Kuna utani kwamba mtu mmoja ambaye alikuwa hajawahi kuvaa miwani nyeusi, aliivaa siku moja, ukiwa ni mchana wa jua kali. Lakini kutokana na weusi wa miwani ile, mtu yule aliona kama ni usiku, yaani giza linaingia. Na alitaka kujisaidia haja ndogo hivyo akasogea pembeni ya njia, akijua ni giza na hakuna anayemuona, akaanza kufanya yake, kumbe ni chana wa jua kali na watu wanamwona na kumshangaa.
Ni vigumu sana kuuona ukweli kwa sababu kila mtu kuna miwani ambayo ameivaa, miwani hiyo inamfanya aone kile anachotaka kuona na siyo kuona ukweli.
Miwani hii ya rangi ambayo kila mmoja wetu amevaa inatokana na mtazamo ambao tunao na mawazo ambayo yanatawala akili zetu. Hivi ndiyo vinaamua tutaona nini.

Kitu kinaweza kuwa wazi kabisa, lakini sisi tukachagua kuona kile ambacho tunataka kuona. Na ndiyo maana kwenye jambo moja, watu tofauti wanakuwa na maoni tofauti na hata misimamo tofauti. Hii ni kwa sababu kila mtu anaona kile anachotaka kuona, na siyo kuona kitu kama ambavyo kipo.
SOMA; UKURASA WA 999; Unapoukaribia Ukweli, Hofu Inaongezeka…
Kama kweli tunataka kuona kitu kama kilivyo, kwanza lazima tuweke msimamo wetu pembeni, tuachane na mawazo yote tuliyonayo juu ya kitu hicho na pia tuache hukumu yoyote ambayo tumeshaijenga juu ya kitu hicho.
Tujilazimishe kukiona kitu kama ndiyo tunakijua kwa mara ya kwanza, kama hatujawahi kukiona tena, kama hatujawahi hata kukifikiria. Ni zoezi gumu sana hili lakini linasaidia, angalau kuacha kujidanganya kwa mitazamo na mawazo yetu.
Ni vigumu kuuona ukweli pale unapokuwa na mitazamo yako juu ya kitu fulani, kwa sababu huwa hatupendi kwenda kinyume na tunavyoamini. Hivyo ukianza kuangusha mitazamo hiyo, utaanza kuuona ukweli kama ulivyo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog