Mara kwa mara watu hukumbwa na msongo wa mawazo kwenye maisha yao. Na msongo huu hutokana na mambo mbalimbali ambayo watu wamekuwa wanapitia. Lakini kubwa kabisa ni pale mtu anapokuwa anapanga kufanya mambo, ila hayafanyi. Anabaki na mipango ambayo kila akiifikiria anapata msongo wa mawazo.

Wakati mwingine mtu anakuwa amewaahidi watu mambo mengi kuliko uwezo wake wa kutekeleza. Hili pia linaleta msongo. Na pia kwa wale ambao wanakubali vitu vingi kuliko uwezo wao wa kufanya au kutekeleza, wanajikuta kwenye msongo wa mawazo.

IMG-20170303-WA0002

Kutokana na sababu hizi za msongo wa mawazo, ambazo tunasababisha wenyewe, kuna mambo mawili tunaweza kuyafanya ili kuondokana na msongo wa mawazo.

Jambo la kwanza ni kufanya kile ambacho tumepanga au kuahidi kufanya. Unachukua hatua ya kufanya, hapa unaleta suluhisho kwenye kitu hicho. Kwa kufanya, unaondokana na ile hali ya kufikiria utafanyaje na utafanya saa ngapi, kwa kuwa unafanya.

Jambo la pili ni kuamua kutokufanya kile ulichopanga kufanya. Yaani hapa unaamua kabisa ya kwamba hutakifanya tena, na hivyo unajiondolea mzigo wa kusema utakuja kufanya na kufikiria utafanyaje na utafanya lini. Maamuzi ya kutokufanya yanakuondoa kwenye mrundikano wa vitu vingi ambavyo huwezi kufanya.

SOMA; UKURASA WA 982; Ni Muda Ambao Ungeutumia Kufanya Mengine Muhimu…

Sasa, maamuzi ya kufanya ni rahisi, kwa sababu ulishapanga kufanya. Ni maamuzi ya kutokufanya ndiyo magumu kufikia, kwa sababu utaanza kufikiria itakuwaje ukiamua kutokufanya? Na jibu ni kwamba itakuwa kama ilivyo sasa, ila tu hutakuwa na msongo. Kwa sababu tofauti ya sasa wakati umesema utafanya na hufanyi na pale utakapoamua kwamba hufanyi ni msongo wa mawazo. Ukishaamua hufanyi, basi msongo nao unaondoka.

Pitia mambo yote ambayo umekuwa unasema utafanya ila yana muda sana hujayafanya. Yaorodheshe yote, kisha chagua yale utakayoanza kufanya na yafanye mara moja, na chagua ambayo hutayafanya na jiambie kwamba hutayafanya. Hili litakupunguzia msongo wa mawazo kwa mambo ambayo hata hutayafanya.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog