Hongera sana rafiki yangu kwa juma hili la 9 la mwaka 2018 ambalo tunalimaliza. Ninachoamini ni kwamba, juma hili limekuwa la kipekee kwako, umejifunza mengi, kujaribu mengi na hata kupiga hatua. Na hata kwa yale unayojiambia umeshindwa, hujashindwa, bali umejifunza.

Nikukaribishe sasa kwenye kipengele chetu cha TANO ZA JUMA ambapo nakushirikisha mambo matano muhimu niliyojifunza na kukutana nayo kwa juma zima, ambayo na wewe rafiki yanaweza kukusaidia sana.

Karibu kwenye TAZO ZA JUMA, ujifunze na uchukue hatua ili maisha yako yawe bora zaidi.

#NENO; TUWASHUKURU WATU WALIOKUFA.

Kama upo hai, basi usijaribu kusema kwamba huna cha kushukuru, hata kama maisha yako ni magumu kiasi gani. Kila mtu aliye hai, hata kama ameumia kiasi gani, hata kama hana fedha na ana madeni, hata kama umenyanyaswa kiasi gani, basi una cha kushukuru.

Na kitu kimoja ambacho kila mmoja wetu anapaswa kushukuru, ni watu waliokufa. Watu waliotutangulia kufa, kwa hali mbalimbali, wamekuwa sababu ya sisi kuendelea kuwa hai. Kama umewahi kuumwa, ukatumia dawa na kupona, ile dawa haikutokea tu yenyewe, bali kuna watu walionekana kuwa wanakufa, uchunguzi ukafanywa kisha ikagundulika dawa hiyo inatibu ugonjwa huo. Hii ina maana kwamba kama wasingekuwa wamekufa watu huko nyuma, na hilo likasababisha watu kugundua dawa hiyo, basi wewe ungekufa, ina maana umetibiwa na kuwa hai, kwa sababu kuna watu huko nyuma walikufa na kuchochea matibabu yatafutwe.

Sijui kama unalielewa hili vizuri au linakuwa zito kueleweka.

Labda tuchukue mfano mwingine, kama umewahi kupanda kwenye gari na kuambiwa ufunge mkanda wa usalama, shukuru sana watu waliokufa. Hii ni kwa sababu hiyo mikanda ya usalama haikutokea tu hewani, bali watu waliona kwamba magari yakipata ajali, watu wanaumia na kufa, lakini kama wakiwa wamefunga mikanda, basi vifo na kuumia kunapungua.

Angalia kila kitu kwenye maisha yako, na utagundua kwamba watu waliokufa wamekufa kwa ajili yako, kufa kwao kumesababisha leo kuwe na viwango. Mfano angalia kipindi ambacho labda kuna ajali nyingi za magari, utaona sheria nyingi zinapitishwa ili kupunguza ajali hizo. Na kweli baada ya sheria hizo, unaona ajali zinapungua. Hii ina maana kwamba, kama sheria hizo zisingepitishwa, basi huenda ajali zingekuwa nyingi na huenda ungekuwa kwenye baadhi ya ajali hizo. Na kama watu wasingekufa kwa ajali, sheria zisingewekwa.

Tushukuru kwa kila tunachopitia kwenye maisha, lakini pia, tusisahau kuwashukuru wale waliotutangulia kufa, maana wao wamechangia sisi kuwa hai mpaka leo.

#1 KITABU NILICHOSOMA; PREDICTABLY IRRATIONAL.

Binadamu tunajisifu kwamba ndiyo viumbe ambao tuna uwezo mkubwa wa kufikiri kuliko viumbe wengine wote hapa duniani. Hii ni kwa sababu ukiangalia viumbe wengine wote, ni sisi binadamu pekee ambao tuna ufahamu mkubwa, tuna utashi na kuweza kufikiri kwa kina na kufikia maamuzi fulani. Lakini tafiti za wanasaikolojia na wachumi zinaonesha kwamba, tunaweza kufikiri na kufanya maamuzi wakati ambao ni wa kawaida, wakati ambao hatuna hatari au hisia zetu zipo juu.

Lakini tunapokuwa kwenye hatari, au tunapokuwa na hisia ambazo zipo juu, huwa tunafanya maamuzi lakini hatufikiri kabisa. Yaani tunajikuta tunafanya mambo ambayo kwa hali ya kawaida, tusingeweza kuyafanya. Na hili limewagharimu wengi.

Sasa mambo yangekuwa poa kama ingekuwa ni wakati wa hatari na hisia pekee tunafanya maamuzi bila ya kufikiri. Mambo yanakuwa mabaya sana kwa upande wetu, pale watu wanapoweza kutabiri hali yetu ya kutokufikiri na kuitumia kwa manufaa yao.

Kwa mfano umeenda dukani kununua kitu, ukakutana na bango linasema nunua mbili upate moja BURE. Hukuwa na mpango wa kununua vitu viwili, au hata wa kununua kitu hicho, lakini akili yako inapoona neno BURE, inaacha kufikiri na unafanya maamuzi ambayo hata hujui kwa nini unafanya. Unachoshangaa unajikuta umerudi nyumbani na vitu ambavyo hukupanga kununua na wala hutatumia.

Kutabirika kwetu kwa kutokufikiri kumekuwa kikwazo kwenye maisha yetu na kumekuwa kunatumiwa na wengi kujinufaisha.

Kupitia kitabu cha PREDICTABLY IRRATIONAL mwandishi na mwanasaikolojia Dan Ariely anatuonesha jinsi kutabirika kwetu kwa kutokufikiri kunatugharibu.

Dan anatuonesha kwa nini huwa tunapima kila kitu kwa kutumia vitu vingine na hilo linavyotugharimu.  Anatuonesha pia kwa nini BURE ina gharama kubwa kwenye maisha yetu kuliko tunavyofikiri.

Dan ameenda mbali zaidi na kuonesha, kwa tafiti kwamba wakati mbaya kuliko wote kwenye maisha yako wa kufanya maamuzi, ni wakati ambapo mtu umesisimka kimapenzi. Pia ametuonesha kwa nini watu wanaweza kupona bila hata ya kutibiwa, kwa kupewa dawa ambayo siyo halisi, huku wakiambiwa ni dawa na wanapona kabisa.

Nilichopenda sana kuhusu kitabu hichi ni kwamba kila kitu ambacho mwandishi anatuonesha tunafanya, anafanya hivyo kwa tafiti. Na tafiti hizo zimepangwa vizuri sana kiasi kwamba zinaakisi uhalisia. Kwa mfano utafiti wa kujua namna kusisimka kimapenzi kunaathiri maamuzi yetu, vijana wa kiume walishiriki kwenye utafiti huu, ambao uliwaweka kwenye mazingira ya kuwasisimua kimapenzi, kuwafanya wajichue na wakati huo huo wanajibu maswali kwenye kompyuta.

Kupitia kitabu hichi, unajifunza namna tabia zetu binadamu zinabadilika kulingana na hali tunayopitia na mazingira pia. Pia kinatusaidia kujitoa kwenye mazingira yanayotupelekea kufanya maamuzi bila ya kufikiri na kuishia kupata hasara.

Uchambuzi wa kitabu hichi utakuwa kwenye AMKA MTANZANIA kwenye juma la kumi, na kitabu chenyewe kitapatikana kwenye KISIMA CHA MAARIFA. Hivyo pata muda usome uchambuzi wa kitabu hichi, na zaidi pata muda usome kitabu chenyewe.

#2 MAKALA YA WIKI; TAJIRIKA KWA KUANZA NA SHILINGI ELFU MOJA.

Wiki hii nakurudisha nyuma kidogo, miaka mitatu na miezi mitano imepita, ambapo niliandika makala yenye kichwa HIVI NDIVYO UNAVYOWEZA KUTAJIRIKA KWA KUANZA NA SHILINGI ELFU MOJA. Makala hii niliiandika kama suluhisho kwa wale wanaosema hawajaanza biashara kwa sababu hawana mtaji na hawakopesheki, nikaangalia na kuona wengi wanasema maneno hayo hayo kwa zaidi ya miaka mitano. Nikajiuliza je mtu wa kawaida kabisa, anayeweza kusoma ninachoandika atakosa shilingi elfu moja kwa siku? Nikaona elfu moja ni kiasi ambacho kila mtu anaweza kuweka pembeni kwa siku. Kama mtu atachagua kuishi maisha ya kawaida, akaachana na vitu visivyo vya lazima, kama kunywa pombe, kunywa soda au hata kunywa maji ya kununua, akaacha kununua nguo au vitu vingine kwa sababu amekutana navyo, basi elfu moja inapatikana, kila siku. Na kama kwa siku ni ngumu kukusanya, basi angalau kila mwezi shilingi elfu 30, au elfu 10 kila wiki. Lakini pia najua watu siyo wazuri kwenye kuweka akiba, hivyo kuweka elfu 30 kila mwezi, utashangaa mwaka unaisha na hujui fedha hiyo imeishia wapi, hivyo nikapendekeza njia ya kuweka fedha hiyo kwenye gereza ambalo huwezi kuitoa.

Sasa napenda kuwakumbusha wote kwamba, tangu nilipoandika makala ile, na kusisitiza mtu achukue hatua siku ile ile na siyo kusubiri, zimepita siku zaidi ya 1240, hii ina maana kama mtu alifuata ushauri ule, basi sasa angekuwa na zaidi ya shilingi shilingi milioni moja na laki mbili, na maisha yake yangekuwa vile vile, yaani asingekuwa amejitesa kwa lolote. Na zaidi sasa, kama mtu angetumia njia niliyopendekeza, angekuwa na zaidi haya ya milioni moja na laki tano. Ni kiasi kidogo, lakini kwa wale wanaolalamika hawana pa kuanzia, ni kikubwa sana.

Sasa kama ulisoma makala ile na hukuchukua hatua, isome tena na anza kuchukua hatua sasa. Na kama hukuisoma isome sasa na uchukue hatua mara moja. Nitaendelea kukukumbusha hili kila mara, ikifika miaka mitano, miaka 10 na kuendelea. Unaweza kusoma makala ile kwa hapa; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutajirika Kwa Kuanza Na Shilingi Elfu Moja. (https://amkamtanzania.com/2014/10/10/hivi-ndivyo-unavyoweza-kutajirika-kwa-kuanza-na-shilingi-elfu-moja/ )

#3 NILICHOJIFUNZA WIKI HII; UNA MIZIGO MINGI UNAYOHITAJI KUITUA.

Kwenye vitabu nilivyokuwa nasoma wiki hii nilikutana na hadithi moja ambayo imebeba somo kubwa sana. Hadithi inasema kwamba kulikuwa na viongozi wa kiroho wa kikundi fulani ambao walikuwa wanavuka mto wenye maji mengi. Viongozi hao, mmoja alikuwa mzoefu na mwingine ndiyo alikuwa anajifunza. Walipofika kwenye eneo la kuvuka mto, walikuta kuna binti anaogopa kuvuka. Sasa utaratibu wa kikundi chao, viongozi hao wa kiroho hawaruhusiwi kuwashika watu wa jinsia tofauti, hata iweje, na hawa walikuwa wanaume. Yule ambaye ni mgeni, akawa anaangalia kwenye ile hali mzoefu ambaye ni mwalimu kwake atachukua hatua gani. Basi yule mzoefu hakusema neno, alimshika yule binti na kumbeba mpaka upande wa pili, kisha kumshusha chini na wakaendeleana na safari yao.

Walitembea kwa muda mrefu bila ya mazungumzo, huku yule ambaye siyo mzoefu akitafakari tukio lile. Mwishowe uzalendo ukamshinda na akaamua aulize. Akamwuliza inakuwaje umeenda kinyume na utaratibu wetu, kwa nini umembeba yule binti wakati haturuhusiwi? Yule kiongozi mzoefu alimwangalia na kumuuliza, mimi nimembeba binti na kumshusha kwenye ng’ambo ya pili ya mto, kwa nini wewe umembeba mpaka sasa?

Ukiangalia yapo mambo mengi sana umeyabeba kwenye maisha yako, ambayo yanafanya maisha yako yawe magumu, yanafanya uwe na msongo wa mawazo, uwe na hasira na hata chuki kwa wengine. Labda ni namna ambavyo mtu alikufanyia vibaya siku za nyuma, au ni namna mtu amekujibu siki iliyopita. Inawezekana pia ni namna mtu alivyokuchukulia. Wakati mwingine au uliobeba mambo yao, wameshasahau kabisa hata kuna kitu wamefanya kwako. Wao wanaendelea na maisha yao, wewe unakazana kubeba mizigo yao.

Leo tua mizigo yote uliyobeba kwa wengine, chochote ambacho unajikumbusha kila mara kwamba mtu alikufanyia, achana nacho na songa mbele na maisha yako.

095a5b996f7db11bfe3b1d93a17b444b.0

#4 HUDUMA NINAZOTOA; KISIMA CHA MAARIFA.

Kama umekuwa unafuatilia kazi zangu, na bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, basi yapo mengi na mazuri unayakosa. Na kama umekuwa unafuatilia mafunzo ninayoyatoa, na unahitaji kujifunza zaidi basi sehemu pekee ya kufanya hivyo ni kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA. Pia kama umekuwa unajifunza sana na maisha yako yamebadilika na kuwa bora, na unasema sijui hata nikulipeje, basi jiunge na KISIMA CHA MAARIFA, siyo tu malipo yako yatakuwa na maana, bali zile hatua unazochukua zitakuwa na maana kwako na kwa wengine pia.

Kama bado haupo kwenye KISIMA CHA MAARIFA, nitumie ujumbe kwenye wasap 0717396253 wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA na nitakupa maelekezo ya kujiunga.

#TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; UNAJIPENDA LAKINI HUTHAMINI MAONI YAKO.

“It never ceases to amaze me: we all love ourselves more than other people, but care more about their opinion than our own.” – Marcus Aurelius

Marcus Aurelius, aliyekuwa mtawala wa Roma na mwanafalsafa wa Ustoa anashangaa iweje tunajipenda sisi wenyewe, lakini tunajali maoni ya wengine kuliko maoni yetu?

Iweje ujipende, kwa kuhakikisha maisha yako yanakuwa salama, kila siku, lakini siku moja unasema unataka kupiga hatua kubwa, wale wanaokuzunguka wanakuambia huwezi, halafu unakubaliana nao kwamba huwezi?

Hivi hata wewe halikushangazi hilo?

Fikiri kwa kina wakati wowote unapoanza kuyapa uzito maoni ya wengine kuhusu wewe kuliko maoni yako juu yako mwenyewe, na utaona kwamba unajinyima mengi kwa sababu ya maoni ya wasiojua hata unaweza nini na unaenda wapi.

Nikutakie kila la kheri kwenye maandalizi ya juma namba 10 la mwaka huu 2018, likawe juma bora kabisa kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog