While we are postponing, life speeds by. – Lucius Annaeus Seneca

Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
TATUA, AMUA NA ONGOZA ndiyo mwongozo wetu wa mafanikio kwa mwaka huu 2018 ambao utatuwezesha kupiga hatua kubwa.

Asubuhi ya leo tutafakari WAKATI UNAAHIRISHA, MAISHA YANAKUPITA..
Linapokuja swala la muda wa kufanya yale ambayo tumepanga kufanya, huwa tunajidanganya sana kitu kimoja.
Huwa tunajiambia tutafanya kesho, au tutakapokuwa tayari, tukifikiri kwamba maisha yatatusubiri mpaka pale tutakapokuwa tayari kufanya.

Ukweli ni kwamba maisha hayatusubiri,
Wakati unaendelea kuahirisha kuchukua hatua, maisha yanakupita, maisha yanasonga mbele kwa kasi ile ile.

Ubaya ni kwamba, hutaliona hilo kwa haraka, wewe utaona muda bado upo na unaweza kufanya hata kesho. Lakini siku moja unastuka na kukuta muda umeenda sana na huwezi tena kuchukua hatua.

Rafiki, kila unapoanza kufikiria kuahirisha kitu, jikumbushe hili, kwamba unaweza kuahirisha utakavyo, lakini maisha hayatakusubiri. Maisha yataendelea kwenda kwa kasi na hivyo wewe utaachwa nyuma.
Njia pekee ya kuweza kwenda na kasi ya maisha, ni kufanya kile ulichopanga kufanya, kwa wakati uliopanga kukifanya.

Usiahirishe kitu, labda kama huna mpango wa kukifanya yena, na jiambie wazi kwamba hutafanya tena.
Uwe na siku bora sana leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha