Mazoea ni sumu mbaya ambayo imekuwa inawasahaulisha watu kule walipotoka na kujikuta wanafanya makosa ambayo yanawarudisha kule walikotoka.

Chukulia mfano wa mtu ambaye hana kazi, na maisha ni magumu, anaomba sana apate kazi, hata kama ni kazi yoyote na ataifanya kwa moyo kwa malipo yoyote.

Kwa kuwa mawazo hujenga, basi mtu huyo anapata kazi ambayo huenda siyo bora sana kwake, lakini kwa kuwa hana kazi siyo mbaya kuanzia, na pia kipato siyo kikubwa kama wengine wanavyopata, lakini pia kwa kuwa hana kipato kabisa, basi siyo vibaya kuingiza kipato hicho.

Mambo ya Kawaida

Lakini sasa, jambo la kushangaza linatokea, kadiri mtu anavyozoea kazi, ndivyo anaanza kujipa hadhi, ndivyo anavyoanza kuona kazi ile siyo ya hadhi yake, ndivyo anavyoona kwamba kipato anachopata siyo ngazi yake.

SOMA; UKURASA WA 946; Njia Bora Ya Kuzishinda Mashine Na Teknolojia Mpya…

Anaanza kukosa hamasa na msukumo wa kazi, anaanza kufanya kwa mazoea na kwenda kwa mtazamo, kwanza nalipwa kiasi gani. Kinachotokea mtu anapoteza kazi hiyo, huku hana maandalizi ya kupiga hatua zaidi na hivyo kurudi nyuma.

Ndiyo maana ni muhimu sana kwa kila mmoja wetu, kukumbuka kule tulipotoka pale tunapoanza kuona tumezoea kitu. Pale tunapoanza kufikiria kwamba tulipo siyo ngazi yetu, hebu kwanza tuangalie ngazi tuliyotoka.

Simaanishi kwamba ukubali kufanya kazi za hovyo au ukubali kupokea kipato kidogo kwa sababu tu ndiyo zimekutoa, bali ninachotaka kukukumbusha ni kwamba, usijenge mazoea kwenye kitu chochote kile.

Unaweza kupiga hatua utakavyo, lakini siyo kwa mazoea. Utapiga hatua kwa kuweka juhudi kubwa, kwa kukazana zaidi kwa kuanzia pale ulipo sasa, na siyo popote pengine. Kama hutaweza kutumia pale ulipo sasa, na kama utaendekeza mazoea, kitakachotokea ni kwamba utapoteza.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog