First learn the meaning of what you say, and then speak. – Epictetus

Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?
Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo. Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Mwongozo wetu wa maisha ya mafanikio kwa mwaka huu 2018 ni TATUA, AMUA NA ONGOZA.

Asubuhi ya leo tutafakari IJUE MAANA KABLA YA KUONGEA…
Moja ya vitu unavyopaswa kuwa navyo makini sana kwenye maisha yako, ni maneno unayoongea.
Hii ni kwa sababu, ukishaongea umeongea, huwezi kufuta maneno uliyoongea, na huwezi kuyarudisha kwenye kinywa chako, yakitoka yametoka.

Pia changanoto nyingine kwenye kuongea ni kwamba, unaweza kuongea utakavyo, lakini watu wakaelewa wanavyotaka wao.
Unaweza kuongea kwa nia njema kabisa, ila watu wakaelewa kwa tofauti, wakawa na maana ambayo siyo nzuri.

Hivyo kwa kujua haya kuhusu maneno tunayoongea, tunahitaji kuwa makini sana kabla ya kuongea.
Kwanza kabisa, ijue maana ya kile unachotaka kusema kabla hujakisema, na siyo tu maana kwa upande wako, bali maana kwa yule unayemwambia, kulingana na mtazamo wake na mazingira yake pia.

Hakuna mtu amewahi kugombana na mwingine kwa sababu hajaongea, wala hakuna mtu amewahi kufungwa kwa kukaa kimya. Lakini maneno watu wanayoongea, yameleta ugomvi na wengine na hata mahusiano kuvunjika.
Jua maana ya kile unachotaka kuongea, kabla hata hujakiongea, itakusaidia kupunguza changamoto zisizo na maana.

Uwe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha