka kazi kubwa, kwamba ipo namna unaweza kupata tu mafanikio kwa haraka na bila kazi, ni njia ambayo ni ndefu mno.

Ni njia ndefu kwa sababu kuu mbili;
Moja, hutapata kile unachotaka kwa njia hiyo, na hivyo itakubidi uanze tena kwa ile njia ambayo ni sahihi. Hivyo muda wote uliotumia kukimbizana na njia hiyo ya mkato, unakuwa ni muda ambao umeupoteza, unakuwa ni muda ambao umeuondoa kwenye kutumia njia sahihi.
Mbili, chochote utakachopata kwa njia ya mkato, utakipoteza. Na hapa ndipo unapoteza muda zaidi na zaidi, kwa sababu chochote utakachopata kwa njia ya mkato, utakipoteza, au kitaondoka, utabaki kama ulivyoanza na utahitaji kuanza tena upya kwa njia sahihi. Kama ulitumia njia ambazo siyo za kisheria, kama wizi au rushwa na ufisadi, utafika wakati wa kurudisha kila ulichochukua.
SOMA; UKURASA WA 549; Adhabu Ya Dunia…
Na muhimu zaidi, kile ambacho kinakuwa kimepatikana kiurahisi, bila ya kuweka kazi kubwa, huwa pia kinatumika na kuisha kiurahisi kabisa.
Dunia haina huruma wala upendeleo, dunia inajiendesha kwa sheria zake, ambazo zinailinda dunia dhidi ya watu wenye tamaa nakutaka kupata bila ya kutoa. Hivyo kama utajidanganya kwa njia yoyote ya mkato, jua tu kwamba dunia inakusubiri ikuadhibu vya kutosha.
Acha kupoteza muda kwa njia za mkato, huwa hazifanyi kazi. Njia sahihi, njia zinazoonekana ni ndefu, ndizo unazopaswa kutumia.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog