As long as you live, keep learning how to live – Lucius Annaeus Seneca

Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Leo ni siku nyingine mpya, siku bora na ya kipekee ambapo tunapata nafasi ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa sana leo.
Na kwa mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA, mwaka huu 2018 utakuwa wa kipekee sana kwetu.

Asubuhi ya leo tutafakari KUISHI NI KUJIFUNZA JINSI YA KUISHI…
Siri moja kubwa ya maisha ni kwamba, hakuna mwenye uhakika na chochote, hakuna anayejua kwa hakika ni jinsi gani ya kuishi haya maisha hapa duniani.
Hivyo kila siku ambayo tunaipata, ni nafasi ya kujifunza jinsi ya kuishi vizuri.

Inakuwa vigumu kujua kwa hakika kila kitu kwa sababu mazingira yanabadilika na pia tunakutana ma watu tofauti tofauti.
Na kila wakati kwenye maisha, kuna changamoto mpya.
Ukimaliza kutatua changamoto moja, unakuta nyingine kubwa zaidi inajitokeza, na yenyewe ni ya kutatua pia.

Hivyo kila unapianza siku, ianze kwa mtazamo wa kujifunza, ianze ukijua leo utakutana na hali ambazo hukutegemea kukutana nazo, na hiyo itakuwa sehemu ya wewe kujifunza.

Pia utakutana na watu ambao watajaribu kufanya ubaya kwako bila ya sababu yoyote. Labda watajaribu kukuibia, kukutapeli, kukudanganya, kukudhulumu na hata kukukasirisha bila ya sababu yoyote.
Lazima ujifunze kuwazuia watu wa aina hii wasiharibu siku yako, ujifunze na kisha kusonga mbele.

Yeyote anayeweza kufikiria kwamba ameshayajua maisha, hana tena cha kujifunza na amefika kwenye kilele cha kila kitu, anakuwa ameanza rasmi njia ya kuanguka na kushindwa.
Kuishi leo ni nafasi ya kujifunza kuishi vizuri zaidi.
Tumia vizuri darasa la kila siku na hutabaki pale ulipo sasa.

Siku yako ya leo ikawe ya kipekee sana, ujifunze yale muhimu na kuyatumia kwenye maisha yako.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha