Katika zama hizi za taarifa watu wamekuwa na mambo mengi sana ya kufanya. Watu wengi wanaimba wimbo wa niko bize, hakuna mtu anayeweza kusema yeye yuko huru, muda umekuwa ni mdogo kuliko mambo ambayo mtu anatakiwa kuyafanya.

Rafiki, watu wamekumbatia sana shughuli za kidunia nakusahau majukumu yao ya kindoa. Wanandoa wamekuwa wakikimbizana na shughuli mbalimbali wengine ndiyo hawana hata habari na wenza wao na familia kiujumla. Kazi ni muhimu kweli ndiyo msingi wa maendeleo lakini kazi isikufanye ukasahau majukumu yako ya kifamilia.

4d1bd-maadui2bwa2bmahusiano

Watu wameingia katika maisha ya ndoa lakini siyo wote wanaotimiza majukumu yao kama inavyotakiwa. Kitu pekee unachotakiwa kumpatia mwenzi wako katika zama hizi za taarifa basi siyo kingine ni muda. Muda umekuwa ni changamoto kubwa kwa wanandoa wengi,na hakuna uhusiano wowote unaojengwa bila ya kuwa na rasilimali muda. Muda ndiyo mtaji wa kwanza wa kupata chochote tunachotaka kupata.

Mpendwa msomaji, wanandoa wanatakiwa kupeana muda. Bila kupeana muda huwezi kujua changamoto za mwenzako, huwezi kujua anapitia nini, huwezi kujua hata siku yake imekwendaje. Lakini unapohakikisha kila siku unatenga muda wa kuwa na mwenzi wako wa ndoa inasaidia kujadiliana mipango yenu kwa ujumla inaendaje. Kama mnakosa muda wa kukaa pamoja na kushirikishana mambo mbalimbali mtawezaje kufika sasa kule mnakotaka kwenda?

Kuna ndugu mmoja alikuwa anamwambia mwenzake kuwa yeye kurudi nyumbani mapema hawezi anakaa baa mpaka muda ambao anajua akienda nyumbani familia imelala, hivyo hapo hata watoto hawapati muda bora na mzazi wao, na anasema akiondoka anaondoka wakati familia imelala. Hivyo hana muda hata wa kukaa na mwenzi wake wa ndoa.

SOMA; Jinsi Wanandoa Wanavyobomoa Ndoa Zao

Hivyo basi, unaweza kuajiri watu kukusaidia majukumu yako mengine lakini huwezi kuajiri mtu kukutimizia majukumu yako ya kindoa. Majukumu ya kindoa yanatimizwa na mwanandoa mwenyewe na siyo mtu mwingine. Kama mwandoa jukumu lako na kwanza ni kutumikia ndoa yako kwanza halafu ndiyo majukumu mengine. Lakini siku hizi mambo yamekuwa kinyume chake, visingizio vya muda vimekuwa ni vingi, kama unapata muda wa kukaa baa kwanini unakosa muda kukaa na familia au mwenzi wako? Usipotimiza majukumu yako ya kindoa unataka nani akusaidie?

Haijalishi umechoka au haujachoka kumbuka kumpa mwenzi wako wa ndoa muda.  Matatizo mengi yanatokea ni kwa sababu wanandoa hawapeani muda. Kuna kuwa kuna mwanya mkubwa ambao unatakiwa kuzibwa.

Hatua ya kuchukua leo, hakikisha unampatia muda mwenzi wako wa ndoa na kutimiza majukumu yako ipasavyo, unaweza kuajiri watu wa kukusaidia majukumu mengine lakini siyo majukumu yako ya ndoa ni kama vile uajiri mtu akusaidie kupiga’’ pushapu’’ ni kitu ambacho hakiwezekani kabisa. Mambo yako ya ndoa yakiwa vizuri hata utendaji wako wa kazi utakua mzuri katika eneo lako la kazi, lakini kama nyumbani pako hovyo basi jua kazi matatizo ya nyumbani yatakuathiri pia katika mambo yako ya kazi.

Kwahiyo, hakuna mahusiano yoyote yanayoweza  kukua na kuimarika bila muda. Muda ni mbolea nzuri ya kuhakikisha kila uhusiano wowote hapa duniani unakuwa vizuri. Maisha ya ndoa yanadai uaminifu hivyo ishi uadilifu katika ndoa yako na utafurahia maisha ya ndoa vinginevyo  ni mateso.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Deogratius Kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com , kessydeo@mtaalamu.net

Unaweza kutembelea tovuti yangu kwa kujifunza zaidi kila siku  ambayo ni www.mtaalamu.net/kessydeo .

Asante sana !