Mazingira yanayotuzunguka, yana nguvu kubwa sana ya kutufanya vile tulivyo sisi. Japo wengi huwa hatulioni hili, na huwa tunafikiri kwamba tuna nguvu ya kuyashinda mazingira yetu. Ukweli ni kwamba hatuna nguvu hiyo.
Mazingira ninayozungumzia hapa ni kila kinachokuzunguka, kuanzia watu, vitu na hata hali mbalimbali zinazokuzunguka.
Kwa mfano kama unazungukwa na watu ambao hawayapendi maisha yao, wana kila cha kulalamikia kuhusu maisha, haitakuchukua muda na wewe utaanza kuyachukia maisha yako na kulalamikia kila kitu. Kama umezungukwa na watu ambao hawapendi kazi zao na wanazifanya kwa kawaida ili tu wasifukuzwe, huwezi kwenda tofauti na wao, hata kama mwanzoni ulijiambia utakuwa tofauti, baada ya muda watakumeza.
Kama upo kwenye eneo ambalo lipo hovyo, mfano chumba ambacho ni kichafu au vitu havijapangwa vizuri, akili na mawazo yako nayo yatakuwa hovyo, hayatatulia. Kadhalika ukisikiliza habari ambazo ni hasi na za kujenga hofu, haitakuchukua muda na wewe utakuwa mtu hasi na mwenye hofu nyingi.

Hii inaenda hata kwa vipindi na sinema unazoangalia, zinayatengeneza maisha yako kupitia kile unachoona. Sasa kama unaangalia mambo yanayokatisha tamaa, maisha yako yatakuwa ya kukatosha tamaa.
Nenda eneo ambalo watu wanalisemea vibaya, hata kama halina shida yoyote, ukishayasikia yale maneno ya watu na wewe utaanza kuona ubaya wa eneo hilo.
SOMA; UKURASA WA 822; Badili Hadithi Unayoishi…
Hivyo ndivyo mazingira yalivyo na nguvu kwenye maisha yetu, mazingira yanatubadilisha sana. Naweza kusema hatuna tofauti na vinyonga, sema tu sisi inatuchukua muda kidogo, kinyonga anabadilika mara moja.
Kwa kujua hili rafiki, vita yako ya kwanza inapaswa kuwa kwenye mazingira unayokubali yakuzunguke. Ukishaona mazingira uliyopo hayaendani na kile ambacho unataka kwenye maisha yako, usijidanganye kwamba utaweza kuyashinda. Angalia kama ni kitu unaweza kubadili na ufanye hivyo, na kama huwezi kubadili, basi kimbia haraka kabla sumu haijakuingia.
Chambua kila unachoruhusu kiingie kwenye akili yako, je kina manufaa gani na kama kinachangia wewe kufika kule unakotaka kufika. Kama kinakwenda kinyume usijifanye una huruma, huruma hiyo itakupoteza haraka sana. Baada ya muda, maisha yako yanafanana na mazingira yako, hivyo hakikisha unayachagua mazingira hayo vizuri.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog
Ukweli mtupu kocha, lazima nijiangalie kwa upya mazingira yangu kwa jicho la tofauti.
LikeLike
Vizuri sana.
LikeLike