No one is laughable who laughs at himself. – Lucius Annaeus Seneca

Hongera mwanamafanikio kwa nafasi hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni fursa ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa kwenye maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari UKIJICHEKA HAKUNA ATAKAYEKUCHEKA…
Kile ambacho hatupo tayari kujifanyia sisi wenyewe, tunawapa wengine nafasi ya kutufanyia.
Kama hutajikosoa mwenyewe, utawapa wengine nafasi ya kukukosoa.
Kama hutajitawala mwenyewe, utawapa wengine nafasi ya kukutawala.
Kama hutajitumia mwenyewe, utawapa wengine nafasi ya kukutumia.
Na kama hutajicheka wewe mwenyewe, utakuwa umewapa wengine nafasi ya kukucheka.

Ni muhimu uwawahi wengine, uweze kufanya kabla hata hawajafikiria kufanya kitu fulani juu yako.
Ukishajicheka wewe mwenyewe, wengine hawapati tena nafasi ya kukucheka.
Ukishajikosoa na kuchukua hatua ya kuwa bora zaidi, wengine hawapati tena hiyo nafasi.
Ukishajitumia wewe mwenyewe, wengine hawakukuti upo upo tu na kukutumia.
Hii ndiyo siri kubwa ya kupiga hatua na kuepuka wengine kuwa kikwazo kwako, wawahi kwa lolote wanaloweza kufikiria kifanya juu yako.

Usikubali hatima ya maisha yako yawe kwenye mikono ya mtu mwingine yeyote.
Hakikisha unaona kila nafasi, kila udhaifu na kila changamoto inayokukabili, kabla mtu mwingine yeyote hajaiona.
Na hapo ndipo utakapokuwa kiongozi mkuu wa maisha yako, ukijua yanaenda wapi na unafikaje kule unakoenda.

Jicheke, jikosoe, jisimamie, jitumie, jiadhibu na utawanyima wengine fursa ya kufanya hayo kwako.
Ukawe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha