Mtu anaposema hajaingia kwenye biashara kwa sababu hajui biashara gani afanye, huwa napata wakati mgumu sana kuelewa. Kwamba huyu mtu anaishi kwenye jamii ambayo hakuna biashara yoyote inayofanyika? Au anaishi kwenye jamii ambayo watu hawana shida wala mahitaji yoyote?

Ukichunguza kwa ndani watu hao wapo kwenye jamii yenye kila aina ya biashara na watu wenye kila aina ya mahitaji, lakini wao wana tatizo moja, wanataka kufanya biashara ambayo ni ya kipekee, ambayo haijawahi kufanyika kabisa.

Taaluma

Na hapo ndipo wanapojiandaa kushindwa kabla hata hawajaanza. Au hata kama wataanza, safari itakuwa ngumu sana kwao kiasi kwamba hawataweza kupiga hatua kubwa.

Hakuna mtu anategemea wewe ufanye kitu kipya kabisa, kitu ambacho hakijawahi kufanya kabisa na mtu mwingine yeyote. Na tena ukipata na kufanya kitu cha aina hiyo, wengi hawatakuelewa na utakuwa mzigo mzito zaidi kwako.

SOMA; UKURASA WA 1151; Wazo Lisilofanyiwa Kazi Ni Maumivu…

Chochote unachotaka kufanya, sehemu ya kwanza kuanzia ni kwa wale ambao tayari wanafanya, kuanza na uhitaji wa watu. Kisha angalia ni namna gani unaweza kufanya kwa ubora zaidi, kuangalia ni hatua ipi unayoweza kupiga zaidi ya wengine wanavyopiga. Siyo kuanza kitu kipya kabisa, bali kuboresha zaidi kile ambacho tayari watu wanakihitaji.

Chochote unachotaka kufanya kwenye maisha yako, anza na kile ambacho tayari kinafanyika. Anza na kile ambacho tayari watu wanahitaji, anza na matatizo ambayo watu wanayo. Watu hawakimbilii upya na upekee wa kitu, bali wanakimbilia kile kinachotatua matatizo yao, kinachotimiza mahitaji yao.

Ukikwama kwa sababu hujapata cha kipekee cha kufanya, labda unaficha uvivu wako, au hutaki tu kufanya. Lakini kama upo tayari kufanya, basi anza kufanya, kwa kuboresha zaidi kinachofanyika na kinachohitajika na wengine.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog