Mara ghafla kesho biashara yako haipo tena, huwezi tena kutoa kile ambacho umekuwa unatoa kwa wateja wako. Nini kitatokea kwa wateja wako ambao ulikuwa unawahudumia?
Ghafla tu huwezi tena kufanya kazi yako, huwezi kwenda kutoa ile huduma ambayo umekuwa unatoa, nini kitatokea kwa mwajiri wako na hata wale wanaotegemea huduma unayotoa?

Haya ni maswali ya kujiuliza siyo kwa ajili ya kujua una umaarufu au unategemewa kiasi gani, bali ya kujiuliza ili kujua kama kweli unachofanya kinagusa watu.
Dhumuni kubwa la maisha yetu, ukiacha malengo na mipango ya kawaida kama ya kupata fedha na vitu vingine, ni kugusa maisha ya wengine kwa namna chanya, kwa namna ambayo unawaacha wakiwa bora zaidi kuliko walivyokuwa.
Kama kupotea kwako ghafla hakumfanyi yeyote akuulizie, kama hakuna atakayekukosa kwa wakati ambao haupo, na kusema fulani angekuwepo mambo yangeenda vizuri, basi bado hujayagusa maisha ya wengine ipasavyo.
SOMA; UKURASA WA 964; Unahitaji Kuongeza Juhudi Kidogo Tu…
Kama kuwepo au kutokuwepo kwako hakuleti tofauti yoyote, basi hakuna mchango mkubwa ambao unaotoa kwa wale ambao wanategemea kile unachofanya.
Na kwa zama hizi tulizopo sasa, kama kuwepo au kutokuwepo kwako hakuna tofauti, basi huna watu unaoweza kuwategemea kwenye kile unachofanya, kwa sababu pia hakuna wanaokutegemea wewe.
Utakuwa unafanya kwa mazoea pekee, na kufanya kwa kubahatisha tu, lakini siyo kwa kutoa mchango mkubwa kwa wengine.
Usikubali chochote unachofanya kiwe cha kawaida kiasi kwamba hakuna anayekukosa kama haupo. Weka juhudi, weka ubunifu na weka kila unachoweza kuweka kwenye kile unachofanya, ili uweze kutoa thamani kubwa kwa wengine na wao wakutegemee wewe kwenye hicho unachotoa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog