“Whosoever desires constant success must change his conduct with the times.” -Niccolo Machiavelli

Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana kwetu,
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa mafanikio, NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wetu kwa mwaka huu, TATUA, AMUA NA ONGOZA vinatuwezesha kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari KUPATA MAFANIKIO YA KUDUMU, BADILIKA.
Wapo watu ambao wanachukua hatua fulani kwenye maisha yao, ambazo zinawawezesha kifanikiwa, kutoka chini na kufika juu.
Lakini baada ya kupata mafanikio hayo kidogo, yanakuwa sumu kubwa kwao, hawaendelei kufanikiwa tena na kinachotokea ni wanashuka chini badala ya kupanda juu.

Hili limekuwa linachangiwa na mambo mawili makubwa,
La kwanza ni kufanya kwa mazoea na kutokubadilika. Kwa kuwa mtu alishaona njia fulani ndiyo imempa mafanikio, basi anaendelea kufanya vile vile hata kama hakileti tena majibu anayotarajia.
Dunia inabadilika na kila kitu kinabadilika, kilichokufikisha hapo ulipo sasa, siyo kitakachokufikisha kule mbali zaidi unakotaka kufika.
Badilika, kwa kuwa dunia inabadilika, kama hubadiliki unarudi nyuma.
Kama leo ni sawa na jana, basi leo umerudi nyuma, kwa sababu dunia imeenda mbele na wewe umesimama.

Jambo la pili linalofanya mafanikio yawe sumu ni kuogopa kujaribu mambo mapya kwa hofu ya kushindwa na kupoteza.
Watu wakipata mafanikio kidogo wanataka kuyalinda yasipotee, kitu ambacho siyo kibaya.
Ila sasa wanapoogopa kuchukua hatua kabisa, kwa sababu wanahofia kupoteza kile walichonacho, ndiyo wanajizuia kabisa kufanikiwa zaidi na wanachangia kushindwa kwao.
Unahitaji kubadilika, unahitaji kuendelea kujaribu mambo mapya, unahitaji kuendelea kujaribu vitu hatari.

Mafanikio siyo kufanya kile ambacho kimekufikisha ulipo, au kuepuka kupoteza, mafanikio ni kujaribu mambo mapya, kuwa kwenye hatari ya kupoteza lakini ukapata zaidi.
Ili kuwa na mafanikio ya kudumu, mara zote badilika.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kipekee, tofauti kabisa na jana.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha